‘Dunia inanenepa’, hakuna hatua zinazochukuliwa kuizuia
Kwa sasa tunaishi katika dunia yenye watu wenye uzito kupindukia kuliko uzito wa chini
Marekani inaongoza duniani kwa wenye uzito kupindukia kumbuka hawa ni askari je mazoezi hayasaidii
Roboti zinafanya kazi zilizokuwa zikifanywa na binadamu kuanzia zile za shuruba hadi nyepesi na kuwafanya wengi wakose kujishughulisha
wanene wakipiga tizi kupunguza miili
Marekani inaongoza duniani kwa wenye uzito kupindukia kumbuka hawa ni askari je mazoezi hayasaidii
Roboti zinafanya kazi zilizokuwa zikifanywa na binadamu kuanzia zile za shuruba hadi nyepesi na kuwafanya wengi wakose kujishughulisha
wanene wakipiga tizi kupunguza miili
MAJESHI ya uchumi hayalali ili kuongeza utajiri na hivyo
moja kwa moja kusababisha ongezeko kubwa la watu wenye uzito wa kupindukia
duniani.
Mwelekeo huo unatufanya sasa tuishi katika dunia yenye watu
wengi wenye uzito wa kupindukia zaidi ya wale wenye uzito wa chini.
Kwa ongezeko la kipato, mataifa yanaongeza kiwango cha
matumizi ya milo yenye kalori nyingi, watu wanahamia mijini kutoka vijijini
kufuata kile wanachokiona fursa nono zilizopo huko.
Wakiwa mijini watu wanakutana na vyakula vya holela (junk
food) pamoja na vinavyotokana na usindikaji viwandani kwa gharama nafuu,
ambavyo bila kujiuliza mara mbili mbili wanavitia tumboni siku hadi siku.
Mashine, hasa roboti sasa zinafanya kazi nyingi, ambazo awali
zilikuwa zikifanywa na binadamu na hivyo kupunguza kiwango cha nishati inayojishughulisha
mwilini.
Hilo moja kwa moja linatengeneza kundi la watu
wasiojishughulisha, ambao unaweza kusema wanaishi kivivu.
Kwa sasa kuna mataifa 114 duniani, ambayo zaidi ya nusu ya
watu wake wazima wanahesabika kuwa wanene kupindukia ikiwamo sehemu kubwa za
Amerika, Ulaya na Mashariki ya Kati kwa mujibu ya takwimu za Shirika la Afya
Duniani (WHO).
Katika mataifa madogo ya visiwa vya Pasifiki na mataifa ya
Ghuba ya Uajemi, zaidi ya theluthi mbili ya watu wake wanahesabika kuwa wenye
uzito wa kupita kiasi au wanene.
Katika takwimu hizo,
China na Marekani, ambazo ndizo zinazoongoza duniani kwa ukubwa wa uchumi wao,
pia zinaongoza kwa wingi wa watu wenye uzito wa kupindukia.
Wakati ikiwa hivyo, Uingereza inaongoza mataifa ya Ulaya
kwa uzito mkubwa miongoni mwa watu wake huku Japan likiwa taifa tajiri lililo
na watu wachache wenye uzito mkubwa.
Ikimaanisha kuwa Wajapan ni watu wenye kudhibiti ulaji wao
pamoja na kuwa na mazoea ya kujishughulisha licha ya utajiri na wingi wa roboti
zilizopora kazi za shuruba za binadamu.
Kwa mujibu wa utafiti mpya, zaidi ya watu milioni 640
wameongeza unene uliopindukia mwilini, kiwango kikubwa kuliko cha wale wenye uzito
mdogo wa kupindukia.
Utafiti huo umeonesha kuwa mmoja kati ya wanaume 10 ana
unene wa kupita kiasi huku mmoja kati ya wanawake saba akiwa katika hali hiyo
pia.
Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, idadi ya watu wanene
wenye uzito wa kupindukia imeongezeka mno.
Watu walio na viwango vya vipimo 30 na zaidi vya kisayansi
vinavyolinganisha urefu na uzito wa binadamu yaani kwa Body Mass Index (BMI),
wameongezeka kutoka watu milioni 105 mwaka 1975 hadi watu milioni 641 mwaka
2014.
Uzito ulio sawa hubainishwa kisayansi kwa kupima uzito wa
mtu kwa kilo kisha kuugawa na urefu wake kwanzia mguu hadi kichwani.
Uzito huo wa BMI unaozidi 25 huwa umepita kiwango na zaidi
ya 30 ni wa kupindukia, huku unapofika 40 na zaidi huitwa uzito wa ugonjwa kwa
kimombo 'morbidly obese'.
