Kanali (mst) Ayubu Shomari Mohamed Kimbau, aaga dunia leo
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512,
2116898
E-mail: ikulucommpress@googlemail.com
Website : www.Kikuyu.go.tz
Fax: 255-22-2113425 |
|
PRESIDENT’S OFFICE,
STATE
HOUSE,
1 BARACK OBAMA ROAD,
11400
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu
za rambirambi kuombeleza kifo cha mwanasiasa mkongwe na aliyekuwa mbunge wa muda
mrefu wa Jimbo la Mafia, Mkoa wa Pwani, Kanali (mst) Ayubu Shomari Mohamed Kimbau, ambaye aliaga dunia asubuhi ya
leo, Jumapili, Agosti 30, 2015 katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Katika
salamu za rambirambi alizomtumia Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Eng. Evarist Ndikilo,
Rais Kikwete ameeleza kusikitishwa kwake na taarifa za kifo cha Mzee Kimbau ambaye
kwa miaka mingi alikuwa Mbunge wa Jimbo la Mafia kupitia Chama cha Mapinduzi
(CCM).
Amesema
Rais Kikwete katika salamu zake: “Nimesikitishwa na taarifa za kuaga dunia kwa
Mzee Ayubu Kimbau ambaye nimejulishwa kuwa amefariki asubuhi ya leo katika Hospitali
ya Muhimbili. Mzee Kimbau atakumbukwa sana kwa utumishi wake wa umma na uzalendo
wake kwa taifa lake kuanzia alipokuwa katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambako alipanda nafasi
hadi kufikia cheo cha Kanali na baadaye katika uwakilishi wa wananchi wa Mafia
katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
“Kupitia
kwako, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, naungana na wananchi wote wa Mafia na wa mkoa wa Pwani
kuomboleza kifo cha mmoja wa magwiji wa siasa na wauwakilishi wa wananchi katika
nchi yetu. Nawaombeni mpokee salamu zangu za dhati ya moyo wangu katika kuomboleza
kifo hiki,”
amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Aidha,
kupitia kwako naitumia familia ya Kanali Kimbau salamu zangu nyingi za pole.
Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa na kuwa msiba wao ni msiba wangu.
Naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu na nawaombea kwa Mwenyezi Mungu
aweze kuwapa nguvu, uvumilivu na subira. Naungana nao pia kumwomba Mungu aiweke
peponi roho ya Marehemu Kanali Ayubu Shomari Mohamed Kimbau. Amen.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
30 Agosti,
2015
Comments
Post a Comment