LEO NI SIKU YA TAKWIMU BARANI AFRIKA
Mkurugenzi wa Taifa ,Uchumi na Sera wa Benki Kuu (BoT), Johnson Nyella, akisoma hotuba kwa niaba ya Gavana wa Benki kuu katika maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, hebu fuatilia hotuba hiyo hapa chini
Wageni waalikwa katika maadhimisho hayo wakisikiliza hotuba
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk. Albina Chuwa, akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika, yaliyofanyika jijini Dar es salaam leo. Hebu fuatilia hotyuba yake hapo chini=,.
Picha ya pamoja na wanafunzi wa shule za Sekondari mkoa WA dAR ES salaam
HOTUBA YA MGENI RASMI,
GAVANA WA BENKI KUU
TANZANIA,
WAKATI WA MAADHIMISHO
YA SIKU YA TAKWIMU AFRIKA TAREHE 20 NOVEMBA, 2017 KATIKA
UKUMBI WA KIMATAIFA WA MIKUTANO WA MWALIMU JULIUS NYERERE,
DAR ES SALAAM
Mwenyekiti
wa Bodi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu;
Mkurugenzi
Mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu;
Menejimenti
ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu;
Mtakwimu
Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar,
Washiriki
kutoka katika Wizara, Idara na Taasisi za Umma na Sekta Binafsi;
Wawakilishi
wa Vyuo Vikuu na Taasisi za Utafiti Tanzania;
Wawakilishi
wa shule za Sekondari;
Wadau
wa Maendeleo;
Wageni
Waalikwa;
Waandishi
wa Habari;
Mabibi na Mabwana.
Ndugu Mwenyekiti, awali ya yote
napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha
kukutana siku ya leo ili kuadhimisha SIKU
YA TAKWIMU AFRIKA KWA MWAKA 2017. Aidha,
natoa shukrani zangu za dhati kwa heshima kubwa mliyonipa ya kuwa Mgeni Rasmi
katika maadhimisho haya muhimu.
Ndugu Mwenyekiti,
napenda kutumia fursa hii kuwakumbusha Washiriki wenzangu kuwa Siku ya Takwimu Afrika huadhimishwa
kila tarehe 18 Novemba ya kila mwaka. Siku
hii hutoa fursa kwa Nchi kutathmini na kufuatilia malengo yaliyofikiwa katika
Mipango ya Maendeleo ya ndani na nje ya Nchi. Kama alivyotangulia kusema
Mkurugenzi Mkuu, kauli mbali mbali zimekuwa zikijadiliwa kila mwaka tangu mwaka
1990, na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Takwimu Bora za Uchumi kwa Maisha Bora”.
Ndugu Mwenyekiti, kabla sijaanza kuzungumzia kaulimbiu hii, naomba
nitoe kwanza baadhi ya takwimu za kiuchumi kwa nchi ya Tanzania, kwa miaka ya
hivi karibuni. Takwimu
za uchumi ni pamoja na takwimu zinazohusu pato la taifa, mfumuko wa bei, viwanda,
ujenzi, kilimo, utalii n.k. Tanzania ni
kati ya nchi za Afrika zenye viwango vya juu vya ukuaji wa uchumi katika
kipindi cha muongo mmoja uliopita (2007 - 2016). Uchumi wa nchi ulikua kwa wastani wa asilimia
6.7. Mwaka 2016, Pato la Taifa lilikua kwa
wastani wa asilimia 7.0, sawa na ilivyokuwa mwaka 2015 na 2014. Kwa miaka minne mfululizo, mfumuko wa bei wa
Taifa umeendelea kupungua na kubaki katika kiwango cha tarakimu moja. Mwaka 2016, mfumuko wa bei ulipungua na
kufikia wastani wa asilimia 5.2 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5.6 mwaka
2015 na asilimia 6.1 mwaka 2014.