Walioko katika hali hii hupata taabu kupumua na kutembea na
hukumba asilimia moja ya wanaume na asilimia mbili ya wanawake.
Utafiti huo uliofanywa na watafiti 700 na kulijumuisha WHO,
ulihusisha watu wazima milioni 20 kutoka mataifa 186.
Hata hivyo, kama ambavyo tumeona awali hapo juu, wengi ya wanaokumbwa
na hali hii hutoka mataifa yaliyo tajiri na kwa maana hiyo wengi ya wanaotoka mataifa
masikini wana uzito wa chini.
Ripoti ya utafiti huo imeongeza kuwa moja ya tano ya watu
wazima watakuwa na uzito kupindukia ifikapo mwaka 2025.
Profesa Majid Ezzati kutoka Chuo cha Afya ya Umma mjini
London, Uingereza anasema uzito kupindukia unaokumba idadi kubwa ya watu
ulimwenguni kote hivi sasa ni tishio kwa afya zao.
Ameongeza kuwa suala hilo haliwezi kusuluhishwa tu
kimatibabu, au kupunguza bei za dawa za kudhibiti uzito kupindukia wala
kuongeza barabara za matembezi na watu kuendesha baiskeli ili kupunguza uzito,.
Bali anaseme, sharti kuwe na mikakati kabambe duniani
ikiwemo kupunguza bei za vyakula vinavyokuza lishe bora na kuongeza bei za
vyakula vinavyozidisha uzito mwilini mfano sukari na vyakula vinavyotengenezwa
viwandani.
Hata hivyo, uzito uliopungua pia umetajwa kuwa changamoto
katika baadhi ya mataifa, mfano robo ya watu katika bara Asia wamepungukiwa
uzito.
Katika Afrika ya Kati na Mashariki asilimia 12 ya wanawake
na 15 ya wanaume wanao uzito uliopungua viwango vinavyohitajika.
Awali ukiwa umehesabiwa kama tatizo la nchi za kipato cha
juu tu, unene kwa sasa unapaa pia katika nchi za kipato cha chini na hasa cha
kati hasa katika maeneo ya mijini.
Katika mataifa
yanayoendelea hasa yanayokuja juu kiuchumi ambayo yaliwekwa na Benki ya Dunia
kama mataifa ya kipato cha chini na kati, viwango vya ongezeko la watoto wenye
uzito kupindukia na unene umeongezeka zaidi ya asilimia 30 ya nchi zilizoendelea.
Uzito wa kupindukia na unene unahusishwa na vifo zaidi
duniani kuliko uzito mdogo wa kupindukia.
Kwa maneno mengine wengi wa watu duniani wanaishi katika
nchi ambazo uzito wa kupindukia na unene unaua watu zaidi kuliko zenye uzito
mdogo kupindukia.
Nini kinasababisha
unene na uzito kupindukia?
Kimsingi sababu ya unene na uzito kupita kiasi ni
kutokuwepo uwiano baina ya kalori zinazoingia na kutoka mwilini.
Duniani kwa sasa imeshuhudia; ongezeko la vyakula vyenye
wanga ambavyo vina mafuta kwa wingi; na ongezeko la watu wasiojishughulisha
kimazoezi kutokana na ongezeko la wingi wa kazi, kubadili mifumo ya usafiri na
ukuaji wa miji.
Mabadiliko ya mlo na kukosekana ujishughulishaji kimazoezi mara
nyingi hutokana na mabadiliko ya kimazingira na kijamii yanayotokana na kupigwa
hatua za maendeleo na ukosefu wa sera zinazounga mkono sekta kama vile afya,
kilimo, uchukuzi, mipango mijini, mazingira, usindikaji vyakula, usambazaji,
masoko na elimu.
Nini
kifanyike?
Ongezeko la upatikanaji wa chakula na ukuaji wa utajiri na
miji kunatarajia kuendelea, hali ambayo itaendelea kuongeza watu wanene
kupindukia.
Kwa sababu hiyo, kuna umuhimu wa uzingatiaji wa masuala ya
afya, mipango miji, kilimo, usindikaji vyakula, mazingira, masoko na elimu na
hasa wakati wa utengenezaji wa sera zinazolenga kukuza utajiri yaani za kiuchumi
na kibiashara.
Hatua hizo ni pamoja na kuhakikisha unafuu wa bei za vyakula
bora na kuongeza kodi kwa vile vya kusindika viwandani na vyenye kalori nyingi.
Bila kuchukua hatua kama hizo, dunia itazidi kunenepa na
kufikia kiwango ambacho tutashtuka tumechelewa kuchukua hatua.




Comments
Post a Comment