MAHAKAMA KUU NCHINI KENYA YALIGOMEA BUNGE NA RAIS
Serikali ya Kenya Kenya imepata pigo jingine baada ya mahakama kuu kuharamisha baadhi ya vipengee katika sheria ya usalama iliyolega kukabiliana na ugaidi.
Muungano wa upinzani nchini Kenya na mashirika mbalimbali yalienda mahakamani mwaka uliopita baada ya bunge kupitisha sheria hiyo.
Jopo la majaji watano wa mahakama kuu wakiongozwa na Jaji Isaac Lenaola waliharamisha vipengee 10 kikiwemo kile kinachohusu uhuru wa vyomo vya habari na haki ya washukiwa wanapofikishwa mahakamani.
Uamuzi huo ulichukua takriban saa tano na majaji wakaamua kuwa baadhi ya vipengele havikuaambatana na katiba.
Katika uamuzi wao walikubali kuwa Kenya imekumbwa na visa vingi vya ugaidi katika miaka mitatu iliyopita na inastahili kuwa na mbinu za kuisaidia kukabilana na tatizo hilo…
hata hivyo majaji walisema kuwa haki za washukiwa zinatakiwa kuzingatiwa.
Mengine yaliyoharamishwa yanajumuisha kuwalazimisha wanahabari kuchapisha baadhi ya picha ya ruhusa ya polisi,
kuwazuilia washukiwa bila kuwapa nafasi ya kujitetea na kuwanyima dhamana washukiwa wakipelekwa mahakamani bila sababu za kuridhisha.
Aidha mahakama imeharamisha jaribio la serikali kutaka kuweka kiwango cha wakimbiai wanaotahili kuhifadhiwa Kenya kutozidi laki moja na nusu na kusema kuwa ni kinyume cha mkataba wa Geneva.
Ni uamuzi uliofurahiwa na muungano wa upinzani CORD.
Wakili wa serikali Njoroge Mwangi amesema serikali itakata rufaa
Sheria hiyo tata ilipitishwa bungeni tarehe 14 Desemba mwaka uliopita katika kikao kilichokumbwa na vurumai huku wabunge wakipigana hadharani.
Baada ya hapo Rais Uhuru Kenyatta alitia saini mswada huo na kuufanya sheria tarehe 22 mwezi huo kisha chama cha CORD kikakwenda mahakamani kikidai kuwa sehemu nyingi za sheria hiyo zilikiuka katiba.
Mashirika mengine yalijiunga katika mchakato huo na kujumuishwa katika kesi ikiwemo tume ya kitaifa ya kutetea haki za binadamu.
Awali jaji wa mahakama kuu alikuwa amezuia vipengele vinane vya sheria hiyo kutotekelezwa na kumchochea mkuu wa sheria kukataa rufaa lakini bado mahakama ya rufaa ikashikilia uamuzi wa mahakama kuu.
Kinachosubiriwa kwa sasa ni kutazama mwelekeo utakaochukuliwa kwa misingi kuwa CORD inasema itaenda kwa mahakama ya rufaa vile vile kutaka sehemu nyingine za sheria hizo kuchunguzwa.
Comments
Post a Comment