VIWANDA VYA SAMAKI MWANZA NOMAA
WAZIRI
wa Wizara ya Mifugo, Kilimo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba amefanya ziara ya
kushitukiza jijini Mwanza na kubaini madudu baadhi viwanda vya samaki vilivyopo na kubaini
kimoja kimekuwa sugu kwa kuchakata samaki wachanga pia uwepo vituo bubu vya
samaki, upotevu wa wa mapato ya mabondo ya samaki.
Dk
Tizeba alifanya ziara hiyo hivi karibuni kwa kutembelea Viwanda vya kuchakata na
kuuza minofu ya samaki nje ya nchi ili kuangalia hali halisi ya mazao ya samaki
yanayofikishwa katika viwanda vya Omega Fish, Tanzania Fish Processor (TFP), Victoria
Pech zamani ikijulikana Mwanza Fish, Nile Perch, Tanpech Fish Ltd na baadhi ya
sehemu za Kirumba, Mkuyuni na Nyakato zinazotumika kupoza samaki kwenye majokofu.
Waziri
alitoa agizo kwa Afisa Mfawidhi wa Uthibiti wa Ubora wa Samaki na Mazao yake
Kanda ya Ziwa Victoria, Steven Lukanga kusimamia kufanya ukaguzi wa kila wakati
na kuhakikisha samaki waliochini ya sentimita 50 na waliozaidi ya sentimita 85 kilo
207 hawaruhusiwi kuingizwa na kuchakatwa katika viwanda hivyo kama alivyokuta
katika kiwanda cha Omega Fish Ltd kilichopo eneo la Ilemela Manispaa.
“Haiwezekani
una wakaguzi wa kuangalia uthibiti na ubora wa samaki lakini unakuta kiwanda
kinachakata samaki ambao hawaruhusiwi kwa mujibu wa taratibu na sheria za uvuvi
endelevu kama kiwanda hiki cha Omega Fish hivyo ni lazima hatua za haraka
zichukuliwe kwa maofisa wanaofanya ukaguzi katika viwanda hivi kwa kuwa
wameshindwa kutimiza wajibu wao, ”Alisema Waziri.
Aidha
aliongeza kuwa suala hilo la hatua za kuchukuliwa dhidi ya kiwanda hicho
atamuagiza Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi wa Wizara hiyo kuchukua hatua za haraka
ikiwemo kukifungia mara moja kwa mwezi mmoja kuchakata samaki na kuuza minofu
ya samaki nje ya nchi hadi hapo serikali itakapojilidhisha kuwa hakitaendelea
kufanya uchakataji wa samaki wachanga wasioruhusiwa kuingia viwandani.
Dk
Tizeba aliagiza maafisa wa ukaguzi wa samaki na uvuvi Mkoa kufanya ukaguzi kila
siku ili kudhibiti wafanyabiashara wanaoshirikiana na wamiliki wa vituo vya
makontena ya kupoza samaki wasiweze kupoza samaki wachanga (madegele) ambao amewakuta
kwenye makontena yao na kutaka wachukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kuyafungia
kufanya kazi hiyo kutokana na kuhujumu rasilimali hiyo.
“Utaratibu
upo wazi tumeagiza samaki waliochini ya sentimita 50 na waliozidi sentimita 85
ni marufuku kuingizwa viwandani pamoja na kwenye hivi viwanda bubu (vituo bubu)
vya kupoza samaki kabla ya kusafirishwa
kwenye masoko, lakini pia wakiendelea hatua kali za kisheria zichukuliwe haraka
na bila kufumbia macho ili kusaidia kulinda uvuvi endelevu ndani ya ziwa Victoria
,”alisisitiza.
Waziri
pia alimuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza (RAS), Clodwig Mteve kuhakikisha
anafuatilia taarifa za kuwepo kwa maafisa uvuvi wawili wa kitengo cha Ukaguzi
wa samaki cha Nyegezi kudaiwa kupigania rushwa baada ya kukamata samaki wadogo
(madegele) katika Meli ya Mv Bigil eneo la Kirumba na kudaiwa kufikishwa kituo cha
Polisi Kirumba Wilaya ya Ilemela ili kuwachukulia hatua za kimaadili.
“RAS
nikuombe ufikishe taarifa ya agizo langu kwa wakurugenzi wa Manispaa ya Ilemela
na Jiji la Mwanza ili kuwaondoa maafisa uvuvi wa Halmashauri hizo katika
majukumu yao ikiwemo uhamisho kufatia kuwa chanzo cha kushindwa kudhibiti uvuvi
haramu pamoja na kuruhusu samaki wadogo kufikishwa katika masoko bila
kuwakamata wafanyabiashara wanaofanya biashara za samaki wachanga (madegele),”alisisitiza
Dk Tizeba.
Waziri
pia aliwataka wamiliki wa viwanda kutoyauza mabondo ya samaki kwa njia za panya
ikiwemo kwa wafanyabiashara wa mabondo wakiwemo wachina kwa kuwa wamekuwa
wakikosesha serikali mapato na ushuru wake yanayotoka katika mazao ya samaki na
kutaka kufuata utaratibu uliopo wakati wakisubilia taarifa ya Tume iliyoundwa
na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ili kutoa mrejesho mzuri wa biashara hiyo.
Naye
Afisa Uvuvi Mkoa wa Mwanza, Lameck Mongo alisema kwamba ofisi yake itaendelelea
kufunga maeneo ya mazalia ya samaki ndani ziwa Victoria hasa kwenye maji ya
kina kifupi ili samaki waweze kuzaliana ambapo alifafanua kuwa kuanzia Januari
hadi Juni kila mwaka hufungwa na kuanzia mwezi Julai hadi Desemba huruhusiwa
kuvuliwa samaki wasiochini ya sentimita 50 na zaidi ya sentimita 85.
Mongo
alikiri kuwepo baadhi ya wavuvi wasiowaaminifu wanaoendelea kufanya uvuvi
haramu na kushirikiana na wafanyabiashara ambao ni walanguzi kuchukua samaki
hizo kwa lengo la kupeleka katika viwanda vya kuchakata samaki na sehemu za
makontena ya kupozea samaki, hivyo kikosi cha doria cha maafisa uvuvi Mkoa na
Kanda ya Ziwa wataendelea na jukumu la kuwasaka na kuwakamata ikiwemo
kuwafikisha kwenye sheria.
MWISHO.
Comments
Post a Comment