MIAKA 45 BAADA YA KIFO CHAKE: MZEE ABEID AMANI KARUME MWANAMAPINDUZI ASIYESAHAULIKA KATIKA VISIWA VYA ZANZIBAR


Imeandaliwa na Augustine Chiwinga

MIAKA 45  iliyopita hapo tarehe 7 Aprili, 1972 Rais wa kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Amani Karume aliuwawa kwa kupigwa risasi katika jengo la Makao Makuu ya Chama cha Afro-Shirazi hapo Kisiwandui mjini Zanzibar.

Bwana Abeid Amani Karume muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar alizaliwa katika kitongoji cha Pongwe, Mudiria ya Mwera kisiwani Unguja tarehe 4 Agosti 1905. 
Karume ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia ya watoto watano ya Bwana Amani Karume na Bibi Amina binti Kadir (Amina Kadudu). Bwana Amani Karume na Bibi Amina Binti Kadudu walifunga ndoa huko Mwera.
Bwana Abeid Amani Karume alizaliwa na ndugu wanne wa baba mmoja na mama mmoja ambao ni wanaume wawili na wanawake wawili. Lakini wote walifariki kutokana na maradhi mbalimbali na kubaki yeye peke yake. Kwa upande wa mama mmoja, Abeid Amani Karume alizaliwa na ndugu watatu, wanawake wawili na mwanaume mmoja ambao ni Asha, Shumbana na Othman. Baba yake mzazi Abeid Amani Karume alifariki dunia mwaka 1909 wakati Abeid Amani Karume akiwa na umri wa miaka minne. Bwana Abeid Amani Karume alipata elimu ya Qurani na alianza masomo ya msingi katika skuli ya Mwera mwaka alofariki baba yake wa 1909, ambapo darasa lao lilikuwa la kwanza kuifungua skuli hiyo.


Katika mwaka 1913 wakati akiwa na umri wa miaka 8 mama yake mzazi alimpeleka mjini Unguja kuendelea na masomo. Huko aliishi na mjomba wake aliyekuwa Sajenti katika jeshi la polisi la King African Rifle (KAR). Kwa bahati mbaya muda wake wote wa masomo ulikuwa miaka mitatu. Akiwa mjini Zanzibar Abeid Karume alipata marafiki kadhaa na kuvutiwa mno na harakati za bandari ya Zanzibar.
Kwa wakati huo, bandari ya Zanzibar ndiyo iliyokuwa kubwa Afrika mashariki. Pia Zanzibar, ilikuwa ndiyo kituo kikuu cha biashara katika eneo zima la Afrika mashariki na Maziwa Makuu.
Meli za mataifa ya nje hasa Marekani, Uingereza, Ufaransa na Italia zilitia nanga bandarini Zanzibar kupakia na kupakua bidhaaa mbalimbali. Pia meli nyingi zilifika Zanzibar kuchukua maji safi ya kunywa yatokayo katika chemchem ya Mwanyanya. Meli hizo zilitoa ajira ya muda ya kusafisha mashine na kupangusa moshi. Mara nyingi mabaharia wa meli hizo waliajiri watoto kuwachukulia vikapu vya kununulia vyakula sokoni na kuwalipa ujira mdogo.
Kwa vile alipendelea kazi ya ubaharia, Abeid Amani Karume alifuatana na bwana mmoja aitwae Juma hadi bandarini. Alijumuika na watoto kadhaa waliofuata ajira ya muda huko bandarini. Ajira ya muda aliyoipata Karume huko bandarini ilimfanya akutane na mabaharia wa nchi mbalimbali na hivyo kuvutiwa na uzuri wa maisha ya ubaharia ya kusafiri na kuona nchi na watu mbalimbali. Hali hiyo ilimfanya Karume azidi hamu na ari ya kutafuta kazi ya ubaharia na kumuomba mama yake ruhusa ya kufanya kazi melini. Mwanzoni mama yake mzazi alikataa shauri hilo. Lakini baadaye alikubali ombi hilo baada ya kufahamishwa kuwa meli atakayofanyakazi mwanawe haitosafiri mbali na itatia nanga bandarini Zanzibar mara kwa mara.
Katika mwaka 1919 Abeid Amani Karume alipeleka barua ya kuomba kazi melini lakini alikataliwa kwa vile alikuwa na umri mdogo wa miaka 14. Hata hivyo hakuvunjika moyo na hakurudi Mwera kwa mama yake bali alimtembelea mara kwa mara. Alijiunga na timu za masumbwi na mpira wa miguu na kujuana na watu mbalimbali.
Kwa wakati huo timu za mpira wa miguu zilizojulikana Unguja zilikuwa ni timu ya skuli ya Kiungani iliyoanzishwa na Mwalimu Augostino Ramadhani na John Majaliwa. Mara nyingi timu hiyo ilishindana na timu ya watumishi serikalini. Baadaye kuliundwa timu nyengine za mpira wa miguu ambazo ni Vuga Boys, New Generation, United Service na New Kings. Karume alijiunga na timu ya New Generation na kucheza nafasi ya mstari wa mbele kushoto Inside left. Baadhi ya waanzilishi wa timu hiyo ni Bwana Malingumu, Shaaban Feruzi, Saad Shoka, Masoud Thani na Mzee wa Shangani.
