SIKU 100 ZA AWAMU YA TANO BALOZI SEFUE ANENA



Picha mbalimbali zikimuonesha Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akitoa taarifa ya siku 100 za kwanza za Serikali ya awamu ya tano.
 













TAARIFA YA SIKU 100 ZA KWANZA ZA SERIKALI YA
AWAMU YA TANO ILIYOTOLEWA NA
BALOZI OMBENI Y. SEFUE, KATIBU MKUU KIONGOZI,
IKULU, TAREHE 12 FEBRUARI, 2016
__________________________


Utangulizi

Serikali ya awamu ya Tano imetimiza siku 100 tangu iingie madarakani tarehe 5 Novemba, 2015. Japo siku 100 ni chache sana kufanya tathmini ya kina, zinatosha kuonesha muelekeo wa serikali na kupata kionjo cha uthabiti wa dhamira yake ya kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.

            Kumekuwa na shauku kubwa ya wananchi kujua kilichofanywa na Serikali hii katika siku zake 100 za mwanzo. Ni shauku ya haki ambayo sisi katika Serikali hii lazima tujaribu tuwezavyo kuikidhi. Ndio maana kuanzia juzi Mawaziri mbalimbali wanazungumzia mafanikio katika hizo siku 100, kila mmoja akienda kwa undani kwenye sekta yake. Nawaomba wananchi wafuatilie kwa karibu yale ambayo Mawaziri hawa wanayatolea taarifa kwenu ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji wao kwa wananchi.

            Mimi pia, kwa nafasi yangu ya Katibu Mkuu Kiongozi, ambaye ni Katibu wa Baraza la Mawaziri na Mkuu wa Utumishi wa Umma, nimepokea maswali mengi ya waandishi wa habari na wananchi wengine kuhusu siku 100 za kwanza za uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Maeneo yanayohusu sekta mbalimbali yatazungumzwa na Mawaziri wanaohusika. Lakini nimeona baadhi ya maswali yanaweza kujibiwa tu na ofisi hii, yaani Ikulu.

            Nimeyaweka maswali hayo katika makundi matano na nitayazungumzia kwa ujumla:

·         Yapo maswali yanayohusu uongozi wa Rais wetu;

·         Yapo maswali yanayohusu sifa binafsi za Rais wetu;

·         Yapo maswali yanayohusu utendaji wake;

·         Yapo maswali yanayohusu mahusiano yake na sekta binafsi kwenye utawala wake; na

·         Yapo maswali yanayohusu mwelekeo wake kwenye mambo ya nje na diplomasia ya Tanzania.


Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano Ukoje?

            Wahenga walisema, “Nyota njema huonekana asubuhi.” Naam! Katika siku 100 za kwanza, Rais Magufuli amethibitisha kwa uwazi zaidi kuwa yeye ni kiongozi bora na wa kupigiwa mfano. Taarifa tunazoletewa na wananchi ni kuwa kwa kauli, matendo na dhamira yake, wananchi wengi wamemwelewa, wamemkubali na wanamwamini. Katika hizi siku 100, Rais amewathibitishia Watanzania kuwa yeye ni kiongozi, mwenye sifa muhimu za uongozi. Sifa hizo ni pamoja na:

·         Kiongozi bora lazima awe na dira, maono na malengo kuhusu anakotaka Taifa liende. Katika siku 100 za kwanza Rais Magufuli amedhihirisha kuwa ana sifa hiyo.

·         Lakini dira bila mkakati ni ndoto. Kiongozi bora lazima awe na mikakati ya kutekeleza dira na maono yake, pamoja na kufikia malengo katika vipindi tofauti. Katika siku 100 za kwanza Rais Magufuli amedhihirisha anayo sifa hiyo.

·         Kiongozi bora lazima aheshimike na awe na mvuto wa kuwafanya wananchi wamwamini, na kumfuata. Katika siku 100 za kwanza za utawala wake, Rais amewafanya hata ambao hawakumpigia kura, wamwamini, wamwombee na kumfuata.

·         Kiongozi bora anagawa majukumu, na haogopi kufanya hivyo, lakini anafuatilia. Katika siku 100 za kwanza Rais Magufuli amethibitisha kuwa anayo sifa hiyo.

·         Kiongozi bora anajua na haogopi kuweka vipaumbele na mpangilio wake wa utekelezaji na kuvisimamia. Katika hizi siku 100 Rais Magufuli amethibitisha anayo sifa hiyo muhimu ya uongozi.

