WAZIRI WA UCHUKUZI PROFESA MBARAWA AOMBA BAJETI YA SH TRILIONI 2.87 KWA MWAKA 2026 HADI 2027

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame  Mnyaa Mbarawa, akiwasilisha bakjeti ya Wizara hiyo leo bungeni jijini Dodoma hebu fuatana naye katika hotuba yake hii.  Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, ambayo imechambua utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2025/26 pamoja na Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/27, ninaomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa likubali kupokea, kujadili na kuidhinisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2026/27. 2. Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uhai na kutuwezesha kukutana tena siku ya leo kujadili maendeleo ya Sekta ya Uchukuzi. Ninamuomba Mwenyezi Mungu atuongoze vyema katika kujadili Hotuba hii ya Wizara ya Uchukuzi na Bajeti ya Serikali kwa ujumla ili kufikia malengo ya Dira 2050 katika kuwaletea Watanzania maendeleo. 3. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee naomba kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushindi alioupata katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba, 2025. Ushindi huu unaonesha imani kubwa ambayo Watanzania 1 wameendelea kuwa nayo kwa Uongozi wake wenye maono na unaowaletea wananchi maendeleo. Aidha, napenda kumpongeza kwa dhati kwa hatua madhubuti alizochukua katika kutekeleza ahadi alizotoa kwa wananchi ndani ya siku 100 za mwanzo katika kipindi chake cha awamu ya pili. Utekelezaji huo umeonesha dhamira ya kweli ya kuhakikisha kuwa Serikali inatekeleza ahadi zilizotolewa na kuleta matokeo chanya katika sekta mbalimbali nchini. Tunamtakia Mheshimiwa Rais afya njema, umri mrefu, hekima na mafanikio zaidi katika kuiongoza nchi yetu ili kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa letu. 4. Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii, kumpongeza Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mchango wake mkubwa wa kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kutekeleza majukumu ya Serikali. Aidha, ameendelea kusimamia kikamilifu Masuala ya Muungano na Mazingira. 5. Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb.), kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais na kuthibitishwa kwa kishindo na Bunge hili Tukufu kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wote ni mashahidi kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu ameonesha umahiri mkubwa katika kusimamia shughuli za Serikali. 6. Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kukupongeza wewe binafsi kwa kuchaguliwa kwa kishindo na Waheshimiwa Wabunge kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nimpongeze pia Mheshimiwa Daniel Barran Sillo (Mb.), kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge hili Tukufu. Aidha, nitumie fursa hii kuwapongeza Wenyeviti wa Bunge, Mheshimiwa Najma Murtaza Giga (Mb.) na Mheshimiwa Philip Mwanyika (Mb.) kwa kuendelea kuaminiwa kuwa Wenyeviti wa Bunge. Kwa namna ya kipekee 2 nimpongeze Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso (Mb.) kwa kuchaguliwa pia kuwa Mwenyekiti wa Bunge. 7. Mheshimiwa Spika, naishukuru na kuipongeza sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu inayoongozwa na Mwenyekiti Mheshimiwa Selemani Moshi Kakoso (Mb.) ambaye amechaguliwa kwa mara nyingine tena kuiongoza Kamati hiyo. Napenda pia kuishukuru Kamati hii kwa uchambuzi uliyoufanya kwenye Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/26 na Mpango wa Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa fedha 2026/27. 8. Mheshimiwa Spika, vilevile, namshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais, kwa kuendelea kuniamini na kuniteua katika nafasi hii kwa mara nyingine ya kuongoza Wizara ya Uchukuzi. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais ya kuwa, kwa kushirikiana na Naibu Waziri Mheshimiwa David Kihenzile (Mb.), tutatekeleza majukumu aliyotukabidhi kwa kufuata miongozo anayotupatia pamoja na miongozo mingine ya nchi yetu. Pia, tutaendelea kutekeleza shughuli za Wizara ili kuweza kufikia malengo mahsusi ya kuendeleza Sekta ya Uchukuzi na kuwa na mchango mkubwa katika kuchochea ukuaji wa Uchumi wa Taifa. Vilevile, niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri walioaminiwa na kuteuliwa ili kuongoza Wizara mbalimbali. 9. Mheshimiwa Spika, nitumie siku ya leo kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote walioteuliwa na waliochaguliwa kuwawakilisha wananchi katika Bunge hili Tukufu la 13. Niwahakikishie kuwa, Wizara iko tayari kupokea ushauri na maoni ya Watanzania kupitia kwenu ili kuendelea kutatua kero na changamoto zilizopo. 3 10. Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa nitoe pole kwa Bunge lako Tukufu, familia na Watanzania wote kufuatia kifo cha Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho kilichotokea tarehe 11 Desemba, 2025; Mheshimiwa Halima Iddi Nassor aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kilichotokea tarehe 18 Januari, 2026; na Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Isimani na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu kilichotokea tarehe 25 Machi, 2026. Hakika tutaendelea kuthamini na kuenzi michango yao katika Bunge hili na Taifa kwa ujumla. Tunamwomba Mwenyezi Mungu awapumzishe mahali pema peponi, Amina. 11. Mheshimiwa Spika, kabla ya kuendelea na uwasilishaji wangu, niwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji kwa hotuba zao ambazo zimefafanua utendaji wa Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo kwa mwaka wa fedha 2026/27. Vilevile, nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote waliowasilisha hotuba zao kabla yangu. 12. Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba sasa uniruhusu niwasilishe Taarifa ya Mapitio ya Mchango wa Sekta ya Uchukuzi katika kukuza uchumi wa Taifa; Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2025/26 hadi kufikia Machi, 2026; na Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/27. Aidha, nitahitimisha kwa kuomba Bunge lako Tukufu liidhinishe bajeti kwa ajili ya kutekeleza shughuli na miradi ya Wizara ya Uchukuzi (Fungu 62) kwa mwaka wa fedha 2026/27. 