Mara tu baada ya kujiunga na timu hiyo, Karume alichaguliwa kuwa msaidizi nahodha. Katika mwaka 1920 Abeid Amani Karume alikubaliwa kuwa baharia katika meli iliyoitwa Golden Crown (Taji la Dhahabu). Meli hiyo ilichukua abiria na mizigo kati ya bandari ya Zanzibar, Dar es Salaam, Pemba, Tanga, Mombasa na Mikindani huko Kilwa.
Baadaye alishuka katika meli hiyo na kufanya kazi katika meli nyengine iliyoitwa Cheko. Kwa bahati mbaya, meli hiyo iligonga mwamba na kuvunjika huko Kimbiji, nje kidogo ya Dar es Salaam lakini watu wote walinusurika.
Kazi ya ubaharia ilimpa tija Abeid Amani Karume kwani alinunua nyumba na viwanja kila alipopata nafasi ya kwenda nyumbani. Kwa muda wote huo Abeid Amani Karume alifanyakazi katika meli zilizopata leseni ya kufanyakazi katika mwambao wa Afrika Mashariki.
Katika mwaka 1922, akiwa na umri wa miaka kumi na saba, Abeid Amani Karume alipata kazi katika meli ya kampuni ya British Indian Steam Navigation Company ya Uingereza. Akiwa na kampuni hiyo Karume, alikaa nje miaka mitatu hadi 1925, aliporejea nyumbani kwa mapumziko.Tayari wakati huo, Karume alikwishatembelea nchi za Japan,Comoro,Madagascar,China,Singapore,New Zealand,Uingereza,Marekani,Canada,Ufaransa, Ubelgiji, India,Ureno,Hispania,Arabuni,Italia na Ugiriki.
Baada ya kupumzika kwa muda, Abeid Amani Karume alijiunga na kampuni ya Eastern Telegraph Company na kufanya kazi katika meli ya kampuni hiyo iitwayo Caranja. Meli hiyo ilikuwa ikitandika waya za simu baharini kati ya Zanzibar na Aden. Aliendelea na kazi ya ubaharia hadi mwaka 1938 alipoacha kazi hiyo kutokana na sababu mbalimbali. Karume alishauriwa na mama yake mzazi kuacha kazi hiyo. Vilevile aliacha kazi hiyo kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama duniani. Wakati huo, tayari vita vikuu vya pili vya dunia vilikaribia. Baadhi ya kazi alizofanya katika meli hizo ni Greaser, Fireman, Sailor na Headsailor.
Katika kipindi fulani cha kazi yake ya ubaharia, Abeid Amani Karume alifanyakazi chombo kimoja na Khamis Heri Ayemba kutoka Tanga. Wote wawili walirudi nyumbani wakati vita vya pili vya dunia vinakaribia. Baada ya kuacha kazi hiyo,Khamis Heri Ayemba alijihusisha na biashara huko kwao Tanga na kuwa tajiri mkubwa. Wakati wa kudai uhuru, Ayemba alishirikiana na Peter Muhando na Mwalimu Kihere kuunda tawi la TANU huko Tanga. Tarehe 23 Oktoba, 1955 wanachama wa mwanzo wa TANU huko Tanga walikutana kuchagua uongozi wa chama hicho. Katika uchaguzi huo, Khamis Heri Ayemba alichaguliwa kuwa Mwenyekiti na Peter Muhando alichaguliwa kuwa katibu.
Kutokana na kusafiri sehemu mbalimbali duniani, Abeid Amani Karume alijifunza mengi ya kimaisha na kuona jinsi gani mataifa ya ulaya na mabepari walivyotumia hila na ujanja kuzinyonya nchi za Afrika. Katika safari zake za ubaharia alikumbana na matatizo kadhaa. Tatizo kubwa zaidi alokumbana nalo ni dhoruba kali sana iliyoikumba meli yao wakati wakitokea Australia kwenda Lorence Marques (Msumbiji).
Katika miaka ya 1930, timu za mpira wa miguu Zanzibar zilikabiliwa na mgawanyiko. Kutokana na mgawanyiko huo, ndipo hapo mwaka 1931 timu zote za New Kings, Vuga Boys, United Service na New Generation zilipoungana na kuunda umoja wa michezo wa waafrika uloitwa "African Sports Club". Timu hiyo ilikuwa na "A" na "B", ambapo Karume alikuwa timu "A" iliyokuwa ya kwanza mwaka huo kwenda Tanganyika kucheza mechi ya kirafiki.
Umoja huo haukwishia hapo kwani katika mwaka 1934 uliundwa umoja wa Waafrika (African Association). Umoja huo wa Waafrika ndiyo ulogeuka kutoka kwenye michezo na kuwa umoja wa kisiasa.
