WAZIRI MKUU DKT. MWIGULU AAGIZA WATENDAJI NCHINI WAJIPANGE KUHUSU UWEKEZAJI USIOKUWA NA UBABAISHAJI
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alishasema isiwepo sheria inayoleta kikwazo katika utendaji kazi wa serikali. Haya tuliyoyabaini, tuyaweke kwenye majedwali na kubainisha lipi ni kikwazo na lipi limefanyika. Leteni hayo mapendekezo.”
“Kuhusu suala la utitiri wa taasisi za udhibiti na kodi, andaeni mapendekezo mahsusi na yawasilishwe kwa Waziri wa Fedha ili yaweze kuingizwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha (Finance Bill) wa mwaka huu. Hatua hii inalenga kuwa sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini,” amesema Dkt. Mwigulu.
Aidha amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe zinaondoa urasimu katika kuanzisha biashara mpya au viwanda vipya katika maeneo yao. “Kufanya hivyo, kutasaidia kuchochea upatikanaji wa ajira mpya kwa vijana, kukuza kipato kwa wawekezaji na wafanyabiashara pamoja na kukuza pato la Taifa.”
Amezitaka mamlaka hizo ziweke mikakati ya kushughulikia changamoto mbalimbali zikiwemo za tozo zisizo rafiki kwa sekta binafsi. “Ni dhahiri kuwa Serikali pekee haiwezi kufanikisha malengo haya bila ushiriki mpana na madhubuti wa sekta binafsi,” amesema.
Mapema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo aliwashukuru Wakuu wa Mikoa yote kwa ushirikiano wao na jinsi walivyolipa kipaumbele suala la uwekezaji kwenye maeneo yao.
Alisema ofisi yake kwa kushirikiana na Waziri wa Nchi, OWM – TAMISEMI wanaandaa nyenzo za kushindanisha mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa (Ease of Doing Competitive Business) katika kuvutia uwekezaji na kulinda biashara.
“Kupitia hii kila mkoa utapimwa jinsi wanavyowezesha biashara na kuvutia uwekezaji ili kuona wanakuza vipi biashara katika maeneo yao. Na watapimwa ufanisi wao kila mwaka mara moja,” alisema.
Naye, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar aliwaeleza washiriki wa mkutano huo kwamba matarajio ya Serikali kwenye utekelezaji wa DIRA 2050 unaendana na MKUMBI II kwenye maeneo yao.
“Uchumi wa nchi yetu kwa sasa ni dola za Marekani bilioni 100 tukichanganya uzalishaji wa bidhaa zetu zote, huduma na biashara za ndani na za nje angalau kwa hesabu za mwaka jana. Katika miaka 25 ijayo, tunataka tufikie dola za Marekani trilioni moja, maana yake tukue zaidi ya mara 10.”
“Ili tufike huko hatupaswi kwenda kama ilivyo sasa, tunapaswa kubadilika sana na tuongeze bidii siyo tu uchumi ukue bali uwe wa kisasa pia,” alisema.
Wakuu wa mikoa nchini wakiwa katika mkutano huo
Askari Polisi wa Blasbendi ya Jeshi la Polisi nchini akiburudisha katika mkutano huo
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, akizungumza kwenye mkutano huoWaziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, akizungumza mbele ya Waziri MkuuWakuu wa mikoa wakibadilishana mawazo baada ya kumalizika mkutano huo

Comments
Post a Comment