·         Kiongozi bora haogopi kufanya maamuzi magumu. Hakuna mwenye shaka kuwa katika hizi siku 100, Rais wetu amedhihirisha kwa kauli na kwa vitendo kuwa, anapotetea maslahi ya Taifa na wananchi, haogopi kufanya na kusimamia maamuzi magumu.

Rais ana Maono na Mikakati pevu ya kutimiza maono yake

Kama nilivyosema, sifa mojawapo ya kiongozi bora, ni kuwa na maono pevu na mikakati madhubuti inayotekelezeka, ya kutimiza maono hayo kwa faida ya wananchi. Tumeona haya kwa Rais Magufuli na Serikali yake katika siku 100 za kwanza. Tangu wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, Rais Magufuli aliweka bayana maono ya Tanzania anayotaka kuijenga, na nini kifanyike ili kutimiza azma hiyo. Maono na shauku yake, kama ilivyo kwetu sote, ni kujenga Tanzania mpya yenye uhuru, haki, neema na fursa mbalimbali kwa wananchi wote; Tanzania yenye amani na utulivu; Tanzania yenye uchumi imara unaotegemea viwanda; Tanzania ambayo kila mtu ananufaika na rasilimali tulizonazo; na Tanzania isiyo na rushwa, ufisadi na dhuluma.


Rais anabadili utendaji wa Serikali

Mtakumbuka, kuwa Serikali ya Awamu ya Tano, iliahidi kuendeleza misingi imara ya kiuchumi, kisiasa na kijamii iliyojengwa na awamu zilizotangulia. Pia iliahidi kuwa, katika juhudi zake za kuinua uchumi na kuondoa kero zinazowakabili wananchi, itazingatia vipaumbele vifuatavyo katika kubadili na kuboresha utendaji Serikalini.

1.      Kupunguza urasimu ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa maamuzi na miradi ya Serikali;

2.      Kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji wenye maslahi kwa Taifa, hususan katika sekta ya viwanda;

3.      Kubana matumizi, kwa kupunguza yale ambayo kwa kuzingatia hali yetu ya uchumi kwa sasa, yanaweza kuepukika;

4.      Kuimarisha huduma za jamii, hasa katika maeneo yenye kero zaidi kwa wananchi;

5.      Kuhimiza na kusimamia utii wa sheria, kurejesha nidhamu ya Serikali, na uzingatiwaji wa maadili kwa viongozi wa umma na watumishi wote wa Serikali, sekta binafsi na watu wote kwa ujumla;

6.      Kudumisha ulinzi na usalama, na kuendeleza mahusiano mazuri na yenye tija baina ya Tanzania na nchi za nje, mashirika na taasisi za kikanda na kimataifa, pamoja na wabia wengine wa maendeleo.




Amiri Jeshi Mkuu
            Katika siku hizi 100 za kwanza, Rais ametekeleza majukumu yake ya Amiri Jeshi Mkuu kwa wepesi na uhodari kama vile samaki kwenye maji. Amekuwa karibu na Jeshi na viongozi wake. Amekagua vifaa vya Jeshi na mazoezi ya kijeshi. Ameteua viongozi wa Jeshi, na kutoa kamisheni kwa Maafisa Wapya. Ametoa maelekezo mahususi ya kuimarisha Jeshi na utendaji wake.

Sifa Binafsi za Rais Magufuli

Kundi la pili la maswali tuliyoletewa linahusu sifa binafsi za Rais Magufuli ambazo zimedhihirika katika hizi siku 100 za uongozi wake. Nitataja chache.

·         Mkweli

Katika hizi siku 100, Rais wetu amewadhihirishia Watanzania kuwa ni mkweli, anayechukia ulaghai na unafiki. Anaposema, “Msema kweli ni mpenzi wa Mungu” anamaanisha hivyo kwa dhati. Wapo watu wanaofikiri kuwa siasa ni ujanja na ulaghai. Rais wetu amethibitisha kuwa yeye si mwanasiasa wa aina hiyo. Hakuna tofauti kati ya alivyokuwa akiwa mgombea na alivyojidhihirisha katika siku 100 za kwanza za Urais. Watanzania wana kila sababu ya kufurahi kuwa alivyojinadi ndivyo anavyotawala.

·         Anatekeleza ahadi

Katika siku 100 Rais wetu amethibitisha kuwa anaheshimu ahadi zake na anazitekeleza kadri iwezekanavyo. Tayari ipo mifano kadhaa. Aliahidi kupunguza ukubwa wa Serikali, na amefanya hivyo kwa kupunguza idadi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri kutoka 55 hadi 35. Amepunguza pia idadi ya Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu kutoka 56 hadi 50. Aliahidi elimu ya msingi (mpaka kidato cha nne) bila malipo na ametekeleza. Alipoiahidi Mahakama kuwa atawapa fedha zao zote za maendeleo, Sh.12.3 bilioni, ndani ya siku tano, ametekeleza hata kabla siku hizo hazijaisha. Na mifano mingine ipo ya anavyotekeleza ahadi zake. Kwa ufupi, aliahidi kuwa hatawaangusha Watanzania na kweli hajawaangusha katika hizi siku 100.