Katika mwaka 1938 bandarini Zanzibar palikuwa na vijana wa Kiafrika walounda umoja uliyoitwa “Motorboats Association”. Vijana hao walikuwa wakivusha abiria kutoka bandarini hadi melini kwa kutumia mashua, kazi ambayo iliwasaidia kupata pesa chache za kuendeshea maisha. Lakini baadaye walijitokeza wafanyabiashara wajanja wenye asili ya Asia wenye uwezo na kununua boti za mashine na kuvusha abiria. Wafanyabiashara hao, walitumia mbinu ya kuungana na waafrika katika biashara hiyo.
Baada ya muda mfupi wafanyabiashara hao wenye asili ya Asia waliunda chama chao kilichoitwa Syndicate. Taratibu wafanyabiashara hao waliwaingiza ndugu zao na wale waafrika waanzilishi waligeuzwa vibarua na kulipwa ujira mdogo sana. Abeid Karume aliwakusanya waafrika hao kudai haki zao na kufanikiwa kufanya mapatano na waasia hao. Wamiliki wa maboti hao, walikubali kuwalipa waafrika asimilia 40% ya mapato yote na wao walichukua asilimia 60% na kugharamia uendeshaji na matengenezo ya boti hizo.
Baada ya mafanikio hayo Abeid Amani Karume alipata sifa nyingi na mwaka 1939 alianzisha harakati za kuunda chama cha mabaharia Zanzibar ili kupigania haki za wafanyakazi hao. Kwa wakati huo ilikuwa vigumu sana kuwashawishi watu wasojua mipango ya vyama vya wafanyakazi. Hivyo basi mwishoni mwa mwaka huo wa 1939 baadhi ya wafanyakazi waloshauriwa kuanzisha umoja huo walikataa kushiriki katika umoja huo. Karume hakusita na juhudi zake za kuanzisha umoja huo. Mwaka huohuo wa 1939, alionana na mzungu aitwae Bwana Douglas Basil Berber aliyekuwa Inspekta wa polisi kuomba kibali cha kuanzisha chama cha mabaharia wa Unguja na Pemba.
Mzungu huyo alimshauri Abeid Karume awakusanye wale wote wanaotaka kuanzisha chama hicho na wajiunge kwa mujibu wa sheria za India. Zanzibar kwa wakati huo haikuwa na sheria kuhusu vyama vya wafanyakazi Waafrika.
Baada ya kuwashauri wenzake, Abeid Karume alipata watu sita walokubali kujiunga na jumuiya hiyo. Watu hao ni Bakari Jabu, Miraji Mselem, Juma Maalim, Ismail Mbarouk, Mbarouk Salim na Kitwana Suwedi. Chama cha Mabaharia wa Unguja na Pemba kilipata usajili tarehe 30 Ogosti, 1949 na Makao Makuu yake yalikuwa Kisima majongoo.
Sheria ya vyama vya wafanyakazi vya Zanzibar ilipitishwa mwaka 1931. Baadaye katika mwaka 1941, sheria hiyo ilifanyiwa mabadiliko na kuwa Sheria Nambari 3 ya vyama vya wafanyakazi.
Jumuiya za mwanzo za wafanyakazi kuanzishwa Zanzibar ni pamoja na Jumuiya ya Mabaharia, Jumuiya ya Wachukuzi na Umoja wa Watumishi wa Majumba ya Wazungu. Hadi kufika mwaka 1951 tayari chama cha mabaharia kilikuwa na wanachama 83. Tarehe 26 Oktoba 1959, Abeid Karume ambaye ni muasisi wa jumuiya ya mabaharia aliacha uongozi wa jumuiya hiyo na kujihusisha zaidi na siasa katika chama cha ASP ,lakini aliendelea kuwa mdhamini wa jumuiya hiyo. Kabla ya hapo katika mwaka 1942, Karume alikuwa katibu wa African Association na Rais wa Jumuiya hiyo hapo mwaka 1953. Baadaye nafasi hiyo ilishikiliwa na Bwana Herbert Barnabas.
Kwa mara ya kwanza Sheikh Abeid Karume alifunga ndoa na Bibi Pili binti Ahmed Ambari mwanzoni mwa miaka ya Arubaini. Mke wake wa pili ni Bibi Ashura binti Maisara. Baada ya kutengana na wake hao wawili, Sheikh Karume alifunga ndoa na Bibi Fatma binti Gulamhussein Ismail (Fatma Karume) katika mwaka 1944 mwishoni mwa mwezi wa Novemba, harusi ambayo ilifanyika huko Bumbwini Misufini.
Bibi Fatma Gulamhussein Ismail alizaliwa Bumbwini mwaka 1929 akiwa ni mtoto wa Bwana Gulamhussein Ismail na Bibi Mwanasha Mbwana Ramadhani. Wazazi wa Bibi Fatma Karume ni wazaliwa wa Bumbwini. Bi Fatma Karume alipata elimu ya msingi katika skuli ya Bumbwini na kuolewa mwaka mmoja baada ya kumaliza masomo hayo. Mara tu baada ya kufunga ndoa, Bibi Fatma Karume na Bwana Abeid Amani Karume walihamia mtaa wa Kisimamajongoo nyumba Nambari 18/22 mjini Unguja kwa Sheikh Karume. Nyumba nyengine mbili za Bwana Karume zilikuwa Gongoni na Michenzani.
