YANGA NA ZAM FC 2-2 TAIFA

 Wachezaji wa Yanga, wakishangilia baadan ya kusawazisha katika mchezo wao na timu ya Azam FC uliofanayika uwanja wa taifa jijini dar es salaam na kutoka 2-2



Mshambuliaji wa Yanga Kpah Sherman, (kushoto) akiwania mpira na beki  wa Azam Himidi Mao, katika mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana.  timu hizo zilitoka sare 2-2
 Winga wa Yanga Simon Msuva, (kushoto) akiwania mpira na beki wa Azam Pascal Wawa, katika mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana.  timu hizo zilitoka sare

Mshambuliaji wa Yanga Amisi Tambwe (kushoto) akimtoka beki wa Azam Erasto Nyoni, katika mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana.  timu hizo zilitoka sare 
 Tambwe. akiwatoka wachezaji wa Azam
Akianguka baada ya kupigwa buti.

YANGA,AZAM, ZASHINDWA KUTAMBIANA

TIMU za Yanga na Azam jana zilishindwa kuwakamata vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Mtibwa Sugar baada ya timu hizo kutoshana nguvu ya mabao 2-2 kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana.

Mchezo wa Mtibwa Sugar dhidi ya Stand United ulioahirishwa juzi baada ya kunyesha mvua kubwa uliendelea jana saa 2 asubuhi na kumalizika kwa timu hizo kuambulia sare ya bao 1-1.

Matokeo ya mchezo huo yaliifanya Mtibwa Sugar kuiweka rehani nafasi yake ya kwanza kutokana na kuzizidi pointi tatu timu zilizoifuatia Yanga na Azam zilizokuwa na pointi 13.

Macho ya wapenzi wengi wa soka yalihamia kwenye pambano baina ya mabingwa watetezi, Azam na Yanga wakitaka kuona ni timu ipi itaifikia Mtibwa kileleni, lakini timu hizo zikaambulia sare hiyo.

Azam iliuanza kwa kasi mchezo huo na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya tano lililofungwa na mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Didier Kavumbagu, aliyefikisha bao la tano msimu huu.

Bao hilo lilitokana na uzembe uliofanywa wa beki, Kelvin Yondani, aliyeanguka chini akiwa kwenye harakati za kuokoa mpira na kupelekea Kavumbagu kumtungua kipa, Deogratius Munishi ‘Dida’, ambaye naye alipotea maboya.

Dakika mbili baadaye Yanga ilisawazisha bao hilo kupitia kwa mshambuliaji wake mpya, Amissi Tambwe, aliyefunga kwa kichwa akimalizia krosi iliyopigwa na kiungo, Salum Telela.

Tambwe alitumia vema udhaifu wa kipa wa Azam, Mwadini Ally, aliyeshindwa kuokoa krosi hiyo kabla ya mpira kutua kichwani kwa mfungaji aliyefunga kirahisi, bao lililomfanya kufikisha mabao mawili msimu huu.

Mshambuliaji wa Yanga, Kpah Sherman, angeweza kuifungia bao la pili timu hiyo dakika ya 25 akiwa ndani ya eneo la 18, lakini shuti alilopiga lilimlenga kipa wa Azam.

Kwa muda mrefu mchezo huo kipindi cha kwanza Azam ilionekana kung’ara sehemu ya kati ya uwanja kutokana na viungo wake, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Mudathir Yahaya kucheza vema kwa ushirikiano.

Dakika ya 35, mwamuzi wa mchezo huo, Mathew Akrama kutoka Mwanza, alilikataa bao la Yanga lililofungwa na Sherman baada ya kudai mshambuliaji huyo alimfanyia madhambi beki wa Azam, Aggrey Morris, kabla ya kufunga.

Hadi kipyenga cha mwamuzi Akrama kinapulizwa kuashiria mapumziko timu hizo zilienda vyumbani kwa sare hiyo. Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kumtoa beki wa kushoto, Edward Charles na kuingia Oscar Joshua.

