WATUMISHI WA MAHAKAMA YA TANZANIA KUHAMIA DODOMA NDANI YA MIEZI MITATU IJAYO
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Mhagama (kulia) akisalimiana leo na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Mohamed Siyani(kushoto ) alipowasili katika viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo kwa ajili ya hafla ya uzinduzi wa majengo ya Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo, Tandahimba, Nanyumbu , na Ngara.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mhe Gloria Lwomile (kulia) akitoa maelezo leo kwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Mohamed Siyani(kushoto) alipowasili katika viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo kwa ajili ya hafla ya uzinduzi wa majengo ya Mahakama ya Wilaya ya Tandahimba, Nanyumbu , Namtumbo na Ngara.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Mohamed Siyani(mwenye mkasi ) akikata utepe leo kuashiria uzinduzi wa majengo ya Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo, Tandahimba, Nanyumbu na Ngara.
@@@@@@@@@@@@@@@@@@@
Na Tiganya Vincent-Mahakama –Namtumbo
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amesema kuwa katika miezi mitatu ijayo kuanzia sasa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania yaliyopo Dodoma yatakuwa tayari yamekamilika kwa ajili ya watumishi wote kuhamia kwenye majengo yake mapya.
Alizungumza hayo leo katika halfa ya uzinduzi wa Mahakama za Wilaya ya Namtumbo, Ngara, Nanyumbu na Tandahimba ilifanyika katika Viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Mhe. Siyani alisema hatua kubwa imepigwa katika ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania Dodoma ambapo ujenzi umefikia asilimia 78.
Aidha Mhe. Siyani alisema uzinduzi wa Mahakama za Namtumbo, Nanyumbu, Tandahimba na Ngara ni matokeo ya uwezeshwaji unaoendelea kufanywa na Serikali pamoja na usimamizi na utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano wa Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu wa Mahakama ya Tanzania.
Aliishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka misingi mizuri inayoiwezesha Mahakama kujenga miundombinu yake na hivyo kuwa na mazingira mazuri yanayoiwezesha Mahakama kutimiza wajibu wake.
Mhe. Siyani aliwahikikishia wananchi kwamba Mahakama itaendelea kujenga na kuboresha miundombinu yake katika ngazi zote.
Alisema ujenzi wa majengo hayo na mengine yanayoendelea kujengwa kote nchini, unaenda sambamba na uwekaji wa miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za Mahakama.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alisema tayari timu ya kwanza imeshahamia Dodoma tangu tarehe 29 Desemba 2022 na timu zinatarajiwa kuendelea kuhamia Makao Makuu ya Mahakama hivi karibuni.
Kwa upande wa Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Leonard Magacha alisema ujenzi wa majengo ya Mahakama za Wilaya ya Namtumbo, Nanyumbu, Ngara na Tandahimba umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.9 , fedha hizo zimetokana na mapato ya ndani ya nchi.
Comments
Post a Comment