Bi.Fatuma Karume alijifungua mtoto wa kwanza wa kike aliyeitwa Asha katika mwaka 1946, lakini mtoto huyo alifariki siku ya pili yake. Mtoto wa pili wa hayati Karume ni Amani Abeid Karume aliyezaliwa tarehe 1 Novemba, 1948. Mtoto wake wa tatu ni Ali Abeid Karume aliyezaliwa tarehe 24 Mei, 1950.
Mama yake mzazi Abeid Amani Karume, Bibi Amina binti Kadudu alifariki dunia 1963 na kuzikwa katika makaburi ya Michenzani. Wake wengine ambao waliolewa na Bwana Karume ni Bibi Nasra, Bibi Helemu na Bibi Fadya ambao kila mmoja alizaa nae mtoto mmoja wa kike.
Mbali ya kuanzisha chama cha mabaharia pia Abeid Amani Karume alikuwa muasisi wa Jumuiya ya Waafrika iliyoitwa African Dancing Club katika mwaka 1940. Jumuiya hiyo ilikuwa na lengo la kuwaunganisha pamoja vijana wa African Association.
Rais wa Jumuiya hiyo ya "African Dancing Club" alikuwa ni Bwana Pearcy Baraka, Abeid Karume alikuwa Katibu Mkuu na Mweka hazina ni Mtumwa Zaidi. Mbali ya kumiliki bendi ya muziki vilevile African Dancing Club ilinunua banda la zamani ambalo lilibomolewa na kujengwa makao makuu. Baadaye hapo tarehe 31 Januari, 1949 “African Dancing Club” ilibadilishwa jina na kuitwa “African Youth Union”.
Kuundwa kwa chama cha Zanzibar Nationalist Party (Hizbu) mapema katika miaka ya 50 na kutolewa kwa mapendekezo ya kufanyika uchaguzi mkuu wa kwanza wa Zanzibar katika mwaka 1957 yaliwafanya viongozi wa Jumuiya ya Waafrika African Association, na wale wa Shirazi Association waone umuhimu wa kushirikiana. Viongozi hao waliona ulazima wa kuungana kuwa kitu kimoja kupigania uhuru. Hivyo basi Jumuiya ya Shirazi Association ilimtuma Bwana Haji Khatibu aliyekuwa rafiki mkubwa wa Abeid Amani Karume apeleke shauri la kuunganishwa Jumuiya ya Waafrika na Jumuiya ya Washirazi.
Kabla ya kukutana, kila jumuiya ilifanya kikao cha faragha kujadili agenda ya mkutano. Shirazi Association walikubaliana kupendekeza jina la Abeid Karume kutoka African Association kuwa Rais wa chama kipya kitakachoundwa.
Nao African Association, walipanga kupendekeza jina la Sheikh Ameir Tajo kutoka Shirazi Association kuwa Rais wa chama kipya kitakachoundwa. Viongozi wa Jumuiya hizo walikubaliana kukutana kuanzia tarehe 1 hadi 5 Februari,1957. Mkutano ulifanyika kama ulivyopangwa hapo Mwembe Kisonge nyumbani kwa Abeid Amani Karume chini ya Mwenyekiti wake Muhidini Ali Omar. Kwa wakati huo, nyumba hiyo ya Abeid Karume alikuwa aliishi Hija Saleh na Haji Ali Mnoga.
Mkutano huo ulimalizika jioni ya tarehe 5 Februari, 1957 kwa viongozi hao kukubaliana kuunganisha Shirazi Association na African Association na kuunda chama kilichoitwa Afro - Shirazi Union.
Baadaye chama hicho kiliitwa Afro - Shirazi Party, jina ambalo lilitolewa na Ali Khamis kutoka Shirazi Association. Viongozi 18 wa African Association na Shirazi Association walikutana na kuunda Afro -Shirazi Party. Kumi ni kutoka African Association na Wanane kutoka Shirazi Association. Viongozi wa African Association walikuwa ni Abeid Amani Karume, Ibrahim Saadala, Abdalla Kassim Hanga, Bakari Jabu, Mtoro Rehani Kingo, Rajabu Swedi, Ali Juma Seif, Mtumwa Borafia, Saleh Juma na Saleh Mapete. Viongozi wa Shirazi Association ni Thabit Kombo Jecha, Muhidini Ali Omar, Ameir Tajo, Ali Khamis, Haji Khatibu, Mdungi Ussi, Ali Ameir na Othman Sharifu.
Katika mkutano huo pia alikuwepo mgeni mwalikwa Rais wa TANU, Mwalimu J.K. Nyerere na Katibu Mkuu wa chama cha TANU, Bwana Zubeir Mtemvu. Pia alihudhuria Bibi Maida Springer Kemp ambaye ni Mmarekani mweusi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi wa Viwanda wa Marekani American Federation of Labour Congress of Industrial Organization AFL - C 10. Bibi Springer alikuwa ziarani barani Afrika kuangalia harakati za ukombozi na alifuatana na Mwalimu Nyerere aliyepitia Zanzibar akielekea Tanga kuitangaza TANU.