Yanga ilionekana kuimarika kipindi cha pili tofauti na kipindi cha kwanza hasa kocha wao, Hans van Pluijm kurekebisha makosa yaliyokuwa yakionekana kwenye safu ya kiungo.


Hatimaye katika dakika ya 51 ya mchezo Wanajangwani hao walifanikiwa kuandika bao la pili lililofungwa na winga, Simon Msuva kwa kichwa akitumia vema mpira mrefu uliopigwa na kiungo, Haruna Niyonzima.

Baada ya bao hilo Kocha wa Azam Mcameroon, Joseph Omog, aliongeza nguvu kwenye eneo la kiungo la timu yake baada ya kumuingiza, Amri Kiemba na kumtoa winga, Kipre Tchetche. Dakika chache baadaye beki, Erasto Nyoni alionyeshwa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Niyonzima.

Mabadiliko ya Azam kumuingiza nahodha wake, John Bocco na kumtoa Sure Boy dakika ya 66 yalizaa matunda baada ya mshambuliaji huyo kuisawazishia timu hiyo kwa kichwa kikali cha juu akimalizia krosi ya Himid Mao.

Bocco aliyekuwa akicheza mechi yake ya kwanza msimu huu baada ya kutoka kwenye majeraha, alifunga bao hilo akiwa ameunasa mpira wake wa kwanza toka alipoingia uwanjani.

Yanga iliyoonekana kusaka ushindi kwa udi na uvumba kwenye mchezo huo, iliwapumzisha nyota wake, Danny Mrwanda na Amissi Tambwe na kuwaingiza Hussein Javu na Mrisho Ngassa, ili kuongeza kasi ya kupata bao.

Azam nayo iliimarisha sehemu yake ya ulinzi kwa kumtoa Mao na kuingia David Mwantika, lakini mabadiliko ya pande zote mbili hayakuweza kubadilisha matokeo na mchezo kuisha kwa sare ya mabao 2-2.

Matokeo hayo yamemfanya kocha mpya wa Yanga, Pluijm kuanza kibarua hicho kwa sare, Mholanzi huyo aliingia kwenye timu hiyo akirithi mikoba ya Mbrazil, Marcio Maximo, aliyetimuliwa na msaidizi wake, Leonardo Neiva, baada ya kufungwa na Simba mabao 2-0 katika mchezo wa Nani Mtani Jembe.

Kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, wenyeji Mbeya City walipata ushindi wa pili msimu huu baada ya kuichapa Ndanda FC ya Mtwara kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji, Themi Felix akiunganisha krosi ya Paul Nonga.

Mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi mwanamke, Mary Kapinga, kutoka mkoani Ruvuma ulishuhudiwa timu zote mbili zikipoteza nafasi nyingi za wazi za kufunga mabao.


Baada ya mechi za raundi ya nane, Mtibwa Sugar sasa inamaliza mwaka huu ikiwa kileleni kwenye msimamo kwa pointi 16, Azam na Yanga zinalingana kwa pointi katika nafasi ya pili na tatu zikiwa na pointi 14, Kagera Sugar inashika nafasi ya nne kwa pointi 13, Coastal Union ya tano ikiwa na pointi 12, huku Simba ikiwa nafasi ya nane kwa pointi zake tisa. 


Vikosi:

Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Edward Charles/Joshua, Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, Salum Telela, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe/Ngassa, Danny Mrwanda/Javu na Kpah Sherman.

Azam: Mwadini Ally, Himid Mao/Mwantika, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Serge Wawa Pascal, Erasto Nyoni, Mudathir Yahaya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Bocco, Didier Kavumbagu, Kipre Tchetche/Kiemba na Brian Majwega. 
 

Comments

Popular posts from this blog

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

KADA MGEJA AHUDHURIA MAZIKO YA MAMA MZAZI WA MWANDISHI MWANDAMIZI WA HABARI KAHAMA