BAADHI YA WABUNGE WA CCM WAWA WATETEZI WA WAKWAPUAJI FEDHA ZA IPTL BUNGENI
BAADHI
ya wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), jana waliungana kuitetea Serikali
katika kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh 300 bilioni zilizokuwa kwenye akaunti
ya Tegeta Escrow, huku wakiiponda ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC).
Hata
hivyo wabunge wa upinzani waliendelea kusisitiza viongozi waliohusika katika
kashfa hiyo wawajibike.
Wakichangia hoja hiyo jana jioni, wabunge hao
wa CCM walisema baadhi ya mapendekezo kwenye ripoti ya PAC yametofautiana kwa
kiasi kikubwa na yale ya CAG.
Baadhi
yao walisema mjadala huo umelenga kuwachafua baadhi ya watu na kuwa hakuna
waziri atakayewajibika bali watendaji.
Wabunge
hao walihama kabisa kwenye suala la kashfa hiyo na kusema kilichopo ni jambo la
kodi tu ambalo Serikali inaweza kuifuatilia.
Mbunge
wa Mtera, Livingstone Lusinde, alisema kamwe viongozi hao hawawezi
kuwajibika kwani hakuna sehemu ambapo ripoti ya CAG imewataja kuhusika na
uchotwaji wa fedha hizo.
Alisema
huenda kamati hiyo ilikuwa na ajenda ya siri ndiyo maana ripoti yake imetoa
mapendekezo kwamba baadhi ya mawaziri akiwamo Waziri Mkuu Mizengo Pinda
wajiuzulu.
“Hapa
hakuna mtu kujiuzulu wala nini, mheshimiwa waziri mkuu endelea na mambo yako
kimyakimya, hakuna kujiuzulu hapa,” alisema Lusinde.
Mbali
na hilo, pia mbunge huyo alimshambulia Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe
akimhusisha na kupata mgawo wa fedha kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya PAP, Seth
Sigh.
“Huyu
Zitto ni mmoja wa watu ninaowaheshimu sana, na huwa spendi kumshambulia bila
sababu, lakini ninataka aliambie Bunge hili hizi fedha alizotuma watu
kuzichukua kwa Sigh zilikuwa za kazi gani.
“Maana
isiwe anataja wenzake kuchota fedha wakati na yeye alinufaika nazo,” alisema
Lusinde.
Mbunge
wa Magomeni, Zanzibar, Muhamad Chomboh (CCM), alisema: “Unajua kuna watu wana
ashki majununi, inakuWaje umma unaambiwa kitu sicho, fedha za IPTL si za umma,
naomba hili litambulike na je katika hili Waziri Mkuu anaingiaje?"
Mbunge
wa Viti Maalumu, Mariam Kisangi (CCM), alisema IPTL ilifuata utaratibu wote
ikiwamo hukumu ya mahakama.
“Barua ziliandikwa mara nne na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, sasa
hili linatoka wapi, wote tunajua katika hili la IPTL zile fedha ni zao je,
inakuwaje ajiuzulu Waziri Mkuu au Muhongo?” alisema
Kisangi.
Mbunge
wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), alieleza kushangazwa na suala la IPTL
kumhusisha Naibu Waziri Nishati na Madini, Stephen Masele huku akiitaka PAC
kuliangalia suala hilo.
“IPTL tunaambiwa kampuni feki je, na umeme wao
mbona tunautumia? Hili hapana,” alisema Ndassa.
Wakati
wabunge hao wakieleza hayo, jana wakati wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu,
kiongozi huyo wa Serikali alisema haoni sababu ya kujiuzulu.
Pinda alisema pamoja na kuwapo shauku kwa baadhi ya watu ya
kutaka jambo hilo litokee, lakini suala hilo linategemea mipango ya Mungu ya
kuwa ndiyo au hapana.
Kauli hiyo aliitoa kutokana na swali aliloulizwa na Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Katika swali lake, Mbowe alisema kwa kuwa Pinda ni kiongozi wa
shughuli za Serikali bungeni, je haoni sababu ya kujiuzulu ili kupisha watu
wengine wenye uwezo ili wamalizie ngwe iliyobaki ya uongozi.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema pamoja na hali hiyo alimtaka
Mbowe kutambua kuwa angeweza kufanya hivyo, lakini haoni sababu.
“Mheshimiwa spika, inawezekana mheshimiwa Mbowe una shauku ya
kutaka litokee hilo, lakini mambo haya yanategemea kama ndivyo Mungu kapanga au
hapana.
“Najua umeingiza mambo
mengi sana kwenye jambo hili, lakini kubwa ni hilo ulilomaliza nalo. Ningeweza
nikajaribu kujibu, lakini sina sababu ya kufanya hivyo.
“Sina sababu ya kufanya hivyo kwa sababu suala lenyewe ndiyo
Subject (mada) ya mjadala hapa bungeni ambao unaanza leo (jana),” alisema
Pinda.
Kafulila
Mbunge
wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alisema aliyekuwa Waziri wa
Fedha, Basili Mramba aliisababishia hasara Serikali ya Sh bilioni 11 na kwa
sasa yuko mahakamani, hivyo haiwezekani watu wengine waliofanya udadali na
kuisababishia hasara Serikali ya zaidi ya Sh bilioni 21 waachwe.