Ndugu
Mwenyekiti, katika kipindi
hicho, sekta ya viwanda ilikua kwa wastani wa asilimia 7.5 na kuchangia wastani
wa asilimia 6.5 katika Pato la Taifa. Kiwango
cha ukuaji wa shughuli za kiuchumi za kilimo kwa mwaka 2016, kilipungua na kuwa
asilimia 2.1 ikilinganishwa na asilimia 2.3 mwaka 2015. Mwaka 2014 ukuaji wa shughuli za kiuchumi za
kilimo ulikua kwa asilimia 3.4. Shughuli za kiuchumi za kilimo zilichangia
asilimia 29.0 ya Pato la Taifa mwaka 2015 na 2016. Mapato yatokanayo na biashara ya utalii yaliongezeka hadi dola za
Marekani milioni 2,073 kutoka dola za Marekani milioni 1,901.9 mwaka 2015, sawa
na ongezeko la asilimia 9.0. Ongezeko
hilo lilitokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii waliotembelea nchini kwa
asilimia 12.9 kutoka watalii 1,137,182
mwaka 2015 hadi watalii 1,284,279 mwaka
2016.
Ukuaji wa uchumi kwa kiasi kikubwa uliendana
na kasi ya kupungua kwa umaskini. Umaskini ulipungua kutoka asilimia 34.4 mwaka
2007 hadi asilimia 28.2 mwaka 2012. Kwa
kipindi cha miaka 15 umaskini ulipungua kwa asilimia 4.6. Kwa kipindi cha miaka mitano ya karibuni
umaskini ulipungua kwa asilimia 6.2.
Ndugu
mwenyekiti,
takwimu bora za uchumi ni muhimu katika kupanga mipango ya maendeleo na
utungaji wa sera kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi. Wakati nchi mbali
mbali duniani ikiwemo Tanzania zimeanza kutekeleza Agenda ya Maendeleo Endelevu
ya Mwaka 2030, mahitaji ya takwimu bora za uchumi yanahitajika sana. Tathmini
ya utekelezaji wa malengo haya italeta changamoto kubwa hasa kwa nchi
zinazoendelea kutokana na mahitaji makubwa ya takwimu bora. Njia mojawapo ya kutatua changamoto hizi ni
kwa wadau mbalimbali wa takwimu kufanya kazi kwa ushirikiano. Wadau hao ni pamoja na wazalishaji na
watumiaji wa takwimu, taasisi za elimu ya juu, sekta binafsi na asasi za
kiraia.
Ndugu Mwenyekiti, takwimu bora za
kiuchumi zinasaidia kuongeza tija serikalini katika kupanga mipango ya
maendeleo na kukabiliana na changamoto kadri zinavyojitokeza. Aidha, takwimu bora zinasaidia watunga sera na
watekelezaji wa programu mbali mbali na kupanga mikakati mipya ya kuboresha
maisha ya wananchi.
Ndugu Mwenyekiti, Serikali kwa
kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaimarisha Mfumo wa Takwimu nchini kwa lengo
la kupata takwimu bora za kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uimarishaji wa
utungaji wa sera na tathmini za mipango yetu ya maendeleo kama vile Mpango wa
Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17-2020/21.
Ndugu Mwenyekiti, Sote kwa ujumla wetu tunafahamu umuhimu wa
viashiria vya uchumi jumla katika kuwavutia wawekezaji hapa Nchini na hususani
katika Viwanda vyetu; ukizingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ya kuiwezesha
Tanzania kufikia hadhi ya nchi zenye uchumi wa kipato cha kati unaoongozwa na
uchumi wa viwanda. Hivyo, Serikali inahitaji
kupata kwa wakati takwimu za uchumi zenye ubora unaozingatia Kanuni zilizowekwa
na Ofisi ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa.
Ndugu
Mwenyekiti,
niruhusu nitoe ufafanuzi kuhusu Sheria ya Takwimu Na. 9 ya Mwaka 2015 ili
kuondoa mkanganyiko uliojitokeza kutokana na maudhui ya sheria husika. Sheria hii haina lengo la kuzuia taasisi au
watu binafsi kufanya tafiti zao hapa nchini, ila inalenga kuweka misingi inayotakiwa
kuzingatiwa na wadau katika utoaji wa takwimu rasmi. Kuanzishwa kwa sheria hii kunalenga kutoa
miongozo kwa taasisi za Serikali, mashirika na watu binafsi wanaotoa takwimu rasmi
nchini kuendesha shughuli za ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji unaozingatia
weledi na taratibu zinazokubalika.
