MKAPA NA WAPUMBAVU NA MAFALA
Haya yalikuwa matusi ya Mkapa au ya CCM?
KWA mujibu wa Kamusi ya
Kiswahili Sanifu (TUKI) toleo la tatu la mwaka 2014, maana ya neno mpumbavu ni
juha, fala, zuzu na mbumbumbu. Kwa ufupi mpumbavu ni mtu asiyetumia akili.
Na neno lofa lina maana kuwa mtu anayezururazurura asiye na kitu wala kazi.
Rais wa awamu ya tatu,
Benjamin Mkapa, juzi Jumapili alipopata wasaa wa kuhutubia maelfu ya wanachama
wa CCM waliokuwa wanazindua kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu katika viwanja
vya Jangwani Dar es Salaam, alirusha kijembe kwa wapinzani
na kusema wanaosema wanatafuta ukombozi ni wapumbavu na
malofa.
Kwamba miongoni mwa wagombea
urais wanane waliopitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), hakuna mwingine
mwenye sifa nzuri kama Dk. John Magufuli.
Kwamba haitoshi kuchukia
umaskini, bali inatakiwa mtu aeleze ni namna gani ataweza kupambana na tatizo
hilo.
Tunasema sawa; na ni vema Mkapa
kama miongoni mwa makada waandamizi wa CCM kukipigia chapuo chama chake kiweze kushinda Uchaguzi Mkuu kwa sababu kila
chama cha siasa jukumu lake kuu ni kushika hatamu za dola.
Lakini katika kujenga hoja
yake, Mkapa aliyewahi kuongoza nchi hii alitakiwa aonyeshe njia kwa kutumia
lugha yenye staha na si matusi, kwani maana ya tusi ni neno chafu la kumuudhi
mtu.
Turudi nyuma kidogo
tupate somo maridhawa. Wakati wa
uzinduzi wa kampeni za CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 katika viwanja
vya Jangwani (Dar es Salaam), Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliiasa CCM kufanya kampeni kwa
kutumia hoja kuntu (authentic) na kwa lugha nzuri na ya heshima.
Aliasa kuwa “…hata kama
Mzee Kifimbo akisema mambo ya ovyo…mnaweza mkamkosoa…mzee mtu nzima anasema mambo
ya ovyo…lakini si matusi…”. Haya yalikuwa maneno ya busara ya Mwalimu Nyerere,
mwasisi wa Taifa letu la Tanzania.
Lakini hizo zilikuwa
enzi za Mwalimu, enzi za kuheshimiana zikichagizwa na umoja wa taifa. Enzi hizi
inaonekana ni enzi za vijembe, matusi, udini na kila aina ya mmomonyoko wa
maadili katika mchakato mzima wa kampeni za kuwania nafasi mbalimbali za
uongozi nchini!
Lakini ni kitu gani
kimetufikisha hapa? Inatosha kusema tu kuwa hivi sasa nchi inakwenda arijojo,
yakiwamo matusi mbele kwa mbele katika medani ya siasa yakivihusisha vyama
vyote vya siasa, hata ndani ya Bunge! Na haya hayajaanza leo.
Katika Jimbo la Arumeru
Mashariki wakati wa kampeni za kumnadi
mgombea wa CCM, Sioi Sumari, CCM iliwatumia makada wake, wakiwamo aliyekuwa mweka
hazina, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Bunda, Stephen Wassira, Mbunge wa Mtera,
Livingstone Lusinde, Waziri Mkuu wa zamani aliyelazimika kujiuzulu, Edward
Lowassa (sasa mgombea urais kupitia Chadema) na hata Rais wa zamani wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa.
Miongoni mwa makada
hawa kuna waliojipambanua katika kuakisi siasa za bei rahisi (cheap politics),
za uongo na matusi, tena mengine ya nguoni! Lakini Lusinde ndiye aliyetia fora!
Kwa upande wake, Mkapa
aliwaita wapinzani ‘vifaranga’ na kuteleza kidogo alipolivalia njuga suala la
mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere, kuwa si wa ukoo wa Mwalimu Nyerere
badala ya kunadi sera za CCM!
Wakati Wasira akisema
kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, aliiba fedha wakati wa ziara ya
Papa John Paul wa II miaka ya 90, Lusinde alisema Dk.
Slaa alishindwa upadre akafukuzwa na kutoa matusi mengine, yakiwamo ya nguoni!
Uongozi wa Kanisa
Katoliki uliamua kutoa tamko kukanusha taarifa ya Wasira.
Ni katika mazingira
haya tunavisihi vyama vyote vya siasa vijenge hoja wakati huu na kuonyesha
vitawafanyia nini Watanzania badala ya kurusha vijembe na matusi ambayo hayana
tija kwao na kwa Taifa kwa ujumla.
Tunasema haya
yataepusha shari huko tunakokwenda ili Uchaguzi Mkuu uiache nchi ikiwa moja na
salama. Mtu mzima.......
Comments
Post a Comment