WABUNGE WA CCM WAWACHAGUA WABUNGE WATATU KWENDA BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI, YUMO MTOTO WA WASIRA
Katibu wa Bunge Baraka I. Leonard akizungumza na wanahabari baada ya kumalizika uchaguzi ndani ya CCM wa wabunge wa Tanzania watakaoingia katika Bunge la Afrika Mashariki kujaza nafasi tatu zilizokuwa wazi, Uchaguzi huo ulifanyika katika ukumbi wa Msekwa jijini Dodoma na mkutano huu wa wanahabari ulifanyika katika Ukumbi wa Spika. Katibu alibainisha haya,
nawajulisha kuhusu Uchaguzi Mdogo utakaofanyika tarehe 4 Mei 2026, kuchagua wajumbe watatu watakaowakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki. Hivyo, tunaomba mfikishe taarifa hii muhimu kwa wananchi.
Uchaguzi huu ni wa kujaza nafasi zilizoachwa wazi katika Bunge la Afrika Mashariki baada ya Mhe. James Kinyasi Millya (Mb), Mhe. Dkt. Ng’waru Jumanne Maghembe (Mb) na Mhe. Angela Charles Kizigha (Mb) kuchaguliwa kuwa Wabunge katika Bunge la Jamuhuri la Muungano wa Tanzania.
Ndugu Waandishi wa Habari Uchaguzi huu mdogo unafanyika kwa mujibu wa Kanuni ya 20 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2025. Kanuni hiyo inaeleza kwamba Uchaguzi Mdogo unapaswa kufanyika ili kujaza nafasi iliyo wazi. Mhe. James Kinyasi Millya (Mb) na Mhe. Dkt. Ng’waru Jumanne Maghembe (Mb) waligombea na kushinda Uchaguzi wa Tarehe 29 Oktoba, 2025 na Mhe. Angela Charles Kizigha (Mb) aliteuliwa na Rais tarehe 2 Aprili 2026 kuwa Mbunge.
Wabunge wote watatu waliapishwa ambapo sasa ni Wabunge wa Bunge la Tanzania. Kwa mantiki, hiyo Wabunge hao wamekoma kuwa wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki kwa mujibu wa Ibara ya 51(3) ya Mkataba wa Kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki, 1999 ikisomwa pamoja na Kifungu cha 7(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Bunge la Afrika Mashariki Na. 4 ya Mwaka 2011. Hivyo hawawezi kuendelea kutumikia Bunge hilo.
Ndugu Waandishi wa Habari, kwa mujibu wa kanuni 18 ya kanuni za Bunge tulimuandikia Spika wa Bunge la Afrika Mashariki kumtaarifu kwamba Wabunge hao wameapishwa kuwa Wabunge wa Tanzania. Spika huyo alitujulisha kwamba nafasi tatu za Tanzania zilizokuwa zimejazwa na Wabunge niliowataja ziko wazi hivyo zinapaswa kujazwa ndani ya siku 90 kwa mujibu wa Kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Bunge hilo.
Ndugu Waandishi wa Habari, Ibara ya 50 (1) ya Mkataba wa Jumuiya imeweka masharti kuhusu Uchaguzi wa Wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki kwamba unatakiwa ufanyike kwa kuzingatia, kwa kadri itakavyowezekana, uwakilishi wa makundi yaliyotajwa katika Ibara hiyo. Kanuni za Bunge zimeainisha makundi ya uwakilishi kuendana na Ibara ya 50 ya Mkataba. Makundi hayo yametajwa chini ya Fasili ya 6(5) na 12 (3) ya Nyongeza ya Tatu ya Kanuni kama ifuatavyo:
(a) Kundi A: Wanawake
(b) Kundi B: Zanzibar;
(c) Kundi C: Walio Wachache Bungeni; na
(d) Kundi D: Tanzania Bara.