4 B. MCHANGO WA SEKTA YA UCHUKUZI KATIKA KUKUZA UCHUMI WA TAIFA 13. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Uchukuzi imeendelea kutoa mchango mkubwa katika kuchochea shughuli za uzalishaji na utoaji huduma katika sekta mbalimbali. Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2024, Sekta ya Uchukuzi ilikua kwa asilimia 4.2 na kuchangia katika Pato la Taifa kwa asilimia 7.5, ambapo imekuwa ya tano (5) kati ya sekta kubwa 17 katika kuchangia Pato la Taifa. 14. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Uchukuzi imeendelea kuchangia zaidi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatokanayo na huduma za bandari. Mathalan, kati ya mwaka wa fedha 2020/21 hadi mwaka wa fedha 2024/25, mapato yatokanayo na kodi ya forodha za kibandari yalichangia wastani wa asilimia 40 ya mapato yote yaliyokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Aidha, mapato hayo yataendelea kuongezeka siku hadi siku. 15. Mheshimiwa Spika, vilevile, Sekta ya Uchukuzi imeendelea kuchangia katika upatikanaji wa fedha za kigeni kupitia mauzo ya huduma za uchukuzi, usafirishaji na huduma za kibandari. Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2025, inaonesha kuwa Sekta ya Uchukuzi ilichangia mauzo ya kiasi cha Dola za Marekani bilioni 2.79 ikilinganishwa na Dola za Marekani bilioni 2.35 zilichangia kwa mwaka 2024. 5 16. Mheshimiwa Spika, katika kukuza upatikanaji wa ajira nchini, Sekta ya Uchukuzi imeendelea kutoa ajira 198,480 wakati wa ujenzi wa miundombinu pamoja na utoaji wa huduma za uchukuzi. (Maelezo ya kina kuhusu mchango wa Sekta ya Uchukuzi katika kukuza Uchumi wa Taifa yameainishwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia Aya ya 14 hadi 20) C. UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA NA TAASISI ZAKE KWA MWAKA WA FEDHA 2025/26 17. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2025/26, Wizara ya Uchukuzi (Fungu 62) iliidhinishiwa jumla ya Shilingi Trilioni 2.746 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni 125.438 zilikuwa ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, sawa na asilimia 4.57 na Shilingi Trilioni 2.621 zilikuwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, sawa na asilimia 95.43. Hadi kufikia Machi, 2026 jumla ya Shilingi Trilioni 1.374 zilikuwa zimetolewa ikiwa ni sawa na asilimia 66.75 ya Shilingi Trilioni 2.059 zilizotakiwa kutolewa katika kipindi hicho. Kati ya fedha hizo zilizotolewa, Shilingi Bilioni 99.682 ni fedha za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Trilioni 1.275 ni fedha za miradi ya maendeleo. Baada ya kupokea fedha hizo, Wizara ya Uchukuzi iliendelea kutekeleza majukumu yake katika maeneo mbalimbali kama ifuatavyo:- C:1 UDHIBITI NA UTOAJI WA HUDUMA ZA UCHUKUZI UDHIBITI WA HUDUMA ZA USAFIRI WA ANGA 6 18. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu ya udhibiti wa usafiri wa anga, Serikali kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeendelea kusimamia ubora wa viwanja vya ndege nchini. Aidha, Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) limeendelea kuikasimisha Tanzania jukumu la uongozaji ndege zinazoruka na kupita urefu wa futi elfu 25 juu ya anga la nchi ya Burundi. Sambamba na jukumu hilo, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, jumla ya ndege 189 zilifanyiwa ukaguzi na kupewa vyeti vya ubora na kuendelea kufanya kazi nchini. 19. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, abiria waliotumia usafiri wa anga waliongezeka na kufikia abiria Milioni 6.81 ikilinganishwa na abiria Milioni 6.037 katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 12.63. Kwa upande wa mizigo katika kipindi hicho, jumla ya tani 34,750.2 zilisafirishwa ndani na nje ya nchi, ikilinganishwa na tani 33,112.5 zilizosafirishwa ndani na nje ya nchi katika kipindi kama hicho mwaka 2024/25. 20. Mheshimiwa Spika, Naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TCAA imeendelea na ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) Jijini Dar es Salaam ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 11.3. (Maelezo ya kina kuhusu udhibiti wa utoaji wa huduma za usafiri wa anga kupitia TCAA yameainishwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia Aya ya 24 hadi 38) UDHIBITI WA USAFIRI ARDHINI 7 21. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imeendelea kutekeleza majukumu ya kusimamia udhibiti wa usafiri ardhini katika maeneo makuu matatu (3) ya usafiri wa barabara, reli na waya. Katika kutekeleza majukumu hayo, LATRA katika kipindi cha kuanzia Julai 2025 hadi Machi 2026, ilitoa leseni 388,715 za usafirishaji, ikiwa ni ongezeko la asilimia 55 kutoka mwaka uliopita. Leseni hizo zilihusisha mabasi ya abiria, magari ya mizigo na ya kukodi. Vilevile, Serikali kupitia LATRA imeendelea kudhibiti nauli na ubora wa huduma huku ikihamasisha matumizi ya nishati mbadala ikiwemo magari ya umeme nchini. 22. Mheshimiwa Spika, Mabasi 13,843 yaliunganishwa kwenye mfumo wa ufuatiliaji wa VTS na madereva 12,699 walisajiliwa kwa ajili ya kuongeza usalama wa safari. Aidha, Mfumo wa Tiketi Mtandao (CeTS) umeendelea kutumika ambapo mabasi 8,126 yaliunganishwa na zaidi ya abiria milioni 21 walitumia mfumo wa tiketi mtandao kununua tiketi hadi kufikia Machi 2026. (Maelezo ya kina kuhusu udhibiti wa usafiri ardhini kupitia LATRA yameoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia Aya ya 39 hadi 57) UDHIBITI WA USAFIRI MAJINI 23. Mheshimiwa Spika, katika kusimamia udhibiti wa usafiri majini, Serikali kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imeendelea kusimamia usalama wa vyombo vya usafiri majini; kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na shughuli za meli katika eneo la Tanzania Bara; na kutoa huduma ya ugomboaji na uondoshaji wa shehena kwa bidhaa mahsusi. Udhibiti wa Watoa Huduma za Usafirishaji Majini 8 24. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, jumla ya watoa huduma 1,794 walisajiliwa na kupewa leseni, ikilinganishwa na watoa huduma 1,556 waliosajiliwa katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2024/25. 25. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha usalama wa usafiri katika Ziwa Victoria, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Uganda zimeendelea kutekeleza Mradi wa Kikanda wa Kuboresha Mawasiliano na Uchukuzi katika ziwa hilo. Mradi huo unajumuisha ujenzi wa Kituo Kikuu cha Uratibu wa Utafutaji na Uokoaji, na ununuzi wa boti mbili (2) za utafutaji na uokoaji pamoja na boti ya matibabu (Ambulance Boat) ambazo zimeanza kutoa huduma katika Ziwa Victoria. Vilevile, Serikali imenunua boti nyingine mbili (2) za kisasa za utafutaji na uokoaji ambazo zimeanza kutoa huduma katika Ziwa Tanganyika na katika ukanda wa Bahari ya Hindi eneo la Mkoa wa Tanga. (Maelezo ya kina kuhusu udhibiti wa usafiri majini kupitia TASAC yameoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia Aya ya 58 hadi 69) UDHIBITI NA UTOAJI HUDUMA ZA HALI YA HEWA 26. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea na utoaji na udhibiti wa huduma za hali ya hewa nchini. 27. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha huduma za hali ya hewa zinazotolewa kwa sekta ndogo ya usafiri wa anga, TMA imekamilisha ufungaji wa mitambo miwili (2) ya uangazi wa hali ya hewa katika viwanja vya ndege 9 vya Mpanda na Pemba. Aidha, TMA imeendelea na ujenzi wa miundombinu ya hali ya hewa ikiwemo maabara ya uhakiki wa vifaa vya hali ya hewa (Calibration Center) Dar es Salaam ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 46. (Maelezo ya kina kuhusu udhibiti na utoaji huduma za hali ya hewa kupitia TMA yameoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia Aya ya 70 hadi 83) C:2 UTOAJI WA HUDUMA ZA UCHUKUZI HUDUMA ZA BANDARI 28. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), inaendelea kusimamia bandari za mwambao wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu kwa kuendeleza miundombinu na utoaji wa huduma za kibandari kwa viwango vinavyokubalika kikanda na kimataifa. Katika kipindi cha Julai, 2025 hadi Machi 2026, TPA ilihudumia jumla ya tani milioni 29.66 za shehena, ikilinganishwa na tani milioni 23.18 zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 27.96. Aidha, shehena iliyosafirishwa kwenda nchi jirani imeongezeka hadi kufikia tani milioni 10.93, ikilinganishwa na tani milioni 8.24 zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 32.64. Ongezeko hilo limetokana na uboreshaji wa miundombinu na ushirikishwaji wa Sekta Binafsi. 29. Mheshimiwa Spika, tangu kupata uhuru, nchi yetu imekuwa na changamoto ya kuhifadhi mafuta. Serikali ya awamu ya Sita imeamua kulifanyia kazi suala hilo kwa vitendo, ambapo TPA imeanza ujenzi wa miundombinu ya kupokelea na kuhifadhi mafuta (Single Receiving Terminal – SRT) unaohusisha ujenzi wa matenki 15 ya mafuta (tank farms) yenye uwezo 10 wa kuhifadhi mita za ujazo 378,000, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 42 na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2026. 30. Mheshimiwa Spika, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, imeainisha umuhimu wa kujenga Bandari ya Bagamoyo. Napenda kulitaarifu bunge lako Tukufu kuwa, Serikali kupitia TPA inakamilisha maandalizi ya kuanza utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati. Bandari hiyo itahusisha ujenzi wa gati lenye urefu wa kilomita 1.32 pamoja na miundombinu wezeshi ya kuhudumia meli kubwa za kisasa aina za Megamax ambazo haziwezi kuhudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa. Katika kutekeleza awamu ya kwanza ya Mradi huo, tayari mitambo kwa ajili ya uchimbaji wa kina cha maji imepatikana na kazi hiyo inatarajiwa kuanza rasmi katika mwaka wa fedha 2026/27. 31. Mheshimiwa Spika, ili kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam, Serikali imeendelea kuhimiza matumizi ya bandari kavu nchini ikiwemo Bandari Kavu ya Kwala iliyopo Mkoa wa Pwani ambayo imeendelea kutoa huduma, ambapo hadi kufikia mwezi Machi, 2026 bandari hiyo ilihudumia makasha 14,460. Katika hatua nyingine, mwezi Machi, 2026 TRC ilianza usafirishaji wa shehena kwenda katika Bandari Kavu ya Isaka. 32. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha bandari katika Maziwa Makuu nchini ambapo hadi kufikia mwezi Machi, 2026 uboreshaji wa Bandari za Bukoba na Kemondo umekamilika na uboreshaji wa Bandari ya Mwanza North umefikia asilimia 75. Serikali inaendelea na Mradi wa Uboreshaji wa Bandari ya Kigoma ambao umefikia asilimia 13. Kwa upande wa bandari ya Mbamba Bay umefikia asilimia 49. Ushirikishwaji wa Sekta 11 Binafsi Katika Shughuli za Uendelezaji na Uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam 33. Mheshimiwa Spika, Kama inavyokumbukwa, mwaka 2023 Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilifanya uamuzi wa kimkakati wa kushirikisha Sekta Binafsi katika shughuli za uendelezaji na uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza ufanisi, ushindani na tija katika utoaji wa huduma za kibandari nchini. Kutokana na uamuzi huo, Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi iliingia mikataba na waendeshaji mahiri wa bandari wenye uzoefu mkubwa kimataifa. Hatua hiyo imeendelea kuzaa matokeo chanya na manufaa makubwa kwa Taifa, ikidhihirisha dira sahihi ya Serikali katika kuimarisha uchumi wa buluu na nafasi ya Tanzania kama lango kuu la biashara kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na yafuatayo:- i. Kuongezeka kwa shehena inayohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam kutoka tani milioni 16.27 mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia tani milioni 27.76 mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 70.62; ii. Kuongezeka kwa wastani wa shehena ya makasha yanayohudumiwa kwa mwezi kutoka makasha TEUs 61,000 hadi TEUs 102,000, sawa na ongezeko la asilimia 67.21; iii. Kupungua kwa gharama za uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kutoka Shilingi bilioni 652.83 mwaka 2023/24 hadi Shilingi bilioni 308.95 mwaka 2024/25; 12 iv. Kuongezeka kwa makusanyo ya mapato ya TPA yatokanayo na ada za huduma za kibandari kutoka Shilingi bilioni 