JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
|
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU MAAMUZI YA RUFAA ZA MAPINGAMIZI YA
WAGOMBEA WA UBUNGE NA UDIWANI KATIKA UCHAGUZI MDOGO
Kwa mujibu wa kifungu cha
40 (6) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume ilipokea Rufaa moja
ya kupinga Uteuzi wa Mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF) katika Uchaguzi Mdogo
wa Bunge Jimbo la Dimani – Zanzibar.
Rufaa hiyo ilikatwa na
Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bwana
Juma Ali Juma akipinga Maamuzi ya Msimamizi
wa Uchaguzi Jimbo la Dimani aliyemthibitisha Mgombea wa Chama Cha Wananchi
(CUF) Bwana Abdul Razak Khatib Ramadhani
kuwa ni mgombea halali.
Rufaa hiyo ilikuwa na sababu mbili ambazo ni:-
(i) Hakurudisha Fomu za Uteuzi kwa
mujibu wa masharti yaliyowekwa na sheria na (ii) Hakudhaminiwa na Chama cha Siasa kugombea Ubunge. Katika kikao
chake cha leo tarehe 30 Desemba, 2016, Tume imepitia Rufaa hiyo na kuona sababu
zilizotolewa na mkata Rufaa hazina nguvu ya kisheria, kwa kuwa, Mgombea wa CUF
amerudisha Fomu za
Uteuzi kwa mujibu wa sheria na taratibu. Pia, Fomu zake za
Uteuzi zimesainiwa na kugongwa muhuri wa Katibu wa Wilaya ya Magharibi B. Kwa
mantiki hiyo, Tume imekubaliana na Uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la
Dimani – Zanzibar. Hivyo, Mgombea wa CUF
amekidhi vigezo na uteuzi wake ni halali na aendelee na kampeni za kugombea
nafasi ya Ubunge wa Jimbo hilo.
Aidha, kwa mujibu wa
kifungu cha 44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292,
Tume imepokea Rufaa tatu; kutoka Kata ya Kijichi – Halmashauri ya Manispaa ya
Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, Kata ya Misugusugu – Halmashauri ya Mji wa Kibaha,
Mkoa wa Pwani na Kata ya Ihumwa – Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Mkoa wa
Dodoma.
Kata ya Misugusugu
Halmashauri ya Mji Kibaha, Rufaa ilikuwa ni ya Mgombea wa CHADEMA Bwana Gasper Melkiory Ndakidemi dhidi ya mgombea wa Chama cha Mapinduzi CCM
Bwana Bogasi Hussen Ramadhani.
Katika Kata ya Kijichi, Rufaa
ilikuwa ni ya mgombea wa CUF Bi. Khadija Abdallah Shamas dhidi ya mgombea
wa CHADEMA Bwana Fredrick Felician Rugaimukamu.
Kata ya Ihumwa Rufaa
ilikuwa ni ya Mgombea wa CHADEMA Bwana
Magawa Edward Juma dhidi ya maamuzi
ya Msimamizi wa Uchaguzi.
Tume katika kikao chake cha
leo tarehe 30 Desemba, 2016 imepitia Rufaa zote na imeamua ifuatavyo:
Rufaa ya mgombea wa CHADEMA Bwana
Gasper Melkiory Ndakidemi katika Kata
ya Misugusugu Halmashauri ya Mji Kibaha na ya mgombea wa CUF Bi. Khadija Abdallah Shamas katika Kata ya Kijichi, hazina mashiko ya kisheria na zimekataliwa. Hivyo, Tume inakubaliana na Maamuzi ya
Wasimamzi wa Uchaguzi wa Halmashauri hizo na wagombea waendelee na Kampeni kwa
mujibu wa Ratiba.
Kuhusu Rufaa ya Mgombea wa
CHADEMA kutoka Kata ya Ihumwa, Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma. Tume, imepokea
barua ya Msimamizi wa Uchaguzi, Manispaa ya Dodoma, ikiwa imeambatishwa na barua
ya Mgombea wa CHADEMA kuiondoa Rufaa yake na kwamba anakubaliana na maamuzi ya
Msimamizi wa Uchaguzi ambayo yalimuengua. Pia, leo Tume imepokea barua za
kujitoa Ugombea za wagombea wa CHADEMA na ACT - WAZALENDO katika Kata ya
Ihumwa. Kwa maana hiyo Rufaa iliyokuwa imekatwa na mgombea wa CHADEMA Kata ya
Ihumwa imeondolewa kwa kuwa mkata Rufaa ameiondoa na amejitoa ugombea kabla
haijasikilizwa.
Mwisho, Tume
inavisisitiza Vyama vya Siasa, Wagombea na Wananchi wote wa maeneo yenye
Uchaguzi Mdogo kufanya Kampeni za kistaarabu kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na
Maadili ya Uchaguzi.
Imetolewa na:-
Jaji Mkuu (Mst. Znz) Hamid
M. Hamid
MAKAMU MWENYEKITI
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
30/12/2016
Comments
Post a Comment