UHURU WA HABARI HAUWEZI KUDUMU BILA UCHUMI IMARA KWA WANAHABARI. WAZIRI MAKONDA

@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema uhuru wa vyombo vya habari hauwezi kuwa wa kweli kama wanahabari wenyewe hawana uhakika wa kiuchumi.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani jijini Arusha, Makonda ameeleza kuwa hali ya kipato duni kwa wanahabari inawafanya kuwa rahisi kushawishiwa na maslahi ya wanasiasa au wafanyabiashara, hali inayohatarisha uadilifu wa taaluma hiyo.
Amebainisha kuwa kuna baadhi ya mifumo isiyo rasmi ambapo watu wenye maslahi binafsi hufadhili wanahabari au vyombo vya habari ili kulinda taswira zao, jambo linalodhoofisha ukweli na kuathiri maamuzi ya wananchi.
Aidha, amesisitiza haja ya kuhamisha mwelekeo wa vyombo vya habari kutoka kwenye “ku-brand watu” kwenda kwenye kuibua fursa za kiuchumi, hasa katika sekta zenye tija kama utalii, ili kujenga msingi imara wa mapato kwa tasnia ya habari.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema kuwa lengo la Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ni kutathimi na kulinda hali ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.
Ameongeza kuwa kupitia Maadhimisho hayo Serikali itapata fursa ya kukutana na washirika wake wa maendeleo na asasi za kiraia kujadili masuala ya mabadiliko ya utendaji kazi katika sekta ya habari pamoja na kuwaendeleza watayarishaji wa maudhui.
Naye, Mkurugenzi wa Taasisi ya Tech and Media Convergency (TMC) na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho hayo kwa mwaka 2026, Asha Abinallah amesema kuwa kupitia Maadhimisho hayo wadau wameandaa mapendekezo kadhaa ikiwemo kuitaka Serikali kuharakisha uanzishwaji wa Mfuko wa Habari na kuandaa sera rafiki za kuvutia uwekezaji katika sekta ya habari.
Vilevile, wameitaka Serikali kupitia Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kuendelea kutimiza majukumu yake ikiwemo kuwajengea uwezo wanahabari katika matumizi ya akili unde.

Comments
Post a Comment