·         Anajali kwa Dhati Shida na Kero za Wananchi.

Katika siku 100 za kwanza, Rais ameonesha namna anavyoumizwa na kufadhaishwa na kero zinazowakabili wananchi. Pia amethibitisha dhamira yake ya dhati ya kuzipatia ufumbuzi, hususan katika upatikanaji wa huduma za jamii ikiwamo huduma za afya, elimu na maji.

Kasi ya kutatua kero za wananchi imeongezeka sana. Ndani ya siku hizi 100, tuna mifano mingi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kuondoa kero, zingine zikiwa za muda mrefu sana. Mmemsikia Waziri wa Ardhi akizungumzia utatuzi wa mgogoro wa muda mrefu wa shamba la Kapunga katika Wilaya ya Mbarali (Mbeya), ambapo hekta 1,870 tayari zimerejeshwa kwa wananchi. Aidha, mmesikia urejeshwaji kwenye miliki ya serikali, kiwanda cha chai cha Mponde, kilichopo mkoani Tanga, ambacho kilikuwa kero kwa wananchi kwa muda mrefu. Kila Waziri ataeleza mifano mingine mingi, kwenye kila sekta, kuonesha kasi mpya ya kumaliza kero na shida za wananchi.

Usimamizi wa Nidhamu bila Uwoga

Sifa nyingine ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano iliyodhihirika katika kipindi cha siku 100 za kwanza ni uwezo wa kusimamia nidhamu bila upendeleo ama uwoga. Orodha ni kubwa ya viongozi na watumishi waliochukuliwa hatua mbalimbali za kisheria na kinidhamu kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Siku 100 za kwanza za Serikali ya Awamu ya Tano zimepambanua wazi ni aina gani ya uongozi na utumishi wa umma unatakiwa katika serikali hii. Imedhihirika wazi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haitamvumilia kiongozi au mtumishi yeyote wa umma atakayeshindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo, au kufanya maamuzi yanayolenga kumnufaisha yeye binafsi. Na tayari mrejesho tunaoupata kutoka kwa wananchi ni kuwa nidhamu kwenye utumishi wa Umma imeongezeka na wananchi wanahudumiwa kwa haraka zaidi, na kwa heshima zaidi.

Tumedhamiria kurejesha nidhamu ya kazi na kutokomeza utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea na kujinufaisha. Katika tafsiri pana zaidi, hatua hizo zinalenga kukuza utamaduni wa uadilifu, uwajibikaji na kufanya kazi kwa uhodari, bidii na ufanisi mkubwa, kunakoendana na kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”. Na ndio maana Rais aliwalisha kiapo cha Uadilifu Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wote aliowateua. Kamwe Watumishi wa Umma wasisahau kuwa wao ni watumishi, sio mabwana, wa wananchi. Wawatumikie kwa ufanisi, kwa uaminifu na kwa heshima.

Ukaribu na Wananchi na Uungwaji Mkono

Siku 100 za kwanza za Utawala wa Awamu ya Tano zimethibitisha ukweli wa usemi usemao “imani, hujenga imani.” Ndani ya siku hizi 100, Serikali imefarijika kuona namna wananchi wengi, bila kujali itikadi zao, walivyoonesha imani kubwa kwa Mheshimiwa Rais na Serikali yake na jinsi wanavyoiunga mkono. Kwa upande mwingine tumeshuhudia jinsi Mheshimiwa Rais na serikali yake ilivyo karibu na wananchi na namna wananchi wanavyozidi kumfurahia Rais wao.

Na wanafanya hivyo kwa vile wamemkubali kama kiongozi wao, na wanamwamini. Hivyo moja ya mafanikio makubwa katika hizi siku 100 ni vile ambavyo Rais ameweza kujijengea imani kubwa miongoni mwa wananchi wenzake, na kuwaunganisha katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao bila kuangalia vyama, dini, kabila na rangi zao.