896.95 mwaka 2020/21 hadi kufikia Shilingi trilioni 1.30 mwaka 2024/25; v. Kupungua kwa muda wa kuhudumia meli za makasha gatini kutoka wastani wa siku 10 hadi siku 3; na vi. Kupungua kwa muda wa meli kusubiri nangani kutoka wastani wa siku 46 hadi wastani wa siku 7 kwa meli za mizigo mchanganyiko na kichele, Hatua za Serikali Kukabiliana na Ongezeko la Shehena katika Bandari ya Dar es Salaam 35. Mheshimiwa Spika, Kutokana na kuongezeka kwa ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam pamoja na kuimarika kwa imani ya watumiaji wa bandari hiyo ndani na nje ya nchi, kumekuwepo na ongezeko kubwa la shehena ya mizigo inayohudumiwa bandarini. Ili kuhakikisha bandari inaendelea kutoa huduma kwa ufanisi, ushindani na viwango vinavyokidhi mahitaji yanayoongezeka, Serikali inaendelea kutekeleza hatua mbalimbali za kimkakati zifuatazo:- i. Kukamilisha ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR inayoingia moja kwa moja bandarini (Port Link), ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 99.7 na majaribio ya usafirishaji wa mizigo kwa treni yanaendelea. Sambamba na hilo TRC, inaendelea kujenga eneo maalum (loading platform) la kupakilia mizigo kwenye treni za SGR ndani ya eneo la bandari kwa lengo la kuongeza kasi, na ufanisi katika utowaji wa mizigo Bandarini; ii. Kuendelea na upanuzi wa eneo la Kurasini lenye ukubwa wa mita za mraba 220,000 kwa ajili ya kuhudumia makasha 700,000 kwa mwaka. Awamu ya kwanza ya mradi huo inatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2026 na kuhudumia 13 makasha 150,000 kwa mwaka, huku Awamu ya Pili ikitarajiwa kukamilika mwezi Julai 2027; iii. Kujenga kituo cha kisasa cha mizigo katika Stesheni ya SGR Morogoro chenye ukubwa wa mita za mraba 68,000 na uwezo wa kuhudumia makasha 600 kwa siku, kwa ajili ya kuhudumia mizigo inayosafirishwa kwa njia ya barabara kuelekea mikoa mbalimbali na nchi za jirani. (Maelezo ya kina kuhusu huduma za bandari, yameainishwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia Aya ya 84 hadi 110). HUDUMA ZA USAFIRI WA RELI Huduma za Usafiri kupitia Reli za MGR na SGR 36. Mheshimiwa Spika, Wizara inaishukuru Serikali kwa kuchukua hatua za kuboresha Shirika la Reli Tanzania (TRC), zoezi lililoanza mwaka 2017. Tangu kuanzishwa kwa Shirika hili, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya mishahara. Naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, katika mwaka 2026/27, TRC haitatengewa tena ruzuku kwa ajili ya mishahara kutoka Serikalini. 37. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TRC, imeendelea na ujenzi na uendeshaji wa reli ya SGR pamoja na kuboresha mtandao wa reli ya MGR yenye urefu wa takriban kilomita 2,707. Ujenzi wa reli ya SGR unatekelezwa kwa awamu mbili ikihusisha kilomita 1,219 za njia kuu kwa awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam – Mwanza; na kilomita 1,590 za awamu ya pili ikijumuisha vipande vya Tabora – Kigoma na Uvinza – Musongati. Kukamilika kwa awamu hizo mbili za reli ya SGR kutaifanya Tanzania kuwa na mtandao wa jumla ya kilomita 2,809 za reli ya SGR. 14 Uendelezaji na Uendeshaji wa Reli ya Kisasa ya SGR 38. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TRC imeendelea na ujenzi wa Reli ya SGR ambapo hadi kufikia mwezi Machi, 2026 ujenzi wa kipande cha kwanza Dar es Salam – Morogoro (km 300) na kipande cha pili Morogoro – Makutupora (km 422) umekamilika kwa sehemu kubwa. Aidha, TRC inaendelea na utoaji wa huduma ya usafiri wa treni kwa vipande husika. Kwa kipande cha Mwanza – Isaka (km 341), ujenzi unaendelea na umefikia asilimia 68.77. 39. Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia mwezi Machi 2026, ujenzi wa reli ya SGR katika kipande cha tatu: Makutupora – Tabora (km 368) na kipande cha nne: Tabora – Isaka (km 165) unaendelea ambapo kazi mbalimbali zinazoendelea kutekelezwa. Kwa ujumla ujenzi wa vipande hivi 2 umekuwa na changamoto kwa muda mrefu, ambazo zilisababisha utekelezaji wake kuwa na kasi ndogo. Hata hivyo, Serikali tayari imepata suluhisho la kukamilisha ujenzi wake kwa kupata mkopo wenye masharti nafuu wa thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.277, sawa na takriban Shilingi trilioni 3.32. Usafirishaji wa Abiria na Mizigo kwa Reli za SGR na MGR 40. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TRC imeendelea na usafirishaji wa abiria kati ya Dar es Salaam na Dodoma kupitia reli ya SGR. Usafirishaji kupitia reli hiyo umezidi kuimarika ambapo katika kipindi cha Julai, 2025 hadi Machi, 2026 jumla ya abiria milioni 2.51 walisafirishwa ikilinganishwa na abiria 15 millioni 2.05 waliosafirishwa katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2024/25 sawa na ongezeko la asilimia 22.40. 41. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia Julai, 2025 hadi kufikia mwezi Machi 2026, TRC ilisafirisha jumla ya tani 102,452 za mizigo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kuanza usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya SGR. 42. Mheshimiwa Spika, Katika hatua za kuunganisha miundombinu ya reli ya SGR na MGR, Serikali imeendelea na uunganishaji wa reli hizo katika eneo la Ruvu ili kuwezesha usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari za Dar es Salaam na Tanga, ambapo utekelezaji wake umefika asilimia 85. Aidha, ujenzi wa kuunganisha reli za MGR na SGR unaendelea katika eneo la Bahi kwa lengo la kuwezesha uhamishaji wa mizigo (transhipment) kati ya reli hizo 2 na unaendelea vizuri. 43. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha Reli ya MGR kwa kubadilisha reli nyepesi na kuweka nzito, pamoja na kuongeza uwezo wa madaraja. Ukarabati huo unaendelea kupitia Mfuko wa Reli, ambapo hadi Machi 2026, kipande cha Kaliua–Mpanda kilikuwa kimekamilika kwa asilimia 32.72. 44. Mheshimiwa Spika, Kukabiliana na mafuriko yanayoathiri Reli ya MGR katika eneo la Kilosa–Kidete–Igandu, Serikali imekamilisha ujenzi wa njia ya reli yenye urefu wa km 6.2 na daraja katika eneo la Godegode–Gulwe ambapo ujenzi umefikia asilimia 99. Aidha, kupitia Mradi wa TIRP II Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na Wadau, inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa mabwawa sita (Kidete, Kimagai, Buigiri, Ikowa, Hombolo na Dabalo) katika 16 Mto Kinyasungwe. Mabwawa hayo yatapunguza mafuriko na kuboresha uendeshaji wa reli mwaka mzima. Huduma za Usafiri kupitia Reli ya TAZARA 45. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Tanzania na Zambia zimeendelea kushirikiana katika kusafirisha mizigo na abiria kwa kutumia Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA). Lakini, kwa muda mrefu reli hii imekuwa na ufanisi mdogo kutokana na uchakavu wa miundombinu na uhaba wa vitendea kazi. 46. Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Hotuba yake wakati wa kufungua Rasmi Bunge la 13, tarehe 14 Novemba 2025, alilitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali yake kwa kushirikiana na nchi mwanahisa imeanza mkakati mahsusi wa kufanya maboresho makubwa ya reli ya TAZARA. Napenda kulitaarifu Bunge lako kuwa, uzinduzi wa mradi wa ufufuaji wa reli ya TAZARA ulifanyika tarehe 20 Novemba, 2025 jijini Lusaka nchini Zambia. Uzinduzi huo ulifanyika kufuatia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Zambia mnamo tarehe 29 Septemba, 2025 kusaini mkataba wa uendeshaji (Concession Agreement) na Kampuni ya CCECC kutoka nchini kwa ajili ya kuboresha reli ya TAZARA. Kampuni hii itawekeza jumla ya Dola za Marekani bilioni 1.4, ambayo ni sawa na takriban Shilingi trilioni 3.6. Maboresho ya reli hii yanatarajiwa kuongeza uwezo wa kusafirisha mizigo milioni 2.4 kwa mwaka na kuzalisha ajira mpya 100,000. 17 (Maelezo ya kina kuhusu huduma za usafiri wa reli na utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya reli kupitia TRC na TAZARA yameoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia Aya ya 111 hadi 145). HUDUMA ZA UCHUKUZI KATIKA BAHARI NA MAZIWA MAKUU Huduma za Usafiri na Usafirishaji katika Maziwa Makuu 47. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TASHICO imeendelea kusimamia ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli zilizopo ili kuimarisha usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo. Kwa kipindi cha Julai, 2025 hadi Machi, 2026 TASHICO ilisafirisha abiria 128,191 na tani 71,796.25 za mizigo ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 22.51 ukilinganisha na kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita. 48. Mheshimiwa Spika, Serikali imekamillisha ujenzi wa Meli ya MV. New Mwanza katika Ziwa Victoria. Serikali pia imeendelea na ukarabati wa meli katika Ziwa Victoria, ambapo ukarabati wa meli ya uokozi ya MT. Ukerewe umefikia asilimia 79. Vilevile, Serikali kupitia TASHICO imeanza maandalizi ya ujenzi wa meli yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 za mizigo katika ziwa hilo. Mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita Kutumia Fursa zilizopo ukanda wa Ziwa Tanganyika 49. Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa ukanda wa Ziwa Tanganyika, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo: 18 Ujenzi wa meli nne (4) za mizigo katika Ziwa Tanganyika zinazojengwa na TPA kwa kushirikiana na Sekta Binafsi ambazo zina uwezo wa kubeba tani 2,000 za mizigo kila meli moja na kwa sasa meli hizo zimekamilika; kuanza ujenzi wa meli mpya ya Abiria, kuanza ujenzi wa karakana ya ujenzi wa meli; Kuanza ujenzi wa magati mawili (2) ya kisasa katika Bandari ya Kigoma, ambao hadi Machi, 2026 utekelezaji wake umefikia asilimia 13; Kuendelea na ukarabati wa meli ya MV. Liemba ambao umefikia asilimia 64. (Maelezo ya kina kuhusu huduma za uchukuzi katika bahari na maziwa makuu kupitia TASHICO yameoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia Aya ya 146 hadi 156) HUDUMA ZA VIWANJA VYA NDEGE 50. Mheshimiwa Spika, katika uendelezaji na uendeshaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege nchini, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imeendelea kusimamia na kuendeleza viwanja vya ndege vya Serikali. 51. Mheshimiwa Spika, katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Serikali imeahidi kukipandisha hadhi Kiwanja cha Ndege cha Mwanza kuwa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa. Wizara kwa kushirikiana na TAA tayari imekamilisha Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa Mradi wa Ujenzi wa Jengo Jipya la abiria litakalokuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 2.5 kwa mwaka pamoja na miundombinu wezeshi. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kufanyika kwa ushirikiano Kati ya TAA na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). 19 Hadi kufikia Machi 2026, Wizara kupitia TAA imeendelea na uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Arusha ambapo ufungaji wa mfumo wa taa za kuongozea ndege umefikia asilimia 65 na ujenzi wa tabaka la juu la lami la barabara ya kuruka na kutua kwa ndege katika kiwanja hicho unaendelea. 52. Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza viwanja vya ndege vya mikoa, Wizara kupitia TAA inaendelea na uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma na Kiwanja cha Ndege cha Moshi. Pia, kwa upande wa Mradi wa ujenzi wa Kiwanja Kipya cha Ndege cha Mkoa wa Kagera, kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Awali zinaendelea. 53. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TAA imeendelea na utekelezaji wa maboresho ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) ikiwemo: ukarabati wa barabara ya kuruka na kutua ndege; ufungaji wa mfumo wa taa za kuongozea ndege (AGL), na ujenzi wa eneo la kuhifadhia mizigo mikavu (dry cargo) ambao umefikia asilimia 5 yanaendelea. Aidha, wakandarasi wa ujenzi wa Jengo Jipya la Watu Mashuhuri (New VIP Terminal) wamepatikana na maandalizi ya ujenzi yanaendelea. (Maelezo ya kina kuhusu huduma za viwanja vya ndege kupitia TAA yameoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia Aya ya 157 hadi 167) HUDUMA ZA USAFIRI WA ANGA 54. Mheshimiwa Spika, Tangu mwaka 2015, Serikali imeendelea kuifufua Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), ambapo idadi ya ndege imeongezeka kutoka ndege 1 mwaka 2016 hadi ndege 16 mwaka 2026. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ongezeko la abiria kutoka 107,166 mwaka 20 2016/17 hadi 1,178,025 mwaka 2024/25, mapato kuongezeka kutoka Shilingi bilioni 23 hadi bilioni 595.7, pamoja na mapato ya fedha za kigeni kupanda kutoka Dola milioni 9.85 hadi milioni 157.7. 55. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, ATCL ilisafirisha abiria 1,072,528 sawa na ongezeko la asilimia 22.38 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita, huku tani 4,129.72 za mizigo zikisafirishwa. 56. Mheshimiwa Spika, Licha ya mafanikio hayo, kampuni bado inakabiliwa na changamoto ya mtaji mdogo na mfumo wa umiliki wa ndege unaoathiri mizania ya kifedha. Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuboresha mfumo huo ili kuimarisha ufanisi na Mizania wa kihesabu ya ATCL. (Maelezo ya kina kuhusu huduma za usafiri wa anga kupitia ATCL yameoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia Aya ya 168 hadi 180 C:3 VYUO VYA MAFUNZO VYA KISEKTA NA MASUALA MTAMBUKA 57. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Uchukuzi inasimamia uendeshaji wa vyuo vya mafunzo ya kisekta vilivyo chini yake ili kuhakikisha sekta ya usafirishaji na usafiri nchini inakuwa na wataalam wa ndani wakutosha. Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT) na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) 58. Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kukijengea uwezo Chuo cha NIT na DMI Serikali imeendelea kutekeleza Miradi ya Kuboresha Miundombinu na 21 Vifaa vya Kufundishia. Na hii imeongeza udahili kwa kozi mbalimbali kwa kiasi kikubwa kama inavyoonyeshwa kwenye kitabu changu cha hotuba ya bajeti kuanzia Aya ya 181 hadi 206. C:5 MAFANIKIO, CHANGAMOTO NA HATUA ZILIZOCHUKULIWA C:5:1 MAFANIKIO 59. Mheshimiwa Spika, Naomba niainishe kwa muhtasari mafanikio makubwa yaliyopatikana katika mwaka wa fedha 2025/26, hadi mwezi Machi, 2026 kama ifuatavyo:- 1. Kuendelea na Ujenzi wa Reli ya SGR kwa Awamu zote Mbili 60. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na ujenzi wa Reli ya SGR kwa awamu zote mbili (2) na utekelezaji wake upo katika hatua mbalimbali kama ilivyoainishwa katika Kitabu changu cha Hotuba. 2. Kuendelea kwa Ufanisi wa Usafirishaji wa Abiria kupitia Reli ya SGR 22 61. Mheshimiwa Spika, Sote ni mashuhuda kuwa, usafirishaji wa abiria na mizigo kupitia reli ya SGR umeendelea kuimarika kati ya Dar es Salaam na Dodoma ambapo takriban wastani wa abiria 280,000 husafiri kwa mwezi, sawa na abiria 9,300 kwa siku. Kwa mwenendo huu, inakadiriwa kuwa, zaidi ya abiria milioni 3 watakuwa wamesafirishwa kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2025/26, ikilinganishwa na wastani wa abiria 400,000 wanaosafiri kwa reli ya MGR kwa mwaka. Kutokana na uendeshaji huo, katika kipindi cha kuanzia Julai, 2025 hadi Machi 2026, jumla ya Shilingi bilioni 82.77 zimekusanywa. Aidha, takwimu hizo zinafanya Serikali kuwa imekusanya jumla ya Shilingi bilioni 169.37 tangu kuanza kwa safari za SGR nchini mwezi Juni, 2024. 3. Kuanza Usafirishaji wa Mizigo kwa Reli ya SGR 62. Mheshimiwa Spika, katika Hotuba yangu ya mwaka wa fedha 2025/26, niliahidi kuanza huduma ya usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya SGR. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, mwezi Julai, 2025 TRC ilianza rasmi usafirishaji wa mizigo kupitia Reli ya SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma (Ihumwa). 4. Serikali TRC kuanza Kujiendesha bila Ruzuku kutoka Mfuko Mkuu wa 63. Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa kuanzia Januari, 2026 TRC imefanikiwa kuanza kujitegemea kwa upande wa Mishahara na Matumizi Mengineyo (OC) bila uwezeshaji kutoka Mfuko Mkuu 23 wa Serikali. Kwa kipindi cha takriban miaka 10, kiasi cha Shilingi bilioni 12.92 kila mwaka kilikuwa kinatolewa na Serikali kwa TRC kwa ajili ya mishahara. 5. Shehena Kuongeza Uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam Kuhudumia 64. Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuiongezea uwezo Bandari ya Dar es Salaam katika kuhudumia shehena, Serikali inaendelea na upanuzi wa eneo la Kurasini (Kurasini Port Extension) lenye ukubwa wa mita za mraba 220,000 kwa ajili ya kuhudumia makasha 700,000 kwa mwaka. 6. Ufanisi wa Ushiriki wa Sekta Binafsi katika Bandari ya Dar es Salaam na Kuongezeka kwa Shehena kwa Bandari zote Nchini 65. Mheshimiwa Spika, kutokana na kuendelea kwa utaratibu wa kushirikisha Sekta Binafsi katika uendeshaji wa bandari nchini hususan Bandari ya Dar es Salaam, kwa kipindi cha Julai, 2025 hadi Machi, 2026 shehena iliyohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam ilifikia tani milioni 27.83 ikilinganishwa na tani milioni 19.31 zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 29.83. Aidha, inatarajiwa kuwa shehena ya mizigo itakayohudumiwa na Bandari hii itaongezeka hadi kufikia wastani wa tani milioni 40.839 na kwa Bandari zote shehena ya mizigo inategemewa kufikia Milioni 59.768 kwa mwaka 2030/31. 7. Kuimarisha usafiri katika Maziwa Makuu 24 66. Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha ujenzi wa Meli ya MV. New Mwanza katika Ziwa Victoria. Aidha, ukarabati wa meli ya MT. Sangara umekamilika na sasa imeanza kutoa huduma. Vilevile, Serikali kupitia TPA kwa kushirikiana na Sekta Binafsi imekamilisha ujenzi wa meli nne (4) za mizigo katika Ziwa Tanganyika zenye uwezo wa kusafirisha tani 8,000 za mizigo. 8. Kuongezeka kwa Mtandao wa Vituo vya Usafiri wa Anga Vinavyohudumiwa na ATCL 67. Mheshimiwa Spika, kutokana na juhudi za Serikali katika kuimarisha utendaji, Kampuni ya ATCL imeongeza vituo vya huduma ya usafiri wa anga ambapo hadi kufikia Machi, 2026 ina jumla ya vituo 33 ikilinganishwa na vituo 23 vilivyokuwepo mwaka 2020/21. Kati ya vituo hivyo, vituo 16 ni vya ndani ya nchi vituo (14) vya kikanda na vituo 3 vya nje ya Bara la Afrika. 9. Kuimarika kwa Ukusanyaji wa Mapato Yatokanayo na Huduma za Usafiri wa Anga kupitia ATCL 68. Mheshimiwa Spika, Kampuni ya ATCL kwa mwaka 2024/25 ilikusanya mapato ya Shilingi bilioni 626.5 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 175.69 zilizokusanywa mwaka 2020/21. 