KIKWETE AMKABIDHI KIJITI MAGUFULI
Mwenyekiti wa CCM Mstaafu na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete(kushoto) akimkabidhi Mwenyekiti mpya Rais Dk. John Magufuli,ripoti ya chama ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka jana baada ya kumtangaza kwenye mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho mjini Dodoma
Wakikumbatiana kwa mara ya mwisho kama mwenyekiti
Mwenyekiti mstaafu wa CCM,Jakaya Kikwetena Mwenyekiti mpya Rais Dk. John Magufuli (kulia), wakiwapungia wanachama wa chama hicho baada ya kumtangaza kwenye Mkutano Mkuu Maalum Dodoma
Wakikumbatiana na rais wa zanzibar
Magufuli ni wa kuogopwa
*Asema walioimba wana imani
na Lowassa kwake yeye wangepotea ndani ya nusu saa
*Asema hana uvumilivu,
atangaza kuifumua CCM, awawashia taa nyekundu wasaliti
*Sasa kuihamishia Serikali
yake Dodoma ndani ya miaka minne
UNAWEZA kumwelezea Rais
John Magufuli kama rais anayetisha, anayepaswa kuogopwa au pengine kuhofiwa
kutokana na kauli anazozitoa hadharani kila anapopata fursa ya kuhutubia.
Hali hiyo ilithibitika
jana mjini Dodoma saa chache baada ya kutangazwa mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Mkutano Mkuu Maalumu ulioitishwa ili
kumkabidhi nafasi hiyo.
Akihutubia Rais Magufuli
kwa mara nyingine alitoa kauli nzito na tata ambazo zilikuwa zinapeleka ujumbe
si kwa wana CCM tu waliokuwa wakimsikiliza ukumbini humo bali pia kwa watu
waliokuwa wakifuatilia Mkutano Mkuu Maalumu huo kupitia vyombo vya habari.
Miongoni mwa kauli hizo
ni pamoja na ile aliyoitaja mwanzoni kabisa katika hotuba yake hiyo akieleza
kushangazwa na kile alichokiita uvumilivu usiomithilika wa mtangulizi wake Rais
mstaafu Jakaya Kikwete.
Akitoa mfano Magufuli
alilitaja tukio la baadhi ya wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambao mwaka jana wakati wa mchakato wa
kumtafuta mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho kwa njia ya wimbo walitangaza
kuwa na imani na aliyepata kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
Kwa maneno yake
mwenyewe, Magufuli alisema: “Na mimi kwa kweli najiona nina changamoto kubwa
kwasababu moyo wako huo wa uvumilivu sina, hakika mimi sijui kama ninaweza
nikavumilia hivyo.
“Na mimi nasema kwa
dhati kabisa Mwenyekiti mstaafu, siku ile ulipoingia kwenye mkutano ukakuta
watu wanaimba wana imani na mtu fulani, siku hiyo hiyo hata robo au nusu
wangepotea. Kwasababu ninajaribu kuuliza moyo wangu na kwa kumtanguliza Mungu
kwamba kingetokea hicho kilichotokea kwako, sifahamu,” alisema Rais Magufuli.
Katika hilo, Rais Magufuli
aliwaomba wajumbe wa mkutano huo kumuombea ili angalau awe na nusu ya uvumilivu
wa Kikwete.
KUIFUMUA CCM
Katika
hatua nyingine Rais Magufuli ametangaza kufanya mapinduzi makubwa ya kimfumo
ndani ya CCM ikiwa ni pamoja na kukomesha uongozi unaopatikana kwa njia ya
rushwa.
Magufuli ambaye amekuwa
akijinasibu kupambana na rushwa na ufisadi, alikitaja waziwazi chama hicho kama
moja ya taasisi zinazotajwa kuongoza kwa rushwa licha ya kukatazwa katika ahadi
ya tatu ya CCM pamoja na kifungu cha 18 cha Katiba ya CCM.
“Niligombea urais niliyaona huko Iringa wakati
wa kutafuta wadhamini, wilaya yote ilikuwa imenunuliwa ilibidi nisafiri kwenda
ndani huko vijijini. Fedha imekuwa kigezo cha mtu kupata uongozi…ukitaka urais
kiasi fulani, ubunge kiasi fulani, diwani kiasi fulani. Tumekuwa tukipoteza
sehemu nyingine kuchagua wenye fedha badala ya anayekubalika,” alisema
Magufuli.
Alisema amedhamiria
kukomesha jambo hilo na kwamba mtu atakayetoa rushwa hatachaguliwa wala
kupitishwa kwa mujibu wa kanuni ambazo alikabidhiwa jana na Mwenyekiti mstaafu.
Akilisisitiza hilo Rais
Magufuli alimwambia Kikwete: “Ulionesha mfano rafiki yako kabisa alipoonesha
ufisadi na rushwa ulimchinjia mbali na kama ingekuwa kwa rushwa nisingekuwa
rais, sasa ole wao nitakapokuwa Mwenyekiti. Ukijipanga kuchukua uongozi kwa
pesa utatumikia pesa zilizokuweka madarakani,” alisema Mwenyekiti huo.
Mwenyekiti huyo
aliwataka wana-CCM kuonesha mfano katika uchaguzi wa ndani utakaofanyika
mwakani kwa kutotoa takrima.