Utekelezaji wa Vipaumbele

Moja ya mambo makubwa tuliyojifunza kutoka kwa Rais wetu katika siku 100 za kwanza za Serikali yake ni umuhimu wa kupambanua na kuelekeza rasilimali zetu katika maeneo ya vipaumbele zaidi. Serikali ya Awamu ya Tano imewawezesha wananchi wote kufahamu kuwa, nchi yetu haiwezi kupiga hatua kubwa kimaendeleo, itakayotuwezesha kumaliza kero zinazotukabili na kufikia hadhi ya nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025, bila ya kuwa na vipaumbele. Si kwamba dhana ya vipaumbele ni mpya. La hasha. Tulikuwa tunaizungumzia siku zote. Lakini Rais huyu ameitekeleza kwa namna iliyovuta hisia za Watanzania na watu wengine wengi barani Afrika na duniani. Mifano ni kama ifuatavyo: 

·         Badala ya sherehe za Uhuru, tumefanya usafi ili kupambana na kipindupindu, na fedha zilizookolewa zinajenga sehemu ya barabara iliyokuwa kero kubwa kwa wananchi.
·         Badala ya Rais na Wabunge kujipongeza kwa sherehe kubwa, fedha zilizookolewa zimetatua tatizo la vitanda kwa wagonjwa.
·         Badala ya sherehe za siku ya UKIMWI, fedha zimekwenda kununua dawa za kufubaisha makali ya UKIMWI.
·         Badala ya semina elekezi ya Mawaziri, fedha zake zitakwenda kutekeleza mradi wa kufunga vifaa vya kisasa vya kuchunguza magonjwa katika hospitali 37 kote nchini.
·         Badala ya safari za nje fedha zilizookolewa zitatumika kwenye miradi ya maendeleo. Zaidi ya Sh.7 bilioni ambazo zingeweza kutumika kwa safari za nje zimeokolewa katika siku 100 na zitatumika kwenye miradi hiyo ya maendeleo.
Hatua hizo, na nyingine nyingi, zimevuta hisia za watu mbalimbali kote duniani. Mnaofuatilia mitandao ya kijamii mnajua hivyo, na wapo wameonesha wazi kutamani tungewaazima Rais wetu kwa muda.

Mapato

Katika siku 100 za kwanza Serikali imefanikiwa kuongeza makusanyo ya kodi na mapato yasiyo ya kodi. Katika kipindi cha siku 100 za kwanza, mapato ya kodi yameongezeka hadi kufikia Shilingi trilioni 3.34, ikilinganishwa na makusanyo ya Shilingi trilioni 2.59 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2014/15, ikiwa ni ongezeko la Shilingi bilioni 746.31. Hali kadhalika, kwa mapato yasiyo na kodi, makusanyo yameongezeka hadi kufikia Shilingi bilioni 281.68, kutoka Shilingi bilioni 224.03 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2014/15, ikiwa ni ongezeko la Shilingi bilioni 57.65. Nyote mmesikia, baada ya kashikashi pale Hospitali ya Taifa Muhimbili, mapato yao yameongezeka maradufu na kuwapa uwezo mkubwa zaidi wa kuhudumia wananchi. Hali ni hiyo pia kwenye Halmashauri.

Ukusanyaji huu wa mapato, umeiwezesha Serikali kugharamia baadhi ya miradi yake kwa fedha za ndani, mathalan, kuwalipa wakandarasi, kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya maji, miundombinu, umeme, kilimo, uwezeshaji wa vijana na kadhalika. Naamini kasi iliyopo sasa itaongezeka kwa siku zijazo na kutupatia uhuru zaidi wa utekelezaji wa mipango yetu. Kwa msingi huo nawasihi wananchi wadumishe uzalendo kwa kulipa kodi kwa kila bidhaa wanazonunua, kwani mapato hayo ni kwa ajili ya kuwahudumia. Pia msisite kutoa taarifa za wakwepa kodi, ambao watashughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria.

Ushirikiano na Sekta Binafsi

Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuongeza kasi ya maendeleo na ukuaji wa uchumi unaolenga kumnufaisha kila Mtanzania. Aidha, inaamini kuwa sekta binafsi ni muhimili muhimu katika kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, ukiwemo wa viwanda. Ndiyo maana, hata kabla hajaunda Baraza la Mawaziri, Mheshimiwa Rais alikutana na wafanyabiashara na wawekezaji wa sekta binafsi, katika juma la kwanza tu, baada ya kuingia madarakani ambapo, pamoja na mambo mengine, aliwahakikishia utayari na dhamira ya Serikali yake kuipa ushirikiano sekta hiyo.

Aidha, alibainisha kuwa Serikali iko tayari kuendelea kuboresha mazingira wezeshi kwa ajili ya kuongeza kasi ya uwekezaji endelevu na wenye tija kwa Serikali na Wananchi, mathalan miundombinu ya nishati, reli na barabara, viwanja vya ndege, bandari, maji, mawasiliano na upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda. Pia aliwataka wazingatie wajibu wao wa kulipa kodi na kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za nchi katika shughuli zao za uwekezaji na biashara.