Akichangia
mjadala wa taarifa ya PAC kuhusu kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300
kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, Kafulia alisema haiwezekani maendeleo ya
Watanzania yakwame kwa sababu ya watu wachache.
Alisema mmiliki wa PAP iliyonunua mtambo wa kufua umeme
wa IPTL, Seth Sigh anaweza kuiangusha CCM kama alivyokiangusha chama tawala cha
KANU nchini Kenya katika kashfa ya Goldenberg.
Kafulila
alisema Sigh alikuwa miongoni mwa waliohusika katika kashfa hiyo iliyokitikisa
Serikali ya chama cha KANU.
Alisema
kwa sasa jambo ambalo linaumiza vichwa vya wengi ni kwamba fedha hizo ni za
umma au za IPTL.
“Hasara tuliyopata ni zaidi ya fedha za
Escrow, hasara ya kwanza ni MCC, hasara ya pili nchi wahisani kupitia bajeti
wamegomea dola milioni 500. Katika MCC 1/3 ilikuwa miradi ya umeme, lakini
tumepoteza.
“Kwenye
hoja hii kinachoumiza vichwa vya wengi ni kwamba fedha ni za umma au za IPTL?
Tukumbushane, waziri wa nishati wa madini alikuwa akisisitiza kuwa fedha
zilitolewa kwa hukumu ya Jaji Utamwa, nilivyohoji nikaitwa tumbili.
“Hukumu
hii hapa kwenye karatasi na hamna sehemu iliyosema fedha hizi ni za Escrow, leo
Profesa Muhongo anasema ni kikao cha Kunduchi Beach Hotel cha Oktoba 8 mwaka
jana na si hukumu.
“Hatusemi
kuwa Muhongo hana mazuri aliyoifanyia
nchi hii, lakini kwenye wizi sheria iko pale pale.
“Hawa
jamaa wamekula fedha za Escrow pamoja na VAT, madalali wa wizara ya nishati
wamesababisha hasara ya Sh bilioni 21 ambazo zote zimeliwa,” alisema Kafulila.
Aidha
mbunge huyo ambaye ndiye alishinikiza sakata hilo bungeni na hatimaye Serikali
ikakubali uchunguzi kufanywa, alieleza kushangazwa kwa kitendo cha Profesa
Muhongo kuendelea kung’ang’ania kuwa masuala hayo yako sahihi na fedha
zilizochotwa ni za watu binafsi.
Mbowe
Akichangia
mjadala wa kikao cha jioni, Mbowe
alisema ingawa wabunge wa CCM wameamua kulikumbatia suala hilo, Watanzania
watajua na litakuja kuwahukumu.
Alisema
kuna ushahidi wa wazi kuwa waziri mkuu aliwajibika juu ya suala hilo na kwa
nafasi yake angepaswa kulishughulikia.
“Mtafunika
jambo hili mwanaharamu apite, lakini hukumu ipo. Jambo hili limeivua Serikali
nguo,” alisema.
Muhongo: Fedha za Escrow si
za Serikali
Awali akitoa utetezi wa
Serikali juu ya kashfa hiyo, Waziri
Muhongo aliendelea kusisitiza kwamba fedha zilizokuwa katika akaunti ya
Tegeta Escrow si za umma bali ni za watu binafsi.
Profesa Muhongo alisema
fedha hizo ni mali ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania
Limited (IPTL), ambapo kama wakala wa kodi anastahili kudaiwa na mwisho kulipa
kodi yote ambayo hajalipa.
Akizungumza bungeni jana
kujibu hoja za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Profesa
Muhongo alisema Tanesco ilikuwa inapata huduma ya umeme bila kulipa moja kwa
moja IPTL, lakini ikawa inapeleka fedha hizo katika Akaunti ya Escrow.
“Tanesco ilisimamisha
kupeleka malipo kwenye Akaunti ya Escrow na wala kulipa IPTL kuanzia Oktoba 30,
mwaka 2010 lakini pamoja na kutokulipa, Tanesco iliendelea kupata huduma ya
umeme kwa kadiri ilivyohitaji kutoka IPTL.
“Kulingana na taarifa hiyo
ukurasa wa 36 hadi 42 imeonyesha kiasi ambacho kilipaswa kuwekwa kwenye Akaunti
ya Escrow kwa mujibu wa ankara za IPTL ni shilingi bilioni 306.68. Hata hivyo,
kwa mujibu wa ukaguzi huo fedha zilizokuwa kwenye akaunti wakati wa kuifunga ni
Sh bilioni 182.77 na kuwa na upungufu wa
Sh bilioni 123.90 ikiwa ni deni ambalo Tanesco bado wanadaiwa na IPTL.
“Kwa msingi huo, taarifa ya PAC haisemi ukweli
kuhusu fedha zilizowekwa katika Akaunti ya Escrow kuwa ni fedha za umma, na ili
kuthibitisha kwamba fedha hizi siyo za umma, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG) katika ukaguzi wake wa hesabu za Tanesco wa Desemba 31, mwaka
2012, alielekeza kutoa fedha za Escrow kwenye vitabu vya hesabu vya Tanesco na
kupunguza deni kwa kiasi hicho hicho,” alisema.
Alisema taarifa ya PAC
imeeleza kwa mujibu wa mkataba wa PPA, Tanesco na IPTL walipaswa kutumia
mtaalamu wa upatanishi katika mgogoro wa gharama za uendeshaji.
Comments
Post a Comment