Chama cha Afro - Shirazi Party kilimteuwa Abeid Amani Karume kuwa Rais, Mtoro Rehani Kingo kuwa Makamo na Thabit Kombo Jecha ni Katibu Mkuu. Wajumbe wa Halmashauri Kuu ni Ibrahim Saadala, Ali Khamis, Ameir Tajo, Mtumwa Borafia na Muhidini Ali Omar. Baadaye wajumbe wa Shirazi Association kutoka Pemba ambao ni Muhamed Shamte, Ali Sharif Mussa, Issa Sharif, Suleiman Ameir na Hassan Ali waliitwa na kufahamishwa juu ya kuunganishwa vyama hivyo.
Katika mwaka 1947 kuliundwa serikali za mitaa (Local Government) na Baraza la Manispaa (Township Council) lilianzishwa 1954. Abeid Karume alichaguliwa kuwa diwani (Councillor). Katika mwezi wa Juni 1957, Bwana Karume alikwenda nchini Ghana kuhudhuria sherehe za uhuru wa taifa hilo. Safari hiyo ilikuwa ni mwaliko wa kiongozi wa nchi hiyo, Bwana Kwameh Nkrumah kwa vyama vyote vya kupigania uhuru barani Afrika.
Abeid Amani Karume alipendekezwa na chama cha ASP kuwa mgombea wa kiti cha baraza la kutunga sheria wa jimbo la Ng'ambo, katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa Zanzibar wa 1957. Katika uchaguzi huo, Abeid Amani Karume alijiandikisha katika jimbo la Ng'ambo kituo Nambari 84 ambacho ni Old Shimoni School (Mao tse Tung) akiwa ni mfanyabiashara, mkaazi wa Kisima Majongoo nyumba Nambari 18/22. Kadi yake ya kupigia kura ilikuwa Nambari 5818. Karume alishinda kiti hicho kwa kura 3,328 dhidi ya wapinzani wake Ali bin Muhsin Barwan wa ZNP aliyepata kura 918 na Ibuni Saleh mgombea binafsi aliyepata kura 55.
Hapo tarehe 15 Januari, 1960 Abeid Karume alishtakiwa na mfanyabiashara aitwae Punja Kara Haji mkaazi wa Darajani mjini Unguja. Karume alishtakiwa kwa madai ya kuvunja mkataba wa kukodi bekari ya mfanyabiashara huyo.
Kesi hiyo Nambari 4 ya 1960 (Civil Case Number 4 of 1960) ilitayarishwa na wakili Dinshaw Karai kwa niaba ya Punja Kara Haji. Ilidaiwa mbele ya Jaji G.J. Horsfall wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kuwa hapo tarehe 17 Aprili,1958, Abeid Karume na Thabit Kombo waliingia mkataba na Punja Kara Haji wa kukodi bekari ya Mchangani, nyumba nambari 2759 mali ya Punja Kara Haji.
Mkataba huo ulieleza kuwa kodi hiyo itakuwa ni ya miaka mitatu kuanzia tarehe 1 Mei 1958 kwa malipo ya Shilingi 7,395/20. Abeid Karume alitakiwa alipe Shilingi 550/- kila mwezi. Waraka wa makubaliano hayo ulotayarishwa na Wakili Dinshaw Karai ulitiwa saini hapo tarehe 18 Novemba, 1959 na Punja Kara Haji kwa niaba yake na Abeid Karume kwa niaba yake na kwa niaba ya Thabit Kombo. Mkataba huo ulishuhudiwa na mawakili Dinshaw Karai na Hemed Said.
Akiwasilisha madai dhidi ya Karume hapo tarehe 27 Januari, 1960 Punja Kara Haji alidai kuwa tarehe 16 Novemba, 1959 Abeid Karume alifika nyumbani kwake na kumueleza kuwa yeye na Thabit Kombo wanataka kuiacha bekari hiyo kwa vile ilikuwa inawatia hasara.
Punja Kara Haji alieleza mahakama hiyo kuwa, baada ya kupata kauli hiyo ya Abeid Karume walifikia makubaliano na mlalamikiwa. Abeid Karume alitakiwa alipe Shilingi 7,395/20 kama ilivyo katika mkataba wao wa tarehe 17 Aprili, 1958. Pia Karume alitakiwa akabidhi jengo la bekari hiyo kwa mwenyewe hapo tarehe 31 Disemba, 1959. Akiendelea kutoa ushahidi wake Punja Kara Haji alidai mahakamani kuwa yeye na Karume walikubaliana fedha hizo Shilingi 7,395/20 zilipwe kwa awamu kwa udhibitisho wa maandishi.
Awamu ya kwanza ya Shilingi 2,000/- ziwe zimelipwa ifikapo Disemba, 1959. Fedha zilizobaki Shilingi 5,395/20 zilipwe kidogo kidogo kwa wastani wa Shilingi 500/- kila mwezi kuanzia tarehe 1 Januari, 1960. Fedha hizo zilitakiwa ziendelee kulipwa kwa utaratibu huo kila siku ya mwanzo ya kila mwezi. Punja Kara alidai kuwa Abeid Karume alishindwa kulipa Shilingi 2,000/- hapo tarehe 1 Disemba,1959 na hakulipa Shilingi 500/-ilipofika tarehe 1 Januari,1960 kama walivyokubaliana. Kutokana na madai yake hayo, Punja Kara Haji alidai mahakamani alipwe na Abeid Karume Shilingi 7,395/20, asilimia 9% ya riba ya mwaka kuanzia tarehe ya hukumu na alipwe gharama za kesi hiyo.