Vile vile katika hizi siku 100, Rais amethibitisha nia yake ya kutoa fursa sawa kwa sekta binafsi. Ameonesha kuwa wenye fedha wasiwe na kiburi cha fedha, wakifikiri wana leseni ya kufanya watakavyo au kuonea wengine. Bali kila mfanyabiashara ambaye ni mtiifu, anayetenda haki na kufuata sheria, atamwona Rais Magufuli kuwa ni mbia wake katika kukuza uchumi wa Taifa letu.

Sera ya Mambo ya Nje

Tanzania tunajivunia msingi imara wa diplomasia na mahusiano mazuri ya kimataifa, uliowekwa na Viongozi wetu, kuanzia Awamu ya Kwanza iliyojikita katika ukombozi wa Mwafrika na jamii nyingine zinazotawaliwa duniani, hadi Awamu ya Nne iliyoendeleza diplomasia ya uchumi.

Hata hivyo, Rais wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, anatambua pia kwa nadharia ya diplomasia na mahusiano ya kimataifa inabainisha kuwa sera ya mambo ya nje inaakisi sera za ndani ya nchi. Foreign policy is an extension of domestic policy.

Tofauti na wanaomlaumu Rais kwa kutosafiri nje ya nchi, Rais wetu anafahamu na kushukuru sana kuwa Marais waliomtangulia wamefanya kazi kubwa na nzuri sana ya kujenga mahusiano yetu na nchi za nje na kuimarisha diplomasia yetu. Lakini Rais anatambua kuwa ili ailinde sifa hiyo, na kuikuza, lazima anyooshe mambo kadhaa ndani ya nchi. Iwapo Tanzania itabaki kuwa maskini, yenye rushwa, ujangili, madawa ya kulevya, na kadhalika hiyo sifa nzuri nje ya nchi itaporomoka. Hivyo ameamua kujipa muda kuimarisha uchumi na maendeleo ndani ya nchi, na kupambana na matatizo mengine yanayoharibu sifa yetu, ili iwe rahisi kudumisha sifa ya Tanzania nje ya nchi.

Wengi mtakubaliana nami kwamba hatua anazochukua Rais Magufuli kuimarisha mifumo na utendaji wa humu ndani, umeipa sifa kubwa Tanzania huko nje pamoja na kwamba yeye binafsi hajasafiri kwenda nje ya nchi tangu achaguliwe kuwa Rais. Hii inadhihirisha wazi kuwa mambo yetu ya ndani yasiposhughulikiwa ipasavyo, kusafiri tu kwa Rais nje siyo kigezo cha kudumisha heshima na urafiki mwema.

Napenda niwahakikishie wananchi wote kuwa dunia inafuatilia yanayotokea nchini, na wanashahuku ya kuona matokeo yake. Kila kona hivi sasa, nchi zinazungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano ndani ya siku 100. Hili ni jambo la kujivunia katika mahusiano yetu na nchi za nje na ni jambo kubwa kidiplomasia.Rais amefanya kazi ya kutangaza Tanzania na kujenga sifa yake bila haja ya kusafiri. Atakapokuwa tayari atasafiri tu.  




Hitimisho


Siku 100 za kwanza za Serikali ya Awamu ya Tano, zimethibitisha kuwa Serikali yetu ni makini na imedhamiria kutekeleza ahadi zake kwenu. Katika kutekeleza majukumu yake ya kuwatumikia wananchi wote, Serikali imezingatia msingi uliowekwa na serikali za awamu zilizotangulia. Na imedhamiria kutekeleza wajibu wake kwa Taifa na wananchi. Ushindi ni lazima.

Nikitakiwa kuelezea kwa maneno machache sana siku 100 za utawala wa Rais Magufuli nitasema, ametuletea aina mpya ya uongozi, unaojenga juu ya msingi wa waliomtangulia, lakini unaoweka Tanzania katika gia mpya (new trajectory) kuelekea uchumi wa kipato cha kati ulioahidiwa na Dira ya Maendeleo 2025.

Tumuunge mkono. Hapa Kazi Tu!

Asanteni kwa kunisikiliza.



Comments

Popular posts from this blog

Je, wajua kwamba Australia ni bara, nchi na kisiwa?

AMANI YETU TUILINDE NAIBU WAZIRI CHANDE AZUNGUMZA KATIKA IJITIMAI JIJINI DODOMA

UNAMKUMBUKA AMINA CHIFUPA WA MPAKANJIAA.