Kuhusu wasaliti
Magufuli alisema ni heri kuishi na mchawi lakini si msaliti huku akisisitiza
katika uongozi wake hawana nafasi na kama wapo watubu kuanzia jana vinginevyo
wawapishe.
“Hatuhitaji CCM pandikizi, CCM masilahi, nahitaji
CCM ambao siku zote usiku, mchana, mvua ikinyesha, njaa wapo…sihitaji ndumilakuwili,
masalia ambao wako kwa ajili ya mtu, nahitaji watu watakaotulia…nataka kuona
CCM ya watu wote wakiwemo wanyonge, nataka kuona CCM inayojitegemea si
inayotegemea wafadhili,” alisisitiza.
Awali
Rais Magufuli mara baada ya kuchaguliwa alikabidhiwa vitabu
vinne na Mwenyekiti mstaafu Kikwete ambavyo alisema vimebeba uchunguzi
walioufanya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Alisema vitabu hivyo
vimeeleza walivyofanikiwa na pale waliposhindwa na waliowaangusha.
Pamoja na hilo, Rais
Magufuli aliahidi kukifumua na kukiunda upya chama hicho kwa kuondoa vyeo
visivyokuwa na tija hasa katika zama hizi za ushindani wa kisiasa.
Magufuli alilitaja
kundi ambalo litaathirika kuwa ni pamoja na chipukizi ambao alisema hawana
sababu ya kujihusisha na masuala ya chama kutokana na umri wao wa miaka 8-15
unaowaruhusu zaidi kuwa shuleni.
“Chipukizi kuitumikia
CCM badala ya kusoma, kama akiwepo chipukizi wa CCM akianzishwa wa Ukawa, UDP,
TLP, NCCR na umri wake ni miaka 8-15 hawa watoto watasoma? Najaribu kutoa
changamoto,” alisema Magufuli.
Kundi lingine ambalo
alisema litaondoka ni Makamanda wa vijana ambao alidai wanapatiwa uongozi ni
wale wenye pesa.
Vyeo vingine ambavyo
alisema vitaondolewa ni pamoja na walezi wa Umoja wa Wanawake (UWT), washauri
ndani ya Jumuiya ya Wazazi akidai kuwa vyeo hivyo vinachochea migogoro badala
ya kuitatua.
Alisema kumekuwa na
mrundikano wa vyeo ndani na nje ya CCM ambapo unakuta Waziri lakini bado ni
Kamanda wa vijana.
“UWT, Umoja wa Vijana
na Jumuiya ya Wazazi tutaziimarisha sasa, masilahi ya wafanyakazi ndani ya CCM
nitayaangalia. Sitapenda wawe ombaomba na wanapokwenda kuomba ndio hao wenye
safari za matumaini huingia huko,” alisema Mwenyekiti huyo.
Akizungumzia mali za
CCM, Magufuli alisema kitaundwa kikosi kuzihakiki huku akimpa jukumu hilo
Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana ambaye alimtangaza kuendelea naye hadi hapo
atakapoamua vinginevyo.
Alisisitiza kuwa chini
ya Kinana, makatibu wote wa ngazi za chini waorodheshe mali za chama hicho.
Pamoja na hilo, Rais
Magufuli aliibua hoja ya wanachama wa CCM kulipa ada akiwataka kufanya hivyo
tena kwa njia ya kielektroniki pamoja na kuondoa wafanyakazi hewa na kuongeza
idadi ya wanachama hasa kundi la vijana kwa zaidi ya iliyopo sasa ambayo ni milioni
8.7.
Serikali
kuhamia Dodoma
Magufuli
pia alitumia mkutano huo kueleza azma yake ya kuihamishia Serikali Dodoma.
Mwenyekiti huyo mpya ambaye
alipata asilimia 100 ya kura za ndio katika kura zaidi ya 2,000 zilizopigwa na
wajumbe hao, aliahidi kuwa atahakikisha anahamishia Serikali yake Dodoma ndani
ya miaka minne iliyobaki.
Akisisitiza suala hilo
lililowashinda marais wote wanne waliopita alisema yeye mwenyewe atakuwa wa
kwanza kuhamia Dodoma na kwamba Makamu wake wa Rais na Waziri Mkuu hawatakuwa
na jinsi nao itabidi wamfuate.
“Wale wateule wangu na
mimi mwenyewe tujipange kuhamia Dodoma, tusitafute kisingizio, kama wajumbe
wote wa CCM wanalala Dodoma wanakula na kunywa, Bunge liko Dodoma sioni sababu
kukaa Dar, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri wote watakuja huku,” alisema Rais
Magufuli.
Alisema pia sherehe za
Mapinduzi mwakani zitafanyika mjini Dodoma na kwamba Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Nyerere hakukosea kuamua Makao Makuu ya nchi kuwa huko.
Rais Magufuli alitumia
mkutano huo kuwaeleza wajumbe hao mambo ambayo Serikali yake imeyafanya ikiwemo
kutoa elimu bure, kuagiza ndege mbili zitakazowasili Septemba, kujenga Reli ya
Kati kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma na Rwanda na kwamba tayari fedha kiasi
cha Sh trilioni 1 zimetengwa.
Pia alisema tayari
mpango wa maendeleo wa taifa umepitishwa na umeanza kufanya kazi mwaka huu wa
fedha kwa kutumia kiasi cha Sh trilioni 29.5 huku asilimia 40 ikienda kwenye
maendeleo.
MWISHO
Comments
Post a Comment