Waraka ulomtaka Abeid Karume kufika mahakamani tarehe 8 Februari, 1960 saa 3.00 asubuhi ulitiwa saini na Mrajisi wa mahakama Hussein A. Rahim tarehe 27 Januari, 1960.
Akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo Abeid Karume aliambia mahakama hiyo kuwa hapo tarehe 20 Januari, 1960 alimlipa Punja Kara Haji Shilingi 1,000/-. Pia walikubaliana kuwa deni lililobaki lilipwe kwa wastani wa Shilingi 500/- kila mwezi. Karume alieleza kuwa licha ya makubaliano hayo, mlalamikaji alifungua mashtaka hapo tarehe 27 Januari,1960 bila kutoa stakabadhi ya malipo ya Shilingi 1000/- alizopewa. Baada ya kupokea waraka wa kumtaka afike mahakamani kujibu kesi hiyo,Karume alikwenda kwa Punja Kara Haji ambaye alimweleza Karume kuwa mashtaka dhidi yake yalifunguliwa na wakili wake aitwae Dinshaw Karai baada ya kutofahamiana na mteja wake.
Punja alimuhakikishia Abeid Karume kuwa atamwambia wakili huyo aifute kesi hiyo mara moja. Abeid Karume alieleza mahakama hiyo kuwa, kwa vile aliyaamini maneno ya Punja hakuona ulazima wa kufika mahakamani kujibu kesi hiyo. Inaelekea mlalamikaji (Punja Kara Haji) alitumia fursa ya kutofika Karume mahakamani na kupata upendeleo wa kisheria kwa vile kesi hiyo ilisikilizwa upande wa mlalamikaji pekee. Hivyo moja kwa moja Punja Kara alidanganya mahakama kuwa Abeid Karume alilipa Shilingi Elfu moja baada ya kufunguliwa mashtaka. Karume alieleza mahakama hiyo kuwa vile vile hapo tarehe 7 Machi, 1960 alitoa mahakamani amana ya Shilingi 2,000/- taslimu na kupatiwa stakabadhi ya malipo yenye Nambari 153/60. Lakini licha ya ukweli huo mlalamikaji aliomba mahakama hapo tarehe 11 Machi, 1960 itoe uwamuzi wa kesi hiyo. Hata hivyo Abeid Karume alishinda kesi hiyo na madai ya mlalamikaji yalitupiliwa mbali.
Katika mwezi wa Oktoba 1960, Sheikh Abeid Amani Karume alihudhuria mkutano mkuu wa chama cha Malawi Congress Party huko Nkhota Kota katika Wilaya ya kati ya Nyasaland (Malawi) akiwakilisha chama cha Afro- Shirazi. Katika mkutano huo wanasiasa wanane wa mwisho wa Malawi walokuwa kizuizini waliachiliwa huru. Wanasiasa hao walitiwa ndani kwa kupinga mpango wa wakoloni wa kiingereza wa kuanzisha Shirikisho la Rhodesia (Zimbabwe) na Nyasaland (Malawi). Baada ya kuachiliwa huru, walikabidhiwa kwa kiongozi wa chama cha Malawi Congress Party, Dr. Kamuzu Banda. Aliyewakabidhi wanasiasa hao kwa Dr.Banda ni Gavana wa mwisho wa Uingereza katika koloni la Nyasaland. Msamaha huo ulitolewa muda mfupi kabla ya nchi hiyo kupata uhuru.
Wanasiasa waloachiliwa ni pamoja na Masauko Chipembere, Matupi Mkandawire, Chimtambi na wengineo. Mkutano huo wa chama cha Malawi Congress Party ulihudhuriwa na maelfu ya wananchi wa Malawi. Viongozi kadhaa wa kisiasa wa Jumuiya ya PAFMECA (Pan African Freedom Movement for East and Central Africa) walialikwa ambapo viongozi wa ngazi ya juu wa vyama hivyo walihudhuria mkutano huo.
Mbali ya Abeid Karume na ujumbe wake wa chama cha Afro -Shirazi kutoka Zanzibar, pia walihudhuria Marton Malianga wa chama cha Southern Rhodesia African National Congress cha Rhodesia (Zimbabwe) kilichoongozwa na Joshua Nkhomo. Wengine ni Namilando Mundia wa chama cha Zambia National Congress kilichongozwa na Kenneth Kaunda, Sheikh Amri Abeid Kaluta na Austin Shaba wa chama cha Tanganyika African National Union, TANU cha Tanganyika.