Ndugu
Mwenyekiti,
kabla ya kuhitimisha naomba nitoe wito kwa jamii ya watakwimu. Kutokana na mahitaji makubwa ya takwimu kwa
matumizi mbalimbali, ni muhimu kuimarisha mbinu za uzalishaji wa takwimu kwa kutumia
teknolojia za kisasa. Matumizi ya
teknolojia yataipunguzia Serikali gharama za uzalishaji wa takwimu na kuongeza
ubora.
Pili;
hakikisheni kuwa wadau wote waliopo kwenye mfumo wa utoaji na utumiaji wa
takwimu mnashirikiana katika uzalishaji wa takwimu ili kupunguza “kukosekana
kwa ulinganifu wa takwimu (data inconsistencies)” na duplications effort.
Tatu; endeleeni
kuongeza nguvu zaidi katika kuelimisha umma kuhusu matumizi ya takwimu bora
katika kupanga, kufuatilia na kutathmini mipango ya maendeleo ya Afrika na Nchi
yetu kwa ujumla. Waelimisheni Wahariri wa Vyombo vya Habari ili watusaidie
kutoa elimu ya matumizi bora ya takwimu kwa wadau wote ndani na nje ya Nchi.
Ndugu
Mwenyekiti, Wageni
Waalikwa, Mabibi na Mabwana, kabla sijahitimisha hotuba yangu ninapenda
kutambua michango mbalimbali ya wadau wote wanaounga mkono juhudi za serikali
katika kuboresha tasnia ya Takwimu hapa Nchini. Wadau hawa ni pamoja na Benki ya Dunia, DFID,
Jumuia ya Ulaya, JICA, IMF, USAID, SIDA, CANADA, Mashirika ya Umoja wa Mataifa
– UNICEF, UNFPA, UNDP, FAO, Irish Embassy na wadau wengine wote wa Maendeleo.
Aidha,
nishukuru Vyombo vya Habari kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha katika juhudi
za kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa Takwimu katika kupanga na kutathimini
mipango ya maendeleo. Niwaombe wadau wote wa Takwimu nchini, hasa wananchi,
kuendelea kutoa ushirikiano katika mazoezi mbalimbali ya ukusanyaji wa Takwimu
yanayofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kutoa taarifa sahihi. Taarifa
hizo zinaiwezesha Serikali kujipima na kuandaa mipango ya kuboresha maisha ya
wananchi.
Baada ya kusema
haya, napenda nitumie fursa hii kutamka rasmi kuwa MAADHIMISHO YA SIKU YA TAKWIMU AFRIKA 2017 yamefunguliwa
rasmi. Mwenyezi Mungu awabariki.
Ahsanteni
kwa kunisikiliza.
Wageni waalikwa katika maadhimisho hayo wakisikiliza hotuba
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk. Albina Chuwa, akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika, yaliyofanyika jijini Dar es salaam leo. Hebu fuatilia hotyuba yake hapo chini=,.
MAELEZO MAFUPI YA
MKURUGENZI MKUU WA
OFISI YA TAIFA YA
TAKWIMU, DKT. ALBINA CHUWA
WAKATI WA MAADHIMISHO YA SIKU YA TAKWIMU AFRIKA TAREHE 20 NOVEMBA, 2017
KATIKA UKUMBI WA KIMATAIFA WA MIKUTANO WA MWALIMU NYERERE,
DAR ES SALAAM
Ndugu Mgeni Rasmi;
Mwenyekiti wa Bodi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu;
Menejimenti ya
Ofisi ya Taifa ya Takwimu;
Watakwimu na
Wachumi kutoka katika Wizara, Idara na Taasisi za Umma na Sekta Binafsi;
Wawakilishi wa Vyuo
Vikuu, Asasi za kiraia na Taasisi za Utafiti;
Wawakilishi wa
Shule za Sekondari;
Wadau wa Maendeleo;
Wageni Waalikwa;
Waandishi wa
Habari;
Mabibi na Mabwana.