Ndugu Waandishi wa Habari, Mhe. Angela Charles Kizigha (Mb) alikuwa ni Mjumbe aliyechaguliwa kupitia Kundi A- Wanawake. Mhe. James Kinyasi Millya (Mb) na Mhe. Dkt. Ng’waru Jumanne Maghembe (Mb) walikuwa Wajumbe waliochaguliwa kupitia Kundi D- Tanzania Bara. Nafasi hizo zilipatikana kwa udhamini wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ndugu Waandishi wa Habari, Ibara ya 50(2) ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inataja sifa za mtu anayestahili kuchaguliwa kuwa Mjumbe katika Bunge la Afrika Mashariki. Sifa hizo ni:
(a) awe raia wa nchi husika;
(b) awe na sifa za kuchaguliwa kuwa Mbunge katika nchi husika;
(c) asiwe waziri katika nchi husika;
(d) asiwe mtumishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na
(e) awe ni mtu aliyedhihirisha uzoefu wake au kuhusika katika kusimamia na kuendeleza madhumuni na malengo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ndugu Waandishi wa Habari, Ibara ya 50(2) (b) inaelekeza Mgombea kuwa na sifa zilizowekwa chini ya Ibara ya 67(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, Ibara hiyo inaeleza:
“67.-(1) Bila kuathiri masharti yaliyomo katika Ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge endapo-
(a) ni raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja, na ambaye anajua kusoma na kuandika katika Kiswahili au Kiingereza;
(b) ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa;
(c) Katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi hakuwahi kutiwa hatiani katika mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya Serikali.”
Ndugu Waandishi wa Habari, Tarehe 14 Aprili, 2026 nilitoa Tangazo katika Gazeti la Serikali na katika vyombo vya Habari. Lengo la tangaazo hilo ilikua Kuutaarifu Umma kuhusu kufanyika Uchaguzi Mdogo wa Wajumbe watatu ili kujaza nafasi katika Bunge la Afrika Mashariki. Aidha, nilitangaza tarehe ya Uteuzi wa Wagombea na siku ya Uchaguzi ni tarehe 4 Mwezi Mei 2026.
Taarifa hiyo ilikitaka Chama Cha Mapinduzi kufanya mchakato wa kupata Wagombea kwa kuzingatia matakwa ya Fasili ya 6 ya Nyongeza ya Tatu ya Kanuni za Bunge. Matakwa hay oni pamoja na kujaza Fomu ya Uteuzi wa Wagombea iliyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge.
Ndugu Waandishi wa Habari, Tarehe 30 Aprili 2026 ilipangwa kuwa Siku ya Uteuzi wa Wagombea. Hadi saa 10:00 Jioni Ofisi yangu ilipokea fomu na stakabadhi za malipo ya ada ya kugombea kutoka kwa Wagombea wafuatao.
(a) Ndg. Fatuma Abdallah Kange
(b) Ndg. Cosato David Chumi
(c) Ndg. Kambarage Masato Wasira
Baada ya Kuchambua Sifa na vigezo vinavyotakiwa kwa Mujibu wa sheria zinazosimamia Uchaguzi huu, nimeridhika kwamba watajwa wana kidhi vigezo vya kugombea nafasi ya Ujumbe katika Bunge la Afrika Mashariki.
Hivyo katika Uchaguzi huu
(a) Ndg Fatuma Abdallah Kange anagombea kujaza nafasi moja iliyo wazi katika Kundi A – Wanawake, na
(b) Ndg. Cosato David Chumi na Ndg. Kambarage Masato Wasira wanagombea Kujaza nafasi mbili zilizo wazi katika Kundi D – Tanzania Bara
Ndugu Waandishi wa Habari, itakapowadia siku ya Uchaguzi, kabla ya Wabunge kupiga kura Wagombea wataruhusiwa kuingia ndani ya Ukumbi wa Bunge, watajitambulisha na wataomba kura kwa lugha ya Kiingereza. Baada ya hatua hiyo Wabunge watapewa fursa ya kuuliza maswali ya papo kwa papo kwa idadi itakayoamuliwa na Spika. Kisha zoezi la kupiga kura litaanza, Kura zitahesabiwa na washindi watatangazwa.
Ndugu waandishi wa Habari, Uchaguzi huu unakusudia kupata wawakilishi wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki. Wananchi wana haki ya kupata Taarifa kuhusu namna wawakilishi wao wanavyopatikana. Hivyo, ni vyema mfikishe maelezo kuhusu uchaguzi huu kwa Wananchi ili waweze kushirikiana na Wajumbe watakaochaguliwa katika kutekeleza majukumu yao ya uwakilishi.
Asanteni kwa kunisikiliza
Baraka I. Leonard
KATIBU WA BUNGE
Katibu wa Bunge Baraka, akisisitiza jambo kwa wanahabari
Comments
Post a Comment