Vilevile alihudhuria Abdulrahman Babu na ujumbe wake wa chama cha ZNP cha Zanzibar. Kwa lengo la kuimarisha umoja na ushirikiano kati ya chama cha ASP na chama cha Malawi Congress Party cha Malawi, Abeid Karume aliwaalika kuitembelea Zanzibar baadhi ya viongozi wa chama hicho cha Malawi mapema mwaka 1965. Viongozi walotembelea Zanzibar kutoka Malawi ni Orton Chingolo Chirwa, Yatuta Chisiza, Willie Chokani, Augustine Bwanausi na Kanyama Chiume.
Abeid Karume alichaguliwa tena kuwa mjumbe wa baraza la kutunga sheria katika uchaguzi wa pili wa Januari, 1961, katika jimbo la Jang'ombe kwa tiketi ya ASP.
Mara tu baada ya kumalizika uchaguzi huo wa 1961 ulokuwa na utatanishi Abeid Amani Karume alichaguliwa kuwa Waziri wa Afya na Mambo ya Kienyeji katika serikali ya pamoja ya miezi sita. Uchaguzi Mkuu wa tatu wa Zanzibar ulifanyika tarehe 1 Juni, 1963.
Karume alichaguliwa tena kuwa Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria katika jimbo la Kwahani na Jang'ombe. Akiwa Waziri wa Afya, Karume alishughulikia Afya, Ajira, Ujenzi wa Nyumba, Serikali za Mitaa na Serikali za Wilaya.
Baada ya kuundwa serikali ya Waziri Mkuu Muhammed Shamte kufuatia uchaguzi wa 1963, Abeid Amani Karume aliteuliwa kuwa kiongozi wa upinzani katika baraza la kutunga sheria.
Wakati wa matayarisho ya Mapinduzi ya 1964 Abeid Karume alikuwa mwenyekiti wa kamati ya watu kumi na nne walotayarisha Mapinduzi hayo kwa siri. Akiwa na umri wa miaka 59, Karume aliongoza Mapinduzi ya 1964 na alitangazwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na vilevile kubaki na wadhifa wake wa Rais wa Afro- Shirazi Party.
Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ziliungana hapo tarehe 26 Aprili,1964 na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Abeid Amani Karume alichaguliwa kuwa Makamo wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapo tarehe 27Aprili,1964.
Akiwa Makamo wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Abeid Amani Karume aliongoza ujumbe wa watu kumi na tisa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutembelea mikoa ya Musoma, Mwanza na Bukoba kuanzia tarehe 5 -15 Septemba,1965. Lengo la ziara hiyo ni kuonana na wananchi wa mikoa hiyo na kuwahamasisha kuhusu uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi wa Septemba, 1965.
Mheshimiwa Karume aliteuliwa kuwa mbunge wa bunge la Tanzania kupitia viti maalum vya kuteuliwa na Rais wa Tanzania. Karume alikuwa ni mmoja kati ya wabunge 23 wa kuteuliwa kutoka Zanzibar kama ilivyokuwa katiba ya wakati huo. Aliapishwa rasmi kuwa Makamo wa kwanza wa Rais wa Tanzania katika ukumbi wa Arnatoghly mjini Dar es Salaam hapo tarehe 30 Septemba, 1965.
Katika mwezi wa Aprili 1967, Mzee Karume akifuatana na Rais wa Tanzania Mwalimu Nyerere na wajumbe kadhaa wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na serikali ya Tanzania walikwenda nchini Misri kuhudhuria mkutano wa siku nne wa nchi tano za Afrika. Mkutano huo, uliandaliwa na Rais Jamal Abdul Nasser wa Misri. Katika ziara hiyo Mwalimu Nyerere na Mheshimiwa Abeid Karume walitunukiwa uraia wa jiji la Alexandria. Baadhi ya viongozi mashuhuri walotembelea Zanzibar wakati wa uhai wa Abeid Amani Karume ni pamoja na Waziri Mkuu wa Hungary, Bwana Gyula Ka'llai, Makamo wa Rais wa Zambia Reuben Kamanga na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Korea Bwana Kang Ryang. Wengine ni Rais Jamal Abdel Nasser wa Misri, Rais Modibo Keite wa Mali , Rais Makarios wa Cyprus na Rais Tito wa Yugoslavia.
Wengine ni Rais wa Hungary Bwana Pal Losonczi, Waziri Mkuu wa Guyana Bwana Burham na Waziri Mkuu wa Swaziland, Prince Makhosini Dlamini.
Mheshimiwa Abeid Amani Karume, kiongozi wa Mapinduzi ya Zanzibar, na mmoja wa waasisi wa Chama cha Afro-Shirazi na Makamo wa kwanza wa Rais wa Tanzania aliuwawa akiwa na umri wa miaka 67. Mauwaji hayo yalitokea siku ya Ijumaa ya tarehe 4 Aprili,1972 saa 12.05 za jioni katika jengo la Makao Makuu ya ASP Kisiwandui.
Mara tu baada ya mauaji hayo hali ya hatari ilitangazwa na msako mkali wa wahalifu ulianza nchi nzima. Watuhumiwa kadhaa wakiwemo raia na maofisa wa vikosi vya ulinzi na usalama walitiwa mbaroni, ambapo mtuhumiwa mkuu akiwa ni Abdulrahman Muhammed Babu aliyekamatwa huko Dar es Salaam.