Ndugu Mgeni Rasmi, napenda kuungana
na Watakwimu na Washiriki wote mliokusanyika siku ya leo kwa lengo la
kuadhimisha SIKU YA TAKWIMU AFRIKA KWA
MWAKA 2017. Pia nitumie fursa hii,
kutoa shukrani zangu za dhati kwako pamoja na wageni wote mlioalikwa, kwa
kuweza kuhudhuria maadhimisho haya pamoja nasi.
Mwenyezi Mungu awabariki.
Ndugu Mgeni Rasmi,
kila tarehe 18 Novemba ya kila mwaka Tanzania huungana na nchi zingine za kiafrika
kuadhimisha Siku ya Takwimu Afrika .
Madhumuni makubwa ya kuadhimisha siku
hii ni kuongeza
uelewa wa umma juu ya umuhimu wa takwimu katika nyanja zote za kimaisha ya
kijamii na kiuchumi. Kauli Mbiu ya mwaka
huu ni “Takwimu bora za uchumi kwa
maisha bora" na inalenga kusisitiza umuhimu wa takwimu za kiuchumi
katika kuleta maendeleo endelevu, na hivyo kuboresha maisha ya wananchi barani
Afrika.
Ndugu Mgeni Rasmi, tangu mwaka 1990, maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika huwa
yanaandaliwa kutokana na kaulimbiu mbali mbali zinazohusiana na umuhimu wa
takwimu katika kupanga maendeleo na kutunga sera katika Bara la Afrika. Kati ya kaulimbiu ambazo zimeshajadiliwa tangu
mwaka 1990 ni pamoja na usawa wa jinsi, hali ya mazingira, takwimu huria,
ulemavu na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uzalishaji wa takwimu.
Ndugu
Mgeni Rasmi,
kaulimbiu hizi huandaliwa na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya
Uchumi ya Afrika (UNECA) kwa kushirikiana na Ofisi za Takwimu
za Afrika. Nchi za Afrika zilikubaliana
kuwa kaulimbiu “Takwimu Bora za Uchumi kwa Maisha Bora” iadhimishwe mwaka huu
kwa sababu ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa takwimu za uchumi, unahitaji
weledi mkubwa hususani katika kipindi hiki cha utekelezaji wa Agenda ya Afrika
ya mwaka 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030. Hapa Nchini kaulimbiu ya mwaka huu inaenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa
ya Maendeleo 2025 na Mpango wa Pili wa Maendelo wa Taifa (2016/17 hadi 2020/21). Kama mnavyofahamu Programu zote hizi zinalenga
kukuza uchumi na kupunguza umaskini hapa Nchini.
Ndugu
Mgeni Rasmi, ili takwimu
zitumike kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi, zinahitajika kuwa takwimu
bora na za kuaminika. Takwimu bora ni
takwimu zilizo sahihi, zinazotolewa kwa wakati, linganifu na za kina na
zinazozalishwa mara kwa mara na zenye ufanisi. Sifa hizi zote zinaendana na
Kanuni za msingi za takwimu rasmi za Umoja wa mataifa na Mkataba wa takwimu wa
Afrika ambazo nasi tumeridhia. Pia, takwimu
bora ni lazima ziweze kupatikana kirahisi na kutumika na watumiaji wa aina
mbalimbali na ziwe kwenye wigo mpana kuweza kukidhi mahitaji ya watunga sera na
jamii kwa ujumla.
Ndugu Mgeni Rasmi, takwimu bora za uchumi kwa nchi yetu ni za muhimu
sana, hasa wakati huu ambao Serikali yetu inaimarisha Uchumi wa Viwanda, ili
Tanzania iweze kuwa Nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 na hivyo
kuboresha zaidi maisha ya wananchi. Takwimu
hizi za uchumi ni pamoja na takwimu za kilimo, viwanda, ujenzi, usafirishaji, nishati,
biashara, mazingira, mfumuko wa bei na uwekezaji.
