DC MBEYA ALIKOLOGA
Na Pendo
Fundisha Mbeya.
MKUU wa
Wilaya ya Mbeya, Munasa Nyiremba Sabi,amesababisha mtafaruku mkubwa kwenye
vituo vya kupigia kura baada ya kuandaa mawakala na kuwajaza vituoni kwa tiketi
ya chama cha NRA huku wakiwa ni wanachama wa CCM.
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili katika vituo mbalimbali umegundua kuwepo na mawakala
waliosimamiwa na mkuu wa Wilaya hiyo baada ya kuwaita kwenye chuo kikuu
cha Mzumbe na kuwapatia barua za uwakala ambazo zimekataliwa na Tume ya
uchaguzi kutokana na dosari zilizojitokeza.
Baadhi ya
vituo vilivyotembelewa na gazeti hili, viliwakuta mawakala wa NRA ambao
ilibainika kuwa hawajaapishwa wala kuthibitishwa na tume ya Uchaguzi wala kuapa
hali iliyotiliwa shaka na mawakala wa CCM na Chadema ambao hawakufahamu uwepo
wa mawakala hao.
Katika
kufuatilia sakata hilo, iligundulika kuwa barua za utambulisho zilitolewa na
Mkuu wa Wilaya kwa kuandaa kundi la vijana wanaokitii chama hicho lakini barua
ya utambulisho ilitolewa ikionyesha kuwa ni mawakala wa NRA.
Kwamujibu
wa taratibu mawakala wote waliokuwa kwenye vituo vya kupigia kura walikuwa na
barua za utambulisho toka kwenye vyama vyao na barua ya Tume iliyowaidhinisha
kuwa mawakala kwa kula kiapo cha utii na kupata ridhaa ya kufanya kazi hiyo.
Msimamizi
wa uchaguzi Jimbo la Mbeya mjini, Dkt. Samweli Lazaro alipohojiwa kuhusu tukio
hilo alisema kuwa chama hicho hakina mawakala kwa kua Tume ya uchaguzi
haijapata barua za kuwatambulisha mawakala hao wala kutoa barua za Tume za
kuwathibitisha kufanya kazi hiyo.
“Ofisi
yetu kama Tume haina taarifa na chama hichi cha NRA, kwani hatujapokea
barua ya aina yoyote na wala mawakala hao hawajaapishwa hivyo sisi
hatuwatambui,” alisema Lazaro.
Aidha,
baadhi ya mawakala wa NRA ambao walikutwa na barua hizo, wakiwa ndani ya vituo
vya kupigia kura na baadhi yao kuhojiwa, walimtaja Mkuu wa Wilaya hiyo Munasa
Sabi kuwa ndiye aliyewakabidhi barua hizo na kuwaandikia Kata wanazotakiwa
kwenda kusimamia zoezi hilo huku akitambua wao ni wanachama wa CCM.
Nuru
Leonard aliyekutwa katika kituo cha Ilemi A akiwa na barua yenye kumbukumbu
namba NRA/HQ-PARTY AGENTY/2015 iliyosainiwa na Hassan K Halmas kuwa ni katibu
Mkuu wa chama hicho ikimtambulisha wakala huyo ambaye alipohojiwa alisema kuwa
yeye ni wakala wa CCM.
Utambulisho
huo, ulishitukiwa na wakala halisi wa CCM aliyekuwa katika kituo hicho bila
kujua kwamba mwenzake anayemkana ni pandikizi la chama chake kwenye kituo cha
kupigia kura.
Wakala
mwingine wa NRA Witnes Nguwila kituo cha mtaa wa Masewe alipohojiwa alisema
kuwa yeye ni mwana CCM na kwamba waliitwa na Mkuu wa Wilaya katika Chuo Kikuu
cha Mzumbe na kukabidhiwa barua hizo pamoja na kulipwa posho ya shilingi 40,000
pamoja na kuelekezwa kazi watakayoenda kuifanya ikiwa ni kuhakikisha wanapiga
kura kwa kujaza fomu maalum kama mawakala.
Samweli
Mwandishe, aliyekutwa katika kituo cha Irowe namba moja naye akiwa na barua ya
NRA na alipohojiwa na waandishi wa habari mbele ya askari polisi alijibu kuwa
yeye ni mwanaCCM na yupo kwenye kituo hicho kama wakala wa NRA.
Akijibu
tuhuma zilizotolewa dhidi yake Mkuu wa Wilaya hiyo Munasa Nyiremba Sabi alisema
kuwa uongozi wa chama hicho ndio uliomfuata na kumuomba awasaidie kupata
mawakala kwakua katika Jiji la Mbeya hawana mawakala waliowapata.
“Nakiri
kufanya kazi hiyo kwakua nilifuatwa nikaitwa nikaenda kwenye chuo cha mzumbe
ambako niliwasaidia kupata mawakala huku zoezi zima likiwa chini ya usimamizi
wangu kama nilivyoombwa,”alisema.
Hata
hivyo,mbali na hali hiyo iliyojitokeza kwa ujumla maeneo mengi yenye vituo vya
kupigia kura vipatavyo 608 katika Jiji la Mbeya ilikuwa shwari na wananchi baada
ya kushiriki zoezi hilo wengi walirejea makwao kuendelea na shughuli zao.
Mwisho.
Comments
Post a Comment