Maziko ya Sheikh Abeid Amani Karume yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kutoka nchi mbalimbali duniani. Wengi wa wageni hao walianza kumiminika Zanzibar kuanzia saa tatu za asubuhi na kwenda kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu katika jumba la serikali Forodhani. Baada ya kutolewa heshima za mwisho,jeneza lilitolewa nje na kikosi cha wanajeshi ili kusaliwa katika uwanja wa Ikulu.
Baada ya marehemu kusaliwa hapo Ikulu, jeneza lilichukuliwa hadi Makao Makuu ya ASP Kisiwandui, kupitia barabara ya hospitali ya Mnazi Mmoja, Makumbusho, Mkunazini na kupindisha kuelekea barabara ya Michenzani hadi Makao Makuu ya Afro-Shirazi.
Hitma ya Abeid Karume ilisomwa katika ukumbi wa klabu ya wananchi tarehe 29 Julai, 1972 wakati wa jioni na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi kadhaa. Kwa vile miongoni mwa malengo ya Mapinduzi ya 1964 yalikuwa ni pamoja na kuwapatia makazi bora wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba, Mzee Abeid Amani Karume aliweka jiwe la msingi la jumba la kwanza la fleti 132 hapo Michenzani tarehe 4 Mei, 1970.
Baadhi ya taasisi ambazo zimepewa jina la Karume ni Chuo cha Ufundi cha Mbweni Zanzibar, Kiwanja cha Ndege cha Chake Chake Pemba, Viwanja vya mpira vya Musoma na Dar es Salaam na Kituo cha Televisheni ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa vile miongoni mwa malengo ya Mapinduzi ya 1964 yalikuwa ni pamoja na kuwapatia makazi bora wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba, Mzee Abeid Amani Karume aliweka jiwe la msingi la jumba la kwanza la fleti 132 hapo Michenzani tarehe 4 Mei, 1970. Jumba hilo la kwanza liligharimu jumla ya Shilingi milioni 4,752,000/-. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikusudia kujenga fleti 7000 katika mji wa Zanzibar na kutoa nafasi za makazi kwa wananchi 30 Elfu.
Kufuatia kuuwawa kwa Sheikh Abeid Amani Karume hapo tarehe 7 Aprili,1972 watu 81 wakiwemo wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, raia na polisi walishtakiwa kwa makosa ya uhaini katika mahkama ya wananchi ya Zanzibar. Kesi hiyo ilianza kusikilizwa rasmi siku ya Jumatatu tarehe 14 Mei, 1973.
Kesi hiyo Nambari 292 ya 1973 iliendeshwa na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Bwana Wolfgang Dourado akisaidiwa na Ussi Khamis Haji. Katika kesi hiyo mshtakiwa mkuu alitajwa kuwa ni Abdulrahman Muhammed Babu. Washtakiwa tisa walikiri makosa yao, washtakiwa 54 walikana makosa ambapo 18 akiwemo kiongozi wa njama hizo za uhaini na kutaka kuipindua serikali halali ya ASP, Abdulrahman Muhammed Babu walishtakiwa wakiwa hawapo kortini.
Mwanasheria Dourado aliiambia mahakama hiyo kwamba mkutano wa mwanzo wa siri ulifanywa Dar es Salaam wakati wa sherehe za saba saba za mwaka 1968. Babu alifanya karamu kubwa ya chakula cha mchana nyumbani kwake, ambapo wasitakiwa kadhaa kutoka Zanzibar na Dar es Salaam walihudhuria karamu hiyo. Siku hiyo Babu ndiye aliyetoa shauri kuwa, kazi za wanachama wa Umma Party zipangwe vyengine na akatoa taarifa ya dhamira ya kutaka kuipindua serikali ya ASP. Baramia aliambiwa awe ni kiungo na mpelekaji habari baina ya Zanzibar na Dar es Salaam.
Kesi ya uhaini ilimalizika tarehe 15 Mei, 1974, ambapo washtakiwa 43 walihukumiwa adhabu ya kifo. Washtakiwa 11 walihukumiwa kwenda Chuo cha Mafunzo miaka 15 kila mmoja na wanne walipewa adhabu ya kifungo cha miaka 4 kila mmoja.
Washtakiwa 16 waliachiliwa kwa kukosekana ushahidi na wengine 6 walisamehewa kwa kukosa kesi ya kujibu. Mshtakiwa mmoja alifariki akiwa kizuizini kabla ya kumalizika kesi hiyo. Ingawa washitakiwa 43 walihukumiwa adhabu ya kifo, wakiwemo tisa walokiri kupanga njama za kumuua Sheikh Karume wote waliachiliwa huru siku ya Jumamosi ya tarehe 19 Mei, 1974.
Kwa vyovyote vile, jina la Abeid Karume halitosahaulika katika historia ya ukombozi wa Zanzibar. Haiwezekani kuandika au kuzungumzia ukombozi na mafanikio ya maendeleo ya Zanzibar bila kujata jina la Abeid Karume.

Comments

Popular posts from this blog

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

AMANI YETU TUILINDE NAIBU WAZIRI CHANDE AZUNGUMZA KATIKA IJITIMAI JIJINI DODOMA

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.