Ndugu Mgeni Rasmi, kwa kutumia takwimu, tunaweza kujua muundo wa kisekta na mwenendo wa uchumi na kwa hiyo sera zinazochochea ukuaji wa uchumi zinaweza kutungwa au kupitiwa upya. Kwa mfano, sekta ya kilimo huchangia sehemu kubwa ya shughuli za kiuchumi katika nchi zinazoendelea, inatengeneza ajira nyingi na hivyo inaboresha maisha ya wananchi. Mwaka 2016 sekta ya kilimo hapa nchini ilichangia asilimia 29.1 katika pato la Taifa. Takwimu za kilimo hutoa taarifa za pembejeo na kipato kutokana na kilimo, pia inajumuisha uzalishaji wa mazao, bidhaa za mifugo, misitu na bidhaa za uvuvi, matumizi ya ardhi, mitambo ya kilimo, matumizi ya maji, mbolea, na dawa. Maendeleo ya takwimu za kilimo ni muhimu kwa ufuatiliaji wa kupunguza umasikini, usalama wa chakula, utunzaji wa mazingira, na kuboresha maisha ya wananchi.
Ndugu Mgeni Rasmi, takwimu za nishati zinasaidia kuelewa hali ya nishati nchini, asilimia ngapi ya nishati mbadala kama vile umeme jua, biogas, na vyanzo vingine vya nishati bora na endelevu inatumika Nchini. Pia hutumika kusaidia kuelewa jinsi gani na ni wapi nishati husambazwa, kiasi gani cha nishati kilichopotea wakati wa usambazaji kwenye gridi ya taifa na athari zake juu ya upatikanaji na uhakika wa usambazaji wa nishati nchini. Ugavi endelevu wa nishati na ufanisi wa usambazaji huhakikisha kuwa nchi inaweza kutoa nishati bora kwa wakazi wake. Hapa Tanzania mwaka 2016, shughuli za kiuchumi za usambazaji umeme zilikua kwa asilimia 8.5 ikilinganishwa na ukuaji halisi wa asilimia 5.8 mwaka 2015.
Ndugu Mgeni Rasmi, maendeleo ya viwanda ni kipaumbele cha nchi katika kufikia uchumi wa kati. Katika kipindi cha mwaka 2007 – 2016, takwimu zinaonesha sekta ya viwanda ilikua kwa wastani wa asilimia 7.5 na kuchangia wastani wa asilimia 6.5 katika pato la taifa. Sekta hii inaajiri wastani wa asilimia 3.1 ya nguvu kazi na kuna fursa ya kuongeza ajira, kupunguza umaskini, kuongeza mapato ya mauzo nje na kukuza uchumi.
Ndugu Mgeni Rasmi, Utalii ni kichocheo muhimu kwa biashara, hutoa ajira, chanzo cha fedha za kigeni, pia hutoa mahitaji ya ziada nje ya uchumi wa ndani. Takwimu za utalii husaidia kuelewa wapi watalii hutoka na wapi wanapenda kwenda ndani ya nchi; kutambua kama kuna "utalii zaidi" ambao unahitaji kusimamiwa ili kuwa wa kudumu; na ni maeneo gani yanayohifadhiwa kwa ajili ya utalii. Mwaka 2016, jumla ya watalii 991,593 walitembelea hifadhi za Taifa ikilinganishwa na watalii 930,205 mwaka 2015, sawa na ongezeko la asilimia 6.6. Kati ya hao watalii 551,083 walitoka nje ya nchi na watalii 440,510 walitoka ndani ya nchi.
Ndugu
Mgeni Rasmi, kwa unyenyekevu mkubwa naomba kuhitimisha maelezo
yangu kwa kuwashukuru Wadau wa Maendeleo ambao wameendelea kutoa misaada ya raslimali
fedha pamoja na masuala ya kitalaam katika uzalishaji wa takwimu rasmi nchini, nikianza na Benki ya Dunia, DFID, Jumuiya ya
Ulaya, CANADA, Mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine wote wa
Maendeleo.
Ahsanteni
kwa kunisikiliza.
Picha ya pamoja na wanafunzi wa shule za Sekondari mkoa WA dAR ES salaam
Comments
Post a Comment