10. Kuimarika kwa Huduma za Viwanja vya Ndege 69. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha huduma za usafiri wa anga nchini, Serikali imekamilisha ukarabati wa viwanja vya ndege vya Sumbawanga, Songea, Shinyanga na Tabora. Aidha, ukarabati mkubwa wa jengo la 25 kuhifadhi mizigo inayoharibika haraka (perishables) katika Kiwanja cha Ndege cha KIA umekamilika na hivyo kuchochea kuimarika kwa mnyororo wa usafirishaji. 11. Kuanza Kutolewa kwa Mafunzo ya Urubani Nchini 70. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoahidi katika Hotuba yangu ya mwaka 2025/26 kuwa Serikali itaanza rasmi kutoa mafunzo ya urubani katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT). Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali kupitia Chuo cha NIT imeanza rasmi kutoa mafunzo ya urubani mwezi Julai 2025, ambapo wanafunzi 22 wamedahiliwa na wanaendelea na masomo. Mafanikio hayo yamewezesha kupunguza gharama za masomo nje ya nchi kwa kozi za urubani. Kuanza kutolewa kwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha usafiri wa anga. (Maelezo ya kina kuhusu mafanikio yaliyopatikana hadi kufikia Machi, 2026 yameoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia Aya ya 223 hadi 252) C:5:2 CHANGAMOTO NA HATUA ZILIZOCHUKULIWA 71. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Uchukuzi imekabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mwaka 2025/26. Changamoto hizo na mikakati ya kuzitatua zimeoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia Aya ya 253 hadi 254. D. MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2026/27 26 72. Mheshimiwa Spika, katika Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27, Wizara imezingatia Dira 2050, Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV 2026/27 – 2030/31), Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa mwaka 2026/27, Mpango Mkakati wa Wizara wa Miaka Mitano (2026/27 – 2030/31) pamoja na maelekezo ya Viongozi Wakuu wa Serikali. 73. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2026/27, Wizara ina vipaumbele mbalimbali ambavyo ni pamoja na: 1. Kuendelea na ujenzi na uendeshaji wa Reli ya Kisasa ya SGR; 2. TAZARA; 3. 4. 5. 6. 7. 8. Kuendelea na ukarabati na uboreshaji wa Reli za MGR na Uboreshaji wa miundombinu na huduma katika Bandari; Kuendelea na uboreshaji wa usafiri wa anga; Kuendelea na ujenzi na ukarabati wa meli; Kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa; Kuboresha udhibiti, ubora na usalama wa huduma za uchukuzi; na Kuendelea na uboreshaji wa vyuo vya mafunzo vya kisekta. 74. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Uchukuzi (Fungu 62) katika mwaka wa fedha 2026/27 imetengewa jumla ya Shilingi Trilioni 2.872 ambapo kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni 126.04 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, sawa na asilimia 4.38 ya bajeti, na Shilingi Trilioni 2. 746 ni kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo, sawa na asilimia 95.62. 75. Mheshimiwa Spika, Kati ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, Shilingi Bilioni 100.135 ni kwa ajili ya Mishahara ya watumishi na 27 Shilingi Bilioni 25.906 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC) kwa Wizara na Taasisi zinazopokea Ruzuku. Vilevile, kati ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Shilingi Trilioni 2.452 ni fedha za ndani na Shilingi Bilioni 294.184 ni fedha za nje. (Vipaumbele na bajeti iliyotengwa katika mwaka wa fedha 2026/27 vimeainishwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia Aya ya 255 hadi 259) D:1 MIRADI YA MAENDELEO ITAKAYOTEKELEZWA KATIKA MWAKA 2026/27 76. Mheshimiwa Spika, Miradi ya kielelezo na kimkakati itakayotekelezwa kwa mwaka wa fedha 2026/27 kama ifuatavyo: Miradi ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Bandari na Huduma za Usafiri Majini 77. Mheshimiwa Spika, miradi itakayotekelezwa katika eneo hili ni: 1. Mradi wa Uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam (DMGP); Miradi mingine ya uboreshaji wa bandari itatekelezwa kupitia mapato ya ndani ya TPA ikiwemo uboreshaji wa bandari za mwambao wa Bahari ya Hindi: Bandari ya Bagamoyo, Bandari ya Mtwara (Kisiwa Mbao) na bandari za 28 Maziwa Makuu: Bandari ya Mwanza North, Mbamba Bay, na Mradi wa Uboreshaji wa Bandari ya Kigoma; na 78. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Bandari ya Dar es Salaam kupitia sekta binafsi, DP World inaendelea na mpango mkubwa wa uwekezaji katika vifaa vya kisasa vya kuhudumia mizigo, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi, kasi na ushindani wa huduma za bandari. Kufikia mwaka 2025/2026, kampuni tayari imevuka zaidi ya nusu ya lengo la uwekezaji la dola milioni 250 sawa na shilingi bilioni 650 ndani ya miaka mitano, ikiwa ni mafanikio makubwa ndani ya miaka miwili ya kwanza ya utekelezaji. Katika mwaka wa fedha 2026/2027, maboresho yataendelea kupitia upanuzi wa miundombinu, uboreshaji wa mifumo ya utendaji, na kuimarisha uwezo wa kuhudumia mizigo kwa viwango vya kisasa. Miongoni mwa mipango hiyo ni ununuzi wa mitambo ya kisasa ya upakuaji na upakiaji (cranes), ujenzi wa mageti mawili yanayounganisha bandari na Barabara ya Nelson Mandela, pamoja na uwekezaji katika mitambo ya kushughulikia shehena za kichele (dry bulk) utakaoongeza uwezo kwa asilimia 65 hadi takriban tani milioni 5.5. Aidha, uwezo wa kuhudumia mizigo mchanganyiko utaongezeka kwa asilimia 25, huku sekta ya usafirishaji wa magari (PCC na PCTC) ikitarajiwa kukua kwa asilimia 30 kutokana na maboresho ya sera na miundombinu. Hatua hizi pia zitaongeza ufanisi wa bandari za Tanga na Mtwara. Kwa ujumla, ifikapo mwaka 2028, sekta ya bandari inatarajiwa kuwa imepiga hatua kubwa ya mageuzi, ikiwa na uwezo wa juu zaidi wa kuhudumia mizigo, kasi ya huduma, na ushindani wa kimataifa, hivyo kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara katika ukanda mzima. 29 2. Miradi ya kuboresha Usafiri wa Anga na Hali ya Hewa Nchini 79. Mheshimiwa Spika, Miradi hiyo ni pamoja na: 1. Ununuzi wa Ndege na Uimarishaji wa Kampuni ya ATCL; 2. 3. Ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga; Ujenzi, ukarabati na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Mwanza, Arusha, Mtwara, Serengeti, Kagera, Kilimanjaro (KIA) na Julius Nyerere (JNIA); na 4. Viwanja vya ndege vya mikoa: Moshi, Lindi, Njombe, Musoma na Singida. 3. Miradi ya Uendelezaji wa Miundombinu ya Reli 80. Mheshimiwa Spika, miradi itakayotekelezwa ni: 1. Ujenzi wa reli ya SGR na ukarabati na uboreshaji wa reli za MGR na reli ya TAZARA. 2. ambapo 3. Ujenzi wa Reli ya Treni ya Mjini katika Jiji la Dar es Salaam Upembuzi Yakinifu utafanyika mwaka 2026/27; na Ujenzi wa Kituo cha Kisasa cha Mafunzo ya Reli. 4. Miradi ya Uboreshaji wa Vyuo vya Mafunzo ya Kisekta 81. Mheshimiwa Spika, miradi itakayotekelezwa katika eneo hili ni 1. Ujenzi wa Miundombinu na Ununuzi wa Vifaa vya Kufundishia katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT); 2. Mradi wa Uanzishwaji wa Kampasi ya Lindi katika Sekta ya Usafiri Majini, Mafuta na Gesi; na 30 3. Mradi wa East Africa Skills for Transformation and Regional Intergration (EASTRIP). (Maelezo ya kina kuhusu miradi itakayotekelezwa kwa mwaka 2026/27 na fedha zilizotengwa kwa kila mradi yameainishwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia Aya ya 260 hadi 286) D:2. SHUGHULI NYINGINE ZITAKAZOTEKELEZWA KWA MWAKA 2026/27 82. Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zitakazotekelezwa na Wizara kupitia Mapato ya Ndani ya Taasisi zilizo chini yake katika udhibiti, utoaji huduma za Uchukuzi, na masuala ya kisera na mtambuka zimeanishwa katika Kitabu cha Hotuba yangu Aya ya 287 hadi 314. E. SHUKRANI 83. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2025/26, umeleta mafanikio makubwa. Mafanikinio ambayo Wizara imeyapata yasingewezakana kutokea bila ya ushauri na usimamizi wa Bunge Lako Tukufu. Kutokana na mafanikio hayo, naomba nitoe shukrani za kipekee kwako wewe binafsi Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa ushauri na michango yenu ambayo imewezesha Wizara kufikia mafanikio hayo. Aidha, niwashukuru wananchi na wadau wengine kwa kuendelea kutoa michango ya hali na mali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda miundombinu ya usafirishaji ambayo Serikali imewekeza kiasi kikubwa cha fedha za Umma. 31 84. Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwapongeza na kutambua michango inayotolewa na viongozi wanaonisaidia katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara, kwa kuanza na Naibu Waziri, Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile (Mb.); na Katibu Mkuu, Prof. Godius Walter Kahyarara. Vilevile, niishukuru Menejimenti ya Wizara; Wakuu wa Taasisi za Wizara; pamoja na Watumishi wote wa Wizara na Taasisi kwa juhudi zao katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara na Taifa kwa ujumla. 85. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee nishukuru Taasisi na Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa ambayo yameshirikiana na Wizara katika uendelezaji wa Sekta ya Uchukuzi nchini. Ninaomba kutaja baadhi ya Mashirika ya Kitaifa kama ifuatavyo: Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PSSSF; Taasisi za kifedha za CRDB, NMB, AZANIA BANK, NBC na TCB na Asasi mbalimbali za kiraia. Aidha, Mashirika ya Kimataifa/Wadau wa Maendeleo wanaoendelea kushirikiana na Wizara ambao ni pamoja na: Trade Mark Africa (TMA); Shirika la Bahari Duniani (IMO); Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO); Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO); Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB); Benki ya Dunia (WB); Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA); Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Korea Kusini (KOICA); Foreign Commonwealth and Development Office (FCDO); Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD); Shirika la Nchi Zinazouza Mafuta ya Petroli Nje ya Nchi zao (OPEC); Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU); Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB); Shirika la Chakula Duniani (WFP); na Shirika la Biashara na Maendeleo la Marekani (USTDA). 86. Mheshimiwa Spika, Wizara pia inashukuru ushirikiano kutoka nchi za kikanda kupitia Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Sekretarieti ya Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Vilevile, kutoka 32 Nchi za Urusi; Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE); Uingereza; China; Sweden, Denmark; Korea Kusini; Jamhuri ya Czech; na Uturuki. Na mwisho si kwa umuhimu nishukuru Sekta Binafsi, hususan wafanyabiashara na watoa huduma za uchukuzi kwa kuendelea kutoa huduma za uchukuzi. (Maelezo ya kina ya shukrani yameainishwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia Aya ya 315 hadi 319). F. MUHTASARI WA MAOMBI YA FEDHA YA WIZARA YA UCHUKUZI KATIKA MWAKA WA FEDHA 2026/27 87. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2026/27, Wizara ya Uchukuzi inaliomba Bunge lako Tukufu kuidhinisha bajeti yenye jumla ya Shilingi 2,872,738,082,000. Kati ya fedha hizo, Shilingi 126,041,236,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 2,746,696,846,000 ni fedha za Miradi ya Maendeleo. 88. Mheshimiwa Spika, pamoja na Hotuba hii, nimeambatisha majedwali mbalimbali yenye taarifa na takwimu kwa ajili ya kutoa uelewa zaidi kwa Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kuhusu Sekta ya Uchukuzi. Naomba majedwali hayo ambayo yameainishwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia ukurasa 198 hadi ukurasa 247 yachukuliwe kama sehemu ya hotuba hii. Hotuba hii pia inapatikana katika tovuti ya Wizara (www.uchukuzi.go.tz). 89. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.  


Wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo na wenyeviti wa bodi zake wakisikiliza hotuba ya bajeti hiyo leo



























Wanafunzi wa Shule ya Kiislamu ya  Ira ya Kondoa, wakishuhudia hotuba ya waziri Profesa Mbarawa  ndani ya ukumbi wa Bunge
 

Comments

Popular posts from this blog

WALIOPITA KURA ZA MAONI CCM